NBC yakabidhi kombe la ubingwa wa Ligi ya Vijana (U20) kwa Azam FC


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam


BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) na Mdhamini Mkuu wa Ligi ya NBC Vijana chini ya Miaka 20 (NBC U20 Youth League), imekabidhi rasmi kombe la ubingwa wa msimu wa 2025/26 kwa Azam FC (U20) baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Yanga SC (U20) katika mchezo wa fainali uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Chamazi Complex, jijini Dar es Salaam.


Kabla ya mchezo huo wa fainali, Mbeya City FC (U20) ilitwaa nafasi ya tatu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 kwa mikwaju ya penalti dhidi ya JKT Tanzania (U20), kufuatia timu hizo kutoka sare katika muda wa kawaida.


Hafla ya kukabidhi kombe hilo iliongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Wajasiriamali, Vijana na Wanawake wa Benki ya NBC, Gaudence Shawa, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Theobald Sabi.


Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa soka nchini akiwamo Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Nassor Idrissa, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Oscar Milambo, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Lameck Nyambaya, viongozi wengine wa TFF pamoja na Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa, Taifa Stars, Miguel Gamondi.


Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Shawa aliwapongeza mabingwa Azam FC (U20), washindi wa pili Yanga SC (U20), washindi wa tatu Mbeya City FC, vilabu vyote vilivyoshiriki, mabenchi ya ufundi na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kufanikisha msimu ulioonyesha kiwango cha juu cha ushindani na maendeleo makubwa ya kiufundi.


“NBC tunaamini kwamba mafanikio ya soka la kulipwa huanzia kwenye uwekezaji madhubuti katika maendeleo ya vijana. Ndiyo sababu tuliamua kuwa sehemu ya safari hii ya kujenga kizazi kipya cha wachezaji wenye uwezo wa kuleta ushindani mkubwa katika Ligi Kuu ya NBC, NBC Championship na hatimaye kuiwezesha Tanzania kuwa na timu za taifa zenye ushindani wa kimataifa.


“Tunafurahishwa kuona kiwango cha ushindani na ubora wa soka katika ligi hii vinaendelea kuimarika kila msimu, jambo linalotupa imani kuwa uwekezaji huu unaendelea kuleta matokeo chanya,” alisema Shawa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa DRFA, Lameck Nyambaya, aliipongeza NBC kwa kuendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo ya soka nchini kupitia uwekezaji wake katika ligi za vijana.


Alisema mashindano ya msimu huu yameonesha mabadiliko makubwa katika ubora wa kiufundi, nidhamu ya mchezo na ushindani miongoni mwa timu zilizoshiriki, hali inayodhihirisha kuwa juhudi zinazowekwa katika kukuza soka la vijana zinaendelea kuzaa matunda.


“Tunashuhudia ongezeko kubwa la ubora wa wachezaji na ushindani kutoka klabu mbalimbali. Hii ni ishara kuwa Tanzania ipo kwenye mwelekeo sahihi wa kujenga msingi imara wa maendeleo ya soka kuanzia ngazi ya vijana. Tunatoa pongezi kwa NBC kwa kuona umuhimu wa kuwekeza katika eneo hili muhimu ambalo ndilo chimbuko la mafanikio ya soka letu,” alisema Nyambaya.

WhatsApp-Image-2026-07-02-at-07.15.22-1024x684 NBC yakabidhi kombe la ubingwa wa Ligi ya Vijana (U20) kwa Azam FC

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Nassor Idrissa (katikati) na Mkuu wa Kitengo cha Wajasiriamali, Vijana na Wanawake wa Benki ya NBC, Gaudence Shawa (kulia – alievaa suti) wakikabidhi kombe la Ligi ya NBC ya Vijana chini ya miaka 20 (NBC U20 Youth League) kwa nahodha wa timu ya Azam FC (U20) Rajabu Somvi baada ya timu hiyo kuwa bingwa wa ligi hiyo kwa msimu wa 2025/2026. (Picha: Mpigapicha Wetu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *