
-Lengo ni kurahisisha huduma za uagizaji na usafirishaji wa bidhaa kwenda nje ya nchi
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
CHAMA cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA) kimetangaza kuanza kutumika kwa mfumo wa kielektroniki utakaosaidia utekelezaji shughuli za uingizaji bidhaa nchini na usafirishaji wa bidhaa kwenda nje ya nchi kuanzia Agosti Mosi, 2026.
Kwa mujibu wa TAFFA, mfumo huo umeunganishwa na Tanzania Electronic Single Window (TANESW) kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma kwa njia ya kielektroniki, kuongeza uwazi na kuboresha ufanisi katika shughuli za uwakala wa forodha.
Mfumo huo utatumika katika shughuli za uingizaji bidhaa nchini, usafirishaji wa bidhaa kwenda nje ya nchi pamoja na mizigo ya transit inayopita Tanzania Bara kuelekea nchi jirani, isipokuwa bidhaa au huduma zilizosamehewa kwa mujibu wa GN Na. 83 ya mwaka 2026.
TAFFA imeeleza kuwa utekelezaji utaanza kwa awamu ya majaribio kwa kushirikisha baadhi ya kampuni za uwakala wa forodha kabla ya kuanza kutumika rasmi kwa wadau wote.
Chama hicho kimewataka wanachama na wadau wa biashara kujiandaa mapema kwa matumizi ya mfumo huo na kufuatilia taarifa rasmi kuhusu usajili, mafunzo na taratibu za matumizi kupitia njia rasmi za TAFFA.