Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TAASISI ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imetangaza kutoa suluhisho la kitaalamu kwa wachimbaji wa madini nchini kupitia tafiti za uchenjuaji zinazolenga kuongeza kiwango cha upatikanaji wa madini na thamani ya rasilimali zao.
Akizungumza katika Mkutano wa Uwekezaji wa Kimataifa wa madini unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, leo Novemba 19,2026 Mkurugenzi wa Huduma za Maabara wa GST, Notka Banteze, amesema taasisi hiyo imejipanga kuwasaidia wachimbaji, hususan wachimbaji wadogo, kupunguza upotevu wa madini unaotokana na kutumia mbinu zisizokidhi mahitaji ya uchenjuaji.

Amesema GST inafanya tafiti za uchenjuaji katika maabara kwa kutumia sampuli zinazochukuliwa kutoka maeneo ya uchimbaji au utafiti, kisha kuandaa mwongozo wa kitaalamu unaojulikana kama Flowsheet, utakaowawezesha wachimbaji kutumia uwiano sahihi wa kemikali ili kupata kiwango kinachostahili cha madini wanayochimba.
Banteze amesema changamoto ya uchenjuaji usiokamilika imekuwa ikisababisha wachimbaji wengi kupoteza sehemu ya madini yao na kulazimika kufanya marudio ya shughuli za uchenjuaji, hali inayoongeza gharama na kupunguza thamani ya madini wanayozalisha.
Ameeleza kuwa GST ni taasisi ya serikali iliyo chini ya Wizara ya Madini, yenye jukumu la kufanya tafiti za jiolojia na madini katika maeneo mbalimbali nchini, kukusanya na kuchakata taarifa za kisayansi, kuzitafsiri na kuzihifadhi kwa ajili ya matumizi ya wadau wa sekta ya madini.

Mbali na huduma za tafiti za uchenjuaji, Banteze amesema GST pia inazalisha vifaa maalumu vinavyotumika katika uchunguzi wa sampuli za madini ya metali kwa kutumia teknolojia ya tanuru (Fire Assay), vinavyojulikana kama Crucibles.
Amesema vifaa hivyo vinapatikana katika ukubwa tofauti wa D30, D40, D50 na D55, vikiwa na uwezo wa kustahimili joto la hadi nyuzi joto 1,400 na vinaweza kutumika zaidi ya mara tatu, jambo linalowezesha wadau kupata huduma hizo kwa gharama nafuu.