Na Mwandishi Wetu, Dar es asalaam
TANZANIA imezindua rasmi ofisi za uratibu wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, zitakazokuwa makao makuu ya uratibu wa mashindano hayo, hatua inayolenga kuratibu maandalizi ya kihistoria ya Tanzania, Kenya na Uganda kuwa wenyeji wa michuano hiyo kwa pamoja.
Uzinduzi huo umefanyika sambamba na hafla ya utiaji saini mkataba kati ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Bodi ya Utalii Tanzania, ukiweka hatua nyingine muhimu katika maandalizi ya mashindano hayo yatakayofanyika mwaka 2027.

Akizungumza katika hafla hiyo leo Novemba 25,2026 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, alisema kuifanya Tanzania kuwa makao makuu ya uratibu wa AFCON 2027 ni heshima kwa nchi na matokeo ya ushirikiano kati ya Serikali na CAF.
Ameishukuru CAF, Rais wake Patrice Motsepe na timu ya uongozi wa shirikisho hilo kwa kukubali Tanzania kuwa makao makuu ya uratibu wa mashindano hayo.

Makonda amesema AFCON 2027 itakuwa ya kihistoria kwa kuwa ni mara ya kwanza nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda kuungana kuwa wenyeji wa mashindano hayo, akiwapongeza marais wa nchi hizo kwa kuunganisha nguvu na kuwezesha ukanda wa Afrika Mashariki kupata nafasi hiyo.
Amesema mashindano hayo yatakuwa na mechi 52 zitakazochezwa na Nchi 24 ndani ya siku 29, katika viwanja vinane, huku Tanzania ikiwa mwenyeji katika miji mitatu ya Dar es Salaam, Arusha na Zanzibar.

Amefafanua kuwa Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa kati ya asilimia 40 na 50 ya mechi zote, huku ikitarajia kupokea watazamaji kati ya 750,000 na 900,000.
Makonda amesema, mashindano hayo yanatarajiwa kuvutia mapato ya dola za Marekani bilioni mbili, sawa na takribani Sh trilioni tano, kupitia sekta za utalii, malazi, usafiri, usafishaji, matangazo na biashara ndogo ndogo.

Amesema kutokana na fursa hizo, Watanzania wanapaswa kujiandaa mapema kwa kupanua biashara zao, kurasimisha shughuli zao na kutumia mifumo ya kidijitali ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na malipo kwa wageni.“Fursa hii ni kubwa, pana na ndefu.
Mzunguko wa fedha utakuwa mkubwa sana. Kila mwenye kuuza atauza. Changamoto haitakuwa soko, bali itakuwa uwezo wa kushiriki soko,” amesema.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya mashindano hayo hayapaswi kuishia katika ubora wa viwanja na idadi ya mabao, bali yanapaswa kuonekana pia katika ajira zitakazozalishwa, biashara zitakazokua na watalii watakaovutiwa kutembelea Tanzania.

“Mafanikio yetu hayatapimwa kwa ubora wa viwanja pekee, idadi ya mabao yatakayofungwa au ukubwa wa shangwe za mashabiki. Yatapimwa pia kwa idadi ya ajira tutakazozizalisha, biashara tutakazozikuza, watalii tutakaowavutia na maisha ya wananchi tutakayoyaboresha,” amesema.
Katika hatua nyingine, Makonda amesema AFCON 2027 itakuwa na historia ya kipekee kwa kutumia Kiswahili kama lugha rasmi ya mashindano hayo, akieleza kuwa hatua hiyo itapanua matumizi ya lugha hiyo katika michezo ya kimataifa na kutoa fursa kwa vijana wa Kitanzania.
Amesema Serikali imejiandaa kuhakikisha usalama wa wageni watakaotembelea Tanzania na kuwezesha timu zitakazocheza nchini kupata huduma na stahiki zao kwa mujibu wa sheria na miongozo ya CAF.
Aidha, amewapongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji katika maandalizi ya mashindano hayo, akisema amekuwa akifuatilia kwa karibu hatua mbalimbali za kuhakikisha Tanzania inakuwa mwenyeji wa kihistoria.