Wapinzani wamekiri Falsafa ya 4R ya Samia imewaunganisha Watanzania

Na Daniel Mbega, Dar es Salaam

KAULI ya Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kusema Falsafa ya 4R ya Rais Samia Suluhu Hassan imewaunganisha Watanzania wala haikuja kwa bahati mbaya.

Mbunge huyo alitoa kauli hiyo Julai 18, 2024 mbele ya Rais Samia, ambaye alikuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye mji wa Tunduma mkoani Songwe, ambapo alikiri kwamba Dkt. Samia amefanikiwa kuwaunganisha Watanzania na kuishi kama ndugu.

Mhe. Fiyao alisema, hapo awali kulikuwa na uadui hasa kutokana na itikadi za kisiasa na wakashindwa kusaidiana kwenye shida na raha lakini baada ya kuingia madarakani, Rais Samia amefanya wananchi kuishi kama watoto wa mama mmoja.

Lakini Rais Samia alisema, Tanzania ni moja na hakuna nyingine, hivyo wananchi wanapaswa kusameheana na kuangalia mabadiliko.

“Tumekuja na falasafa ya maridhiano, kusameheana, kujenga upya na kuangalia mabadiliko gani tufanye ili nchi yetu iwe moja, Watanzania wawe wamoja. Nataka kushukuru katika kuifanyia kazi falsafa ile, tulikaa na vyama vyote vya siasa pamoja na tukaingia kwenye mkumbo huo huo tusameheane, tuangalie mabadiliko na tuangalie taifa tulijenge vizuri,” akasema.

Akaongeza: “Niwaombe sana Watanzania twendeni kama kitu kimoja, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni moja tu ulimwengu mzima, hakuna nyingine na Watanzania ndiyo sisi na sisi tunatakiwa kujenga Tanzania yetu.”

Mbunge Fiyao si mwanasiasa pekee wa upinzani ambaye amesifu falsafa hiyo, kwani hata viongozi wengi wa vyama vya upinzani nchini walimsifu Rais Samia, tena siku moja tu baada ya Serikali kuondoa marufuku ya mikutano ya hadhara iliyowekwa tangu mwaka 2015 na mtangulizi wake, Hayati John Magufuli, kwa vyama vya upinzani na kuukwamua mchakato wa Katiba Mpya, huku wakisema hilo lilikuwa ni tukio la kihistoria.

Baada ya Rais Samia kuondoa marufuku hiyo Machi 3, 2023, viongozi hao wa vyama vya siasa walisema hilo ni tukio la kwanza katika historia ya Tanzania, tangu mfumo wa vyama vingi uanze.

Joseph Selasini kutoka NCCR Mageuzi alipongeza hatua ya Rais Samia, lakini akatoa angalizo kuwa, huenda wapo aliowaita ‘wahafidhina’ ambao hawakupendezwa na uamuzi wa Rais.

Lakini pamoja na mambo mengine, viongozi hao walimsifu Rais Samia kwa kuwarudisha Chadema katika ushiriki wa matukio ya kisiasa, yanayoandaliwa na serikali, hatua waliyoeleza kuwa ni ukomavu wa kisiasa.

Wakati alipozungumza na viongozi wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, Rais Samia alisema: “Serikali inadhamiria kukwamua mchakato wa marekebisho ya Katiba, kwa jinsi tutakavokuja kuelewana huko mbele, wengine wanasema tuanze na Katiba ya Warioba, wengine tuanze na Katiba Pendekezwa, lakini kuna mambo ya ulimwengu yamebadilika.”

Akwaambia kwamba, itaundwa Kamati Maalumu kwa ajili kutoa ushauri wa namna ya kwenda kupata Katiba.

“Si muda mrefu, tutakwenda kuanza na kamati itakayokuja kutushauri, nataka kusema Katiba hii ni ya Watanzania, si ya vyama vya siasa,” akasema.

