
-Licha ya kulipwa Sh. bilioni 33, kasi ya utekelezaji wa mradi bado hairidhishi
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati kutomuongezea muda wa mkataba Mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 220 kutoka Songea hadi Tunduru kupitia Masasi wenye urefu wa kilomita 214.5, pamoja na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme katika Wilaya ya Tunduru.
Waziri Ndejembi ametoa maagizo hayo wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma, baada ya kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya Kalpataru, ambayo imeshindwa kutekeleza mradi kwa mujibu wa mkataba licha ya Serikali kufanya malipo yake.
“Mkataba wake unaisha mwezi wa tisa, lakini kama mnavyojionea hana wafanyakazi wa kutosha site kwa ajili ya kukamilisha kazi hii. Namtaka Katibu Mkuu kuhakikisha kuwa mkandarasi huyu haongezewi hata siku moja,” amesema Waziri Ndejembi.
Waziri Ndejembi ameeleza kuwa miezi mitatu iliyopita alipotembelea mradi huo, mkandarasi alikuwa amesimamisha kazi akieleza kuwa changamoto ilikuwa ni malipo, hata hivyobaada ya ziara hiyo Serikali ilimlipa shilingi bilioni 33, lakini pamoja na kulipwa fedha hizo kasi ya utekelezaji bado hairidhishi.
Ameeleza kuwa pindi muda wa mkataba utakapomalizika tarehe 30 Septemba, 2026, Serikali itaanza kuchukua hatua za kisheria kwa mujibu wa mkataba dhidi ya mkandarasi huyo, ikiwemo kumtoza liquidated damages kwa kushindwa kukamilisha mradi kwa wakati.
Ndejembi amesema utekelezaji wa mradi huo, ambao umefikia asilimia 51, ni sehemu ya mpango mkakati wa Serikali wa kuhakikisha mikoa ya Lindi na Mtwara inaunganishwa kwenye Gridi ya Taifa ili kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa kutosha.
Aidha, Waziri Ndejembi amesema licha ya mkandarasi huyo kuongezewa muda wa utekelezaji hapo awali, ambao unaisha Septemba 2026, ameomba kuongezewa muda tena, jambo ambalo Serikali haikubaliani nalo.
Ameeleza kuwa hali halisi ya utekelezaji wa mradi inaonesha mkandarasi huyo hajawasilisha mpango kazi unaoweza kuthibitisha kuwa atakamilisha mradi kwa wakati, Kutokana na hali hiyo Serikali imeamua kuanza taratibu za kumchukulia hatua za kisheria kwa mujibu wa mkataba.






