Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
ZIARA za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Uganda na Ethiopia zimefungua fursa mpya kwa Watanzania katika ajira, biashara, uwekezaji, viwanda na mafunzo ya kitaalamu, huku zikitarajiwa kuimarisha nafasi ya Tanzania katika uchumi na maendeleo ya afya barani Afrika.
Fursa hizo zinatokana na makubaliano ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Uganda, yakiwemo maendeleo ya miradi ya nishati, reli, bandari na biashara, pamoja na mpango wa Umoja wa Afrika wa kuboresha afya ya mama na mtoto utakaotekelezwa katika nchi zote 55 za Umoja huo kuanzia mwaka 2026 hadi 2030.

Akizungumza kuhusu manufaa ya ziara hizo Novemba 24,2026 Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu, alisema ziara ya Uganda iliyofanyika Novemba 18 na 19, mwaka huu, ililenga kufungua fursa za kiuchumi, wakati ile ya Ethiopia ya Novemba 22 na 23 ililenga kuimarisha uongozi wa Tanzania katika ajenda ya afya ya mama na mtoto barani Afrika.
Katika ziara ya Uganda, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema moja ya fursa kubwa ni mpango wa kuifanya Tanga kuwa kitovu cha nishati Afrika Mashariki, kupitia uwekezaji katika miundombinu ya kuhifadhi, kusafirisha na kusambaza mafuta, pamoja na uzalishaji wa mbolea, plastiki na kemikali za viwandani.

Amesema uwekezaji huo utafungua ajira kwa vijana katika ujenzi, uhandisi, uendeshaji wa mitambo, matengenezo na huduma za usafirishaji, huku wajasiriamali wakipata nafasi za kusambaza bidhaa na huduma.
Amesema pia kukamilika kwa mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 93.9, kutafungua fursa katika uendeshaji, matengenezo, usalama, usafirishaji na huduma za ugavi katika maeneo yanayopitiwa na bomba hilo.

Aidha, reli ya kisasa itakayounganisha Tanzania na Uganda kupitia Isaka, Lusahunga, Murongo, Kikagati hadi Mpondwe yenye urefu wa kilomita 620, inatarajiwa kuongeza biashara kupitia Bandari ya Dar es Salaam na kupanua ajira katika ujenzi, uhandisi, uendeshaji na matengenezo ya reli.
Kwa upande wa usafiri wa majini, makubaliano ya kuboresha Bandari ya Port Bell nchini Uganda na kuimarisha muunganiko wa reli ya MGR kutoka bandari hiyo hadi Kampala yanatarajiwa kuongeza usafirishaji wa mizigo kupitia Ziwa Victoria.

Hatua hiyo itafungua fursa kwa vijana wa Mwanza na Kanda ya Ziwa katika shughuli za bandari, huduma za meli, usafirishaji, ugavi, biashara na utalii.
Pia, kuanzishwa kwa kamati ya pamoja ya biashara kati ya nchi hizo kutasaidia kushughulikia vikwazo vinavyowakabili wafanyabiashara na kupanua masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini.

Katika eneo la nishati, makubaliano ya kuunganisha mifumo ya umeme ya kilovolti 400 kupitia Wobulenzi, Masaka, Ibadakuli hadi Shinyanga yanatarajiwa kuimarisha uhakika wa upatikanaji wa umeme na kuchochea shughuli za viwanda na uzalishaji.
Prof. Mbarawa amesema mafanikio hayo yatatoa nafasi kwa vijana kushiriki katika ajira za kiufundi, biashara, ujasiriamali na utoaji wa huduma, akiwataka kujiandaa kutumia fursa hizo kwa kuongeza ujuzi na uwezo wa kufanya biashara.

Katika ziara ya Ethiopia, fursa nyingine zimefunguliwa kupitia mpango elekezi wa kuboresha afya ya mama na mtoto barani Afrika wa mwaka 2026–2030 uliozinduliwa na Rais Samia Novemba 23, mwaka huu.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema hatua za awali za utekelezaji wa mpango huo zinahusisha nafasi 60 za mafunzo ya ubobezi kwa wataalamu wa afya, katika maeneo ya ukunga, magonjwa ya wanawake na uzazi, ganzi na huduma za watoto wachanga.

Amesema nafasi hizo zinaweza kuongezeka hadi 100 na hata 200 kadiri wadau watakavyowezesha.
Akieleza fursa kwa Watanzania, Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Bruno Sunguya, amesema ukinara wa Rais Samia katika ajenda hiyo utawezesha wataalamu na vijana kushiriki katika kubadilishana uzoefu, programu za afya, tafiti za kisayansi na mafunzo, huku taasisi za ndani zikipata nafasi ya kushirikiana na nchi nyingine za Afrika.

Ameongeza kuwa sekta binafsi itapata fursa za uwekezaji katika dawa, vifaa tiba, bidhaa za afya, teknolojia za kidijitali na mifumo ya usafirishaji wa wagonjwa, hatua inayoweza kupanua ajira na kukuza ubunifu.
Prof. Sunguya amesema vijana wanapaswa kutumia nafasi hiyo kushiriki katika uongozi, maamuzi, utafiti na ubunifu wa teknolojia zinazoweza kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, badala ya kujiona kama walengwa wa huduma pekee.

Kwa ujumla, ziara hizo zimeweka msingi wa fursa zinazogusa sekta mbalimbali za uchumi na huduma za jamii, huku mafanikio yake yakitegemea utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa na ushiriki wa Watanzania katika kuzitumia fursa hizo.