Ukiacha Katiba mpya, kwa muda mrefu nchini humo kulikuwa na kilio hasa kutoka kwa wanasiasa na jamii za kimataifa kuhusu haki ya kufanya siasa hasa mikutano ya siasa kuruhusiwa, ambayo ipo kisheria.

“Hii ni haki kwa sheria zetu, ni haki kwa vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara, uwepo wangu leo mbele yenu ni kuja kutangaza, lile tangazo la kuzuia mikutano ya hadhara sasa linaondoka,” akasema.

Akaongeza: “Lakini ndugu zangu, tuna wajibu, wajibu wetu serikali ni kulinda mikutano ya vyama vya siasa, wajibu wenu vyama vya siasa ni kufuata sheria na kanuni zinavyosema. Twendeni tukafanye siasa za kistaarabu, tukafanye siasa za kupevuka, tukafanyeni siasa za kujenga siyo za kubomoa, si kurudi nyuma hapa tulipofika. Sisi ndani ya CCM tunaamini katika kukosolewa na kujikosoa.”

Tangu Rais Samia alipoingia madarakani mwaka 2021 alionyesha dhamira ya kuleta maridhiano kwa kuunda kikosi kazi cha kukusanya maoni.

“Wakati mnanikabidhi kuongoza nchi hii, busara zilinituma, kwamba jinsi nilivyolipokea taifa hili, kuna haja ya kufanya taifa liwe kitu kitu kimoja, wote tuzungumze lugha moja, ili taifa lilwe moja, lazima tuwe na maridhiano, nikasema kwanza tuwe na mazungumzo kwenye vyama vya siasa,” alisema.

Tanzania ina vyama 19 vyenye usajili wa kudumu ambavyo ni UPDP, NRA, TADEA, TPL, CHADEMA, CUF, NCCR, UDP, UMD, chama tawala CCM, Demokrasia Makini, DP, SAU, AFP, CCK, ADC, CHAUMMA na ACT- Wazelendo.

Hata hivyo, kabla ya kuruhusu mikutano ya vyama vya siasa, Rais Samia alifanya jambo kubwa Februari 10, 2022 wakati Serikali yake ilipotangaza rasmi kuyafungulia magazeti manne ya Mwanahalisi, Mawio, Tanzania Daima na Mseto.

Na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, akatoa leseni za magazeti hayo.

“Agizo la Rais ni sheria, natoa leseni kwa Mwanahalisi, Mawio, Mseto na Tanzania Daima, kwa sababu mambo haya ni vizuri tutoke kwenye maneno twende kwenye matendo, tufungue ukurasa mpya, ili tumalize maneno, mwenye maneno yake aanze yeye, ukikutana na jiwe unarudi nyuma, unalipisha, kikubwa kazi iendelee,” akasema Nape Nnauye.

Falsafa ya 4R

Katika uongozi wake, Rais Samia anaamini katika kile kinachojulikana kama 4R – ikiwa ni ufupisho wa maneno manne ya lugha ya Kiingereza; Reconciliation (Maridhiano), Resilience (Ustahamilivu), Reforms (Mabadiliko) na Rebuilding (Kujanga Upya), falsafa ambayo imeleta mafanikio makubwa kwenye uongozi wake tangu aingie madarakani Machi 19, 2021.

Maridhiano

Kwenye kujenga upya Tanzania bora, Rais Samia anasema kuwa anatamani kujenga jamii yenye maridhiano na maelewano. Anatamani kujenga umoja pasipo kujali tofauti za kisiasa, kidini, kikabila na nyingine zote.

Hili litawezekana kwa kujenga jamii inayopata haki sawa mbele ya sheria, isiyobaguana na inayotoa fursa sawa sawa za kiuchumi kwa wote.

Rais Samia anaamini kuwa, maridhiano hayawezi kupatikana penye ubaguzi na pale ambapo kuna wanaokosa fursa na haki zao za kiuchumi na kiraia.

Ustahimilivu

“Tanzania haiwezi kusonga mbele kama wananchi na viongozi watakuwa legelege kulinda yaliyo yao. Wahenga walisema ‘Umoja ni Nguvu’ na namna pekee ya kupambana na changamoto zote zinazoikumba Dunia kwa sasa ni kwetu sisi kufanya hivyo kwa Umoja na Mshikamano,” anasema Rais Samia.

