Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WASICHANA wanachangia asilimia 77.7 ya maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) yanayotokea miongoni mwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24, hali inayohitaji kuimarishwa kwa juhudi za kuwakinga na kuwawezesha kupata elimu sahihi kuhusu afya zao.
Aidha, kundi hilo la vijana linachangia asilimia 33.3 ya maambukizi yote mapya ya VVU.

Takwimu hizo zinadhihirisha umuhimu wa kuweka mkazo zaidi katika mikakati ya kinga, upimaji na utoaji wa elimu kwa vijana, hususan wasichana.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi aliyasema hayo leo, Novemba 19,2026 wakati akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kuhusu maadhimisho ya Siku ya UKIMWI duniani 2026, yanayotarajiwa kufanyika Disemba Mosi mwaka huu.

Amesema takwimu hizo zinapaswa kuwa changamoto kwa jamii, viongozi na wadau wote kuongeza ushiriki katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.
Prof. Kabudi amesema takwimu hizo zinaiweka jamii katika wajibu wa kuongeza juhudi za kuwafikia vijana kwa elimu sahihi, huku akisisitiza kuwa kila mmoja anapaswa kuwajibika katika kujikinga na VVU na kujua hali yake ya maambukizi.

“Pia, ninatoa wito kwa kila mmoja wetu, hususan vijana, kuwajibika katika kujikinga na VVU, kujua hali yake ya VVU na kushiriki katika kutoa elimu sahihi kwa jamii,” amesema.
Katika hotuba hiyo, Prof. Kabudi amesema Serikali ina dhamira ya kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma katika juhudi za kutokomeza UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030.
Amesema Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika mapambano hayo kwa kuhakikisha huduma za kinga, upimaji na matibabu zinapatikana na kuwafikia wananchi wote.

Amesisitiza pia umuhimu wa kuondoa unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya watu wanaoishi na VVU, akieleza kuwa mapambano hayo yanahitaji jamii yenye upendo, mshikamano na inayoheshimu utu wa kila mmoja.
“Napenda kuwasisitiza Watanzania kuwa tusimnyanyapae wala kumbagua mtu anayeishi na VVU,” amesema na kuongeza kuwa jamii inapaswa kuwapa watu wote nafasi ya kuishi kwa utu na kushiriki katika maendeleo ya Taifa.