*Serikali yaweka mkakati wa 2030
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI imeweka mkakati wa kuingiza tiba asili katika mfumo rasmi wa huduma za afya nchini ifikapo mwaka 2030, kufuatia tafiti zinazoonesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wanatumia tiba hizo.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wanapata dawa salama, zenye ubora na kuthibitishwa kisayansi.

Mkakati huo unalenga kuimarisha tafiti, ubunifu, uzalishaji wa dawa za tiba asili na uwekezaji katika viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini, huku Serikali ikikusudia pia kuwezesha tiba hizo kutambuliwa katika mifumo ya bima ya afya kwa wote.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, ameyasema hayo leo Novemba 19,2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya Dhifa ya Uwekezaji katika Dawa za Tiba Asili (Asili Investment Gala 2027), inayotarajiwa kufanyika Aprili 2027.
Amesema Serikali inalenga kuhakikisha tiba asili inatambuliwa na kuingizwa katika mifumo ya afya kuanzia ngazi ya msingi hadi taasisi za kitaifa, huku dawa zinazotumiwa na binadamu zikipitia taratibu za uthibitishaji na kupata ushahidi wa kisayansi kuhusu usalama na ufanisi wake.

“Moja ya harakati kubwa ambazo tunaendelea nazo sasa ni pamoja na kuijumuisha pia katika bima ya afya kwa wote, lakini kuhakikisha kwamba mifumo yetu yote ya afya inatambua tiba asili,” amesema Mchengerwa.
Amesema lengo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 tiba asili inakuwa sehemu ya mfumo rasmi wa huduma za afya nchini, kwa kuzingatia sera na taratibu zilizowekwa katika sekta ya afya.
Mchengerwa amesema pamoja na kuwepo kwa dawa za tiba asili zilizosajiliwa, bado zipo nyingine ambazo hazijapitia taratibu rasmi za Serikali, hivyo ni muhimu kwa wadau kurasimisha bidhaa zao ili ziweze kufanyiwa tathmini na kuthibitishwa kisayansi.
Amesema dhifa hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwa na lengo la kuhamasisha uwekezaji na ushirikiano katika tafiti, ubunifu, uzalishaji wa dawa na kujenga uwezo wa rasilimali watu.
Amesema kaulimbiu ya dhifa hiyo ni ‘Wekeza katika dawa zetu za ndani za tiba asili,’ inayolenga kuhamasisha wadau kutambua, kuthamini na kutathmini rasilimali za tiba asili zilizopo nchini ili kukuza tafiti, ubunifu na uzalishaji wa viwandani.
Kwa mujibu wa Mchengerwa, uwekezaji huo unatarajiwa kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa bidhaa za afya, sambamba na Mpango Mkakati wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wa Tiba Asili wa mwaka 2025–2034.
Amesema mpango huo wa WHO unasisitiza ujumuishaji wa tiba asili zenye ushahidi wa kisayansi, ufanisi, usalama na ubora katika mifumo ya afya.
Ametaja matokeo yanayotarajiwa katika dhifa hiyo ni upatikanaji wa dawa za tiba asili za kutibu magonjwa ya kipaumbele zenye ushahidi wa kisayansi, kuimarika kwa uwezo wa kitaifa wa kufanya tafiti na kujengwa kwa viwanda vya dawa vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini.
Aidha, amesema mpango huo utajumuisha mafunzo kwa watoa huduma za afya ili kuwawezesha kuelewa na kutumia ipasavyo mfumo wa tiba asili utakaotambuliwa rasmi, hatua itakayosaidia kuimarisha usalama wa wagonjwa.

Ameongeza kuwa uwekezaji katika sekta hiyo utafungua fursa za kiuchumi kupitia mnyororo wa uzalishaji wa dawa za tiba asili, ikiwemo kilimo cha mimea tiba na uchakataji wa kisasa wa malighafi.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza ajira kwa vijana, kukuza uzalishaji wa ndani na kuongeza pato la Taifa.