OTR yaifungulia milango RMB kushiriki mageuzi ya taasisi za umma

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

OFISI ya Msajili wa Hazina (OTR) imefungua milango kwa Rand Merchant Bank (RMB) kuangalia fursa za ufadhili na uwekezaji katika taasisi na kampuni za umma zilizo katika usimamizi wake.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha uwezo wa taasisi hizo kupata mitaji kwa ajili ya miradi ya kimkakati na kupanua shughuli za kiuchumi.

1003802976-1024x682 OTR yaifungulia milango RMB kushiriki mageuzi ya taasisi za umma

Mwaliko huo ulitolewa Jumanne, Novemba 18, 2026, na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alipokutana na ujumbe wa FirstRand Bank Limited, ambayo huendesha shughuli zake za kibenki na uwekezaji kupitia RMB, ulioongozwa na John Njuguna, Mkuu wa Huduma za Kibenki kwa Wateja wa Taasisi katika Ukanda wa Afrika Mashariki, katika ofisi za OTR jijini Dar es Salaam.

FirstRand Bank Limited ni miongoni mwa taasisi kubwa za kifedha barani Afrika, ikiwa imeorodheshwa katika Soko la Hisa la Johannesburg, Afrika Kusini, na Soko la Hisa la Namibia, na thamani ya mtaji wake katika soko la hisa inayozidi dola za Marekani bilioni 30.

1003802979-1024x682 OTR yaifungulia milango RMB kushiriki mageuzi ya taasisi za umma

Kupitia RMB, benki hiyo ina uzoefu wa muda mrefu wa kutoa suluhisho za ufadhili kwa serikali, kampuni na taasisi zinazomilikiwa na umma, taasisi za kifedha na kampuni za sekta binafsi katika Afrika Mashariki, ikiwemo Tanzania.

Mazungumzo hayo yalihusu fursa za ufadhili na uwekezaji katika sekta za miundombinu, nishati jadidifu, kilimo, usafirishaji, mawasiliano, madini, dawa na maeneo mengine ya uzalishaji, kwa kuangalia namna utaalamu wa kifedha wa RMB unavyoweza kusaidia taasisi na kampuni za umma kupata mitaji ya kutekeleza miradi ya kimkakati na kupanua shughuli zao.

1003802977-1024x682 OTR yaifungulia milango RMB kushiriki mageuzi ya taasisi za umma

Mchechu amesema OTR iko tayari kuratibu ushirikiano kati ya benki hiyo na taasisi za umma ili kubaini miradi yenye tija kibiashara na kuandaa mifumo ya ufadhili inayokidhi mahitaji ya kila taasisi.

OTR inasimamia taasisi na kampuni za umma 308, zikiwemo kampuni 252 ambazo Serikali inamiliki hisa nyingi na kampuni 56 ambazo Serikali inamiliki hisa chache.

1003802975-1024x682 OTR yaifungulia milango RMB kushiriki mageuzi ya taasisi za umma


Thamani ya jumla ya uwekezaji katika taasisi na kampuni hizo inafikia Sh trilioni 92.3, ikiwa ni mtaji mkubwa wa umma ambao unaweza kutumika zaidi kuchochea shughuli za kiuchumi na ukuaji wa uchumi nchini.

Mchechu amesema Serikali inazihimiza taasisi za umma kuimarisha uwezo wao wa kujiendesha kifedha kwa kutumia ipasavyo rasilimali na mali walizonazo ili kuvutia mitaji, badala ya kutegemea kwa kiwango kikubwa fedha zinazotengwa katika bajeti ya Serikali.

Ameeleza kuwa njia mbadala za kupata mitaji ni pamoja na mikopo kutoka benki za biashara, utoaji wa hati fungani na uuzaji wa hisa kupitia soko la mitaji.

1003802975-1-1024x682 OTR yaifungulia milango RMB kushiriki mageuzi ya taasisi za umma

Amehimiza RMB kuchunguza fursa zilizopo katika taasisi hizo na kuandaa mapendekezo ya ufadhili yatakayojadiliwa kwa pamoja na OTR na kampuni husika.

Kwa upande wake, Njuguna amesema RMB ina nia ya kuimarisha ushirikiano na taasisi za umma nchini, ikitumia uzoefu wake katika kufadhili miradi ya miundombinu na shughuli za kibiashara katika masoko mbalimbali ya Afrika.

Amebainisha kuwa vipaumbele vya Tanzania katika maendeleo ya miundombinu, pamoja na nafasi yake ya kimkakati katika biashara na usafirishaji wa kikanda, vinatoa fursa kwa benki hiyo kuchangia kupitia suluhisho za kifedha na uwekezaji zinazolingana na mahitaji ya miradi husika.

Aidha Mkuu wa Suluhisho za Uwekezaji katika Sekta ya Miundombinu wa RMB kwa Afrika, Sindisiwe Mosoeu, ameeleza kuhusu mifumo mbalimbali ya ufadhili inayoweza kutumika katika miradi ya taasisi za umma.

Mifumo hiyo ni pamoja na ufadhili wa miradi, ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, na ufadhili wa miradi ya nishati jadidifu.

Ameeleza kuwa aina ya ufadhili inayofaa kwa kila mradi itategemeana na aina ya shughuli zinazotekelezwa, uwezo wa mradi kuzalisha mapato, uwezekano wake wa kujiendesha kibiashara na uwezo wa kuvutia mitaji kutoka nje.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *