Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezitaka nchi za Afrika Mashariki kuimarisha ushirikiano katika kukuza sekta ya viwanda badala ya kushindana, akisisitiza umuhimu wa kujenga minyororo ya thamani ya kikanda ili kuongeza uzalishaji na kuimarisha ushindani katika masoko ya kimataifa.
Rais Samia amesema uwekezaji wa viwanda katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unapaswa kukamilishana na kusaidiana ili kuongeza ajira, kuhamisha teknolojia na kuimarisha uchumi wa kikanda.
Ametoa kauli hiyo Novemba 19, 2026 nchini Uganda wakati akihutubia hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha kuunganisha magari cha Double Q Motors, akisisitiza kuwa Afrika Mashariki inapaswa kubadilika kutoka kuwa eneo linalotegemea bidhaa zinazoagizwa kutoka nje na badala yake kuwekeza katika uzalishaji wa ndani.
“Tunapaswa kuwa na dhamira ya kutengeneza, kuunganisha na kuzalisha bidhaa badala ya kuwa watumiaji wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje,” amesema.
Aidha, Rais Samia amesisitiza umuhimu wa kuwa na kanuni zinazofanana katika shughuli za kuunganisha na kutengeneza magari katika nchi za Afrika Mashariki, akieleza kuwa hatua hiyo itarahisisha uwekezaji, kuimarisha minyororo ya thamani ya kikanda na kuchochea maendeleo ya viwanda pamoja na sekta nyingine za uchumi.








