Juhudi za uhifadhi zachangia ongezeko la idadi ya wanyapori nchini

WhatsApp-Image-2026-06-17-at-06.40.13-1024x870 Juhudi za uhifadhi zachangia ongezeko la idadi ya wanyapori nchini

Na Mwandishi Wetu, Arusha

JUHUDI za usimamizi na ulinzi wa Wanyamapori nchini zinazofanywa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) zimechangia mafanikio makubwa ya ongezeko la wanyamapori yaliyoainishwa katika takwimu zilizowasilishwa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) katika uzinduzi wa matokeo ya sensa ya Kitaifa ya Wanyamapori uliofanyika leo Juni 17, 2026 jijini Arusha.

Sensa hiyo ya wanyamapori iliyofanyika kwa mwaka 2024/2025 imebainisha idadi na mwenendo chanya wa wanyamapori nchini kwa kipindi cha muongo mmoja (Miaka 10), sambamba na ongezeko la asilimia 10% ya maeneo ya kiikolojia yaliyofikiwa ambapo mwaka 2014/2015 eneo la 297,224 Kilomita za mraba na 2024/2025 eneo la 340,748 Kilomita za mraba yalifanyiwa sensa ya wanyamapori sawa na ⅓ ya eneo la nchi nzima.

Akizungumza katika hotuba yake Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Dkt. Ashatu Kijaji(Mb) alieleza kuwa Tanzania inaongoza barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya nyati wapatao 324,437 na simba wapatao 17,200.

Aidha, Tanzania ipo katika nafasi ya tatu barani Afrika kwa kuwa na tembo 66,700 na nafasi ya nne kwa idadi ya faru weusi na weupe wapatao 302, takwimu zinazothibitisha juhudi kubwa zinazofanywa na mamlaka za uhifadhi nchini (NCAA, TANAPA,TAWA na TFS) katika kuboresha ulinzi wa wanyampori unaochangia kukua kwa utalii duniani.

Vilevile, aliongeza kuwa shughuli holela za kibinadamu ikiwemo kilimo, uvuvi na ufugaji zimekuwa na athari za moja kwa moja katika kubadili ikolojia ya wanyamapori nchini.

“Pamoja na mwenendo chanya uliobainika wa ongezeko la wanyamapori, pia sensa hii imebaini uwepo wa shughuli za kibinadamu kama viashiria hatarishi katika maeneo mbalimbali yenye wanyamapori. Changamoto hizi huathiri ustawi wa mifumo ikolojia, wanyamapori na maendeleo ya utalii” alisema Dkt. Kijaji.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe.Timotheo Mzava (Mb), alieleza kuwa takwimu hizo za kisayansi zitatumika kusimamia uhifadhi endelevu na kuendesha mijadala mikubwa ndani ya bunge itakayotoa mstakabali wa usalama wa wanyamapori na wananchi wanoishi pembezoni mwa maeneo ya hifadhi.

Awali, akiwasilisha takwimu za matokeo ya sensa hiyo Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) Dkt.Eblate Mjingo alieleza kuwa matokeo yanaonesha uwepo wa spishi 28 za wanyamapori wa kimo cha kati na wakubwa katika mifumo yote ya ikolojia na kuimarika kwa idadi ya wanyamapori ikilinganishwa na miaka 10 iliyopita.

Wanyama walioongezeka ni pamoja na Tembo, Nyati, Faru, Simba, Twiga, Nyumbu na Tandala huku Hifadhi za Taifa Serengeti, Ruaha, Nyerere, Mikumi, Tarangire na Katavi zikiwa vinara kwa idadi kubwa ya wanyama katika takwimu za sensa hiyo.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ikiwemo Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Wakuu wa Wilaya, Makamishna wa Uhifadhi na wawakilishi kutoka TANAPA, TFS, NCAA, TAWA, viongozi wa kisiasa na wadau wa utalii.

WhatsApp-Image-2026-06-17-at-06.40.18-1024x683 Juhudi za uhifadhi zachangia ongezeko la idadi ya wanyapori nchini
WhatsApp-Image-2026-06-17-at-06.40.19-1024x683 Juhudi za uhifadhi zachangia ongezeko la idadi ya wanyapori nchini
WhatsApp-Image-2026-06-17-at-06.40.20-1024x683 Juhudi za uhifadhi zachangia ongezeko la idadi ya wanyapori nchini
WhatsApp-Image-2026-06-17-at-06.40.21-1024x683 Juhudi za uhifadhi zachangia ongezeko la idadi ya wanyapori nchini
WhatsApp-Image-2026-06-17-at-06.40.22-1024x683 Juhudi za uhifadhi zachangia ongezeko la idadi ya wanyapori nchini
WhatsApp-Image-2026-06-17-at-06.40.22-1-1024x683 Juhudi za uhifadhi zachangia ongezeko la idadi ya wanyapori nchini

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *