Antalya, Turkiye
MEYA wa Jiji la Dar es Salaam, Nurdin Bilal Juma (Shetta), ametangaza mkakati wa jiji hilo wa kupunguza uchafuzi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuimarisha usimamizi wa taka kupitia mfumo wa uchumi wa mzunguko (Circular Economy), unaolenga kuzigeuza taka kuwa rasilimali zenye manufaa kwa jamii na uchumi.
Akizungumza katika Mkutano wa Mameya wa Mtandao wa C40 Cities uliofanyika sambamba na Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), jijini Antalya, Türkiye, Meya alisema mkakati huo unalenga kuachana na mfumo wa kawaida wa kukusanya na kutupa taka na badala yake kuzitumia kama rasilimali zinazoweza kuchakatwa na kutumika tena.

Katika mkutano huo, Meya aliambatana na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, ndugu Elihuruma Mabelya, ambapo alieleza kuwa upotevu na utupaji wa chakula si changamoto ya usafi pekee, bali pia unahusiana na mabadiliko ya tabianchi, ukuaji wa uchumi na usalama wa chakula.
“Chakula kinapaswa kuwalisha watu, si kujaza madampo. Miji ina nafasi kubwa ya kukabiliana na upotevu wa chakula kwa sababu changamoto na suluhisho lake vinakutana mijini. Tunasimamia masoko, mifumo ya taka, tunashirikisha jamii na kutengeneza ajira za ndani,” amesema.
Amesema takribani asilimia 25 ya uzalishaji wa gesi chafuzi katika Jiji la Dar es Salaam unatokana na shughuli zinazohusiana na taka, ikiwemo maji taka na utupaji wa taka ngumu.
Aidha, amebainisha kuwa takribani asilimia 60 ya taka zinazozalishwa jijini hazikusanywi, huku asilimia 40 zikifikishwa katika eneo kuu la utupaji taka la Pugu Kinyamwezi.

Kutokana na hali hiyo, amesema jiji limeweka mikakati mbalimbali ikiwemo kuimarisha utenganishaji wa taka katika kaya, kuongeza uwezo wa urejelezaji, kusimamia sheria zinazokataza utupaji holela wa taka na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu usimamizi bora wa taka.
Amwfafanua kuwa jiji limeweka lengo la kuhakikisha angalau asilimia 25 ya kaya zinatenganisha taka ifikapo mwaka 2030, sambamba na kuongeza kiwango cha urejelezaji wa taka kwa asilimia 50.
Aidha, amesema jiji linaandaa uwekezaji katika miundombinu ya kuchakata hadi asilimia 50 ya taka za asili zinazozalishwa kila siku na kaya, hatua inayolenga kupunguza uzalishaji wa gesi ya Methane na kuzalisha mboji kwa ajili ya kilimo pamoja na kuongeza maeneo ya kijani.
Meya pia amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wajasiriamali wadogo, vikundi vya kijamii na wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi wanaojishughulisha na ukusanyaji na urejelezaji wa taka, akieleza kuwa ushirikiano na makundi hayo ni sehemu muhimu ya kufanikisha mfumo wa uchumi wa mzunguko.
Vilevile, alitambua mchango wa Mtandao wa C40 katika kuimarisha programu za mazingira na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu utunzaji wa mazingira jijini Dar es Salaam.
Akitoa wito kwa miji mingine duniani, Meya alihimiza viongozi kutumia takwimu katika kupanga na kutekeleza mikakati ya mazingira, kujenga ushirikiano na kuhakikisha jamii inashiriki kikamilifu katika kupunguza upotevu wa chakula na kuboresha usimamizi wa taka.
“Tunapounganisha nguvu zetu kama miji, tunaweza kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi, kuboresha usalama wa chakula, kutengeneza maelfu ya ajira za kijani na kujenga mazingira safi na yenye afya. Kama Dar es Salaam, tumejidhatiti kuhakikisha hakuna chakula kinachopotea wakati wananchi bado wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa chakula,” alisema.
Alisisitiza kuwa mustakabali wa miji isiyo na taka (Zero Waste Cities) unategemea hatua za vitendo, uwekezaji katika teknolojia na miundombinu ya kisasa, ushirikiano wa wadau na ushiriki wa wananchi, akieleza kuwa Dar es Salaam iko tayari kushiriki kikamilifu katika kujenga jiji safi, salama na endelevu lenye uchumi unaozingatia matumizi bora ya rasilimali.