Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TANZANIA na Uganda zimekubaliana kuharakisha utatuzi wa vikwazo vya biashara, kupanua masoko ya bidhaa zao na kuboresha usafirishaji ili kukuza biashara na uwekezaji kwa manufaa ya nchi zote mbili.
Hayo yamefikiwa leo Jumatano Novemba 18, 2026 wakati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipoanza Ziara ya Kitaifa ya siku mbili nchini Uganda.

Mapema leo asubuhi, Rais Samia amewasili Ikulu ya Entebbe na kupokelewa na mwenyeji wake, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda.
Katika mazungumzo rasmi baina yao, walijadili namna ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa nchi zao, kuongeza biashara na uwekezaji, kurahisisha upatikanaji wa masoko na kuondoa vikwazo vinavyoathiri usafirishaji wa bidhaa kati ya Tanzania na Uganda.

Rais Dkt. Samia amesema Tanzania na Uganda zimepiga hatua katika kutekeleza maamuzi ya awali kuhusu biashara, uwekezaji, nishati, usafiri na miundombinu.
Ametaja changamoto za usafiri na usafirishaji kuwa miongoni mwa sababu zinazorudisha nyuma ukuaji wa biashara, na kueleza hatua zinazochukuliwa na Tanzania katika kuboresha miundombinu hiyo.

Rais Dkt. Samia amesema Tanzania ipo tayari kushirikiana na Uganda katika mradi wa reli ya kisasa utakaounganisha Isaka na maeneo ya mpakani na Uganda.
“Tanzania itaendelea kushirikiana na Uganda kwa moyo wa watu wamoja, hatima moja. Sasa ni wakati wa kuharakisha utekelezaji wa tuliyokubaliana,” amesema Rais Dkt. Samia, akibainisha hatua za upanuzi na maboresho ya Bandari za Dar es Salaam na Tanga kuwa sehemu ya jitihada za kuboresha usafiri na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Pia, Rais Dkt. Samia ameipongeza Uganda kwa kuanza ujenzi wa ubalozi wake katika Mji wa Serikali Dodoma, ikiwa ni Taifa la kwanza kufanya hivyo tangu kuzinduliwa kwa Mji huo.
Kwa upande wake, Rais Museveni amesema biashara kati ya Tanzania na Uganda inapaswa kuzingatia mahitaji ya pamoja, akitolea mfano wa mchele wa Tanzania wenye uhitaji mkubwa nchini Uganda, na sukari inayozalishwa Uganda yenye soko kubwa nchini Tanzania.
