Na Benny Mwaipaja, Paris, Ufaransa
Waziri wa Fedha wa Tanzania, Balozi Khamis Musa Omar (Mb), amesema changamoto kubwa inayozikabili nchi nyingi za Afrika katika kupata fedha za maendeleo si ukosefu wa mitaji, bali ni uhaba wa miradi iliyoandaliwa vizuri na inayoweza kuvutia uwekezaji na kufadhiliwa kupitia masoko ya mitaji na dhamana.
Amesema hayo jijini Paris, Ufaransa, wakati akichangia mjadala kuhusu Usanifu Mpya wa Kifedha wa Afrika kwa Maendeleo (NAFAD), unaolenga kutafuta njia mbadala za kuongeza fedha za kutekeleza miradi ya kimkakati ya maendeleo barani Afrika.
Balozi Omar amesema Afrika ina rasilimali kubwa za kifedha, zikiwemo akiba za ndani za muda mrefu zinazokadiriwa kufikia dola za Marekani trilioni nne, lakini sehemu kubwa ya fedha hizo bado haijaelekezwa ipasavyo katika uwekezaji wa uzalishaji, huku bara hilo likikabiliwa na pengo la ufadhili wa maendeleo linalozidi dola za Marekani bilioni 400 kwa mwaka.
Amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuwekeza katika maandalizi ya miradi ili kuhakikisha inakuwa na sifa zinazokidhi vigezo vya ufadhili wa kibiashara na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya bara hilo.
Akizungumzia matumizi ya akiba za ndani, hususan fedha za mifuko ya pensheni na bima, Waziri huyo amesema taasisi hizo zina wajibu wa kulinda fedha za wanachama na mara nyingi hupendelea uwekezaji wa muda mfupi wenye hatari ndogo. Hivyo, amesisitiza kuwa matarajio ya kutumia akiba hizo kufadhili miradi mikubwa yanapaswa kuzingatia uwezo na mazingira ya masoko ya kifedha, hasa katika nchi zenye masoko madogo.
Katika hatua nyingine, amesisitiza umuhimu wa kudhibiti vihatarishi vya kifedha vinavyoweza kusababishwa na madeni ya dharura, ikiwemo dhamana zinazotolewa na Serikali, akitaka dhamana zote zisajiliwe na kuingizwa katika taarifa za madeni na fedha za umma ili kuimarisha uwazi na usimamizi wa madeni.
Aidha, amependekeza matumizi ya viwango vya uwezo wa nchi kulipa madeni vinavyotolewa na mashirika ya kimataifa kama Moody’s na Fitch katika kuamua bei ya dhamana zinazotolewa katika masoko ya kimataifa.
NAFAD inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za kifedha za kitaifa na kikanda, benki za biashara, mifuko ya pensheni, kampuni za bima, masoko ya mitaji, Serikali na wawekezaji binafsi ili kutumia vizuri rasilimali zilizopo na kuongeza fedha zinazowekezwa katika miradi ya maendeleo.
Mjadala huo umefanyika pembezoni mwa Jukwaa la 25 la Kimataifa la Uchumi kwa ajili ya Afrika, lililoandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kushirikiana na Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD), ukiwa na lengo la kujadili namna ya kuimarisha mfumo wa kifedha wa Afrika na kuelekeza mitaji katika vipaumbele vya maendeleo ya bara hilo.

Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar akizungumza jijini Paris nchini Ufaransa, wakati akichangia mada kuhusu Usanifu Mpya wa Kifedha wa Afrika kwa Maendeleo (NAFAD), kama chanzo mbadala cha fedha za kutekeleza miradi ya kimkakati ya maendeleo katika nchi za Bara la Afrika, ulifanyika kando ya Jukwaa la 25 la Kimataifa la Uchumi kwa ajili ya Afrika, ulioandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Ushirikino wa Kiuchumi na Maendeleo la Ufaransa-OECD, ukilenga kuimarisha mfumo wa kifedha wa Afrika ili mitaji ielekezwe kwa ufanisi zaidi katika vipaumbele vya maendeleo ya Bara la Afrika.

Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar akizungumza jijini Paris nchini Ufaransa, wakati akichangia mada kuhusu Usanifu Mpya wa Kifedha wa Afrika kwa Maendeleo (NAFAD), kama chanzo mbadala cha fedha za kutekeleza miradi ya kimkakati ya maendeleo katika nchi za Bara la Afrika, ulifanyika kando ya Jukwaa la 25 la Kimataifa la Uchumi kwa ajili ya Afrika, ulioandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Ushirikino wa Kiuchumi na Maendeleo la Ufaransa-OECD, ukilenga kuimarisha mfumo wa kifedha wa Afrika ili mitaji ielekezwe kwa ufanisi zaidi katika vipaumbele vya maendeleo ya Bara la Afrika. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WF, Paris-Ufaransa)