Huko tuendako, anasema, tutatikiswa na kuyumbishwa. Iwe kiuchumi, kimazingira, kijamii na kisiasa, lakini ni lazima tujenge ustahamivu.

“Hii ni kwa sababu hakuna nchi nyingine zaidi ya hii na hapa ndiyo kwetu. Nilitiwa nguvu sana na namna Watanzania walivyopokea tukio la Royal Tour kwa uzalendo wa kipekee,” anasisitiza.

Mabadiliko

Kuna msemo mmoja maarufu kwamba kitu pekee cha uhakika kwa mwanadamu ni mabadiliko.

Rais Samia amedhamiria kwamba serikali yake itajitahidi kufanya mabadiliko katika mifumo ya kisiasa, kiuchumi na katika sheria za uchaguzi, jambo ambalo tayari amekwishalifanya.

Lengo ni kwamba, Tanzania iende na wakati na – kama ilivyokuwa wakati mwingine – tujue mapema ni wakati gani wa kufanya jambo hata kama watu wanaliunga au hawaliungi mkono kwa wakati husika.

Mabadiliko katika sheria za uchaguzi ambazo baadhi tayari zimeshapitishwa yataleta ushindani wa haki na kuwapa watu fursa ya kuwachagua wawatakao kuwaongoza.

Hili amelisistiza sana kila anakopita na amewaahidi Watanzania kwamba chaguzi zijazo zitakuwa huru na haki huku akiliagiza Jeshi la Polisi Tanzania kutenda haki katika kipindi hicho.

Kwenye uchumi, mabadiliko yatakuwa na lengo la kutoa fursa kwa watu wengi zaidi kunufaika kiuchumi badala ya wachache.

Kujenga Upya

“Ninafahamu kwamba wananchi hawali maridhiano, ustahamivu wala mabadiliko,” Rais Samia anasema.

Kama walivyofanya watangulizi wa Rais Samia, lengo kuu linatakiwa kuwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Uchumi utakaoongeza ajira kwa vijana na utakaofungua fursa kwa makundi yote ya kijamii yaliyo nchini.

Tayari serikali inaendeleza miradi mikubwa ya miundombinu na mingine kwenye sekta ya madini na nishati.

Juhudi zilizofanywa kupitia kampeni ya Royal Tour zina lengo la kuzimua sekta muhimu ya utalii iliyoathiriwa sana na ugonjwa wa Uviko-19.

Katika kilimo serikali inafanya mabadiliko makubwa ili sekta hiyo muhimu ianze kuwa na mchango unaostahili kwenye uchumi na wiki iliyopita aliahidi kuanza kutoa ruzuku katika pembejeo za kilimo.

“Ninaamini kwamba kwa jitihada zetu za R 4, tutaweza kutimiza malengo ya kuwa na mfumo wa vyama vingi vya siasa. Lengo kuu halikuwa kuwa na vyama vingi vya siasa bali lengo lilikuwa kujenga jamii yenye uzalendo, maridhiano, ustahamivu na yenye uchumi unaokua kwa wote na endelevu,” alisistiza Rais Samia wakati huo.

Mafanikio ya 4R

Katika kipindi chake cha utawala, Falsafa za Samia za 4R zimeleta mafanikio makubwa katika jamii ya Watanzania, kuanzia uhuru wa habari na utoaji wa maoni, ambapo tumeshuhudia hata wapinzani wakifanya mikutano yao kwa amani bila kuingiliwa.

Zaidi tu ni kwamba, Watanzania sasa ndio wamebaki kuwa mahakimu kwa kuchuja sera za wanasiasa na kufanya uamuzi sahihi wao wenyewe kuhusu kipi cha kufuata baada ya hapo.

Wapinzani wamekuwa wakitoa maoni yao na kukosoa masuala mbalimbali, lakini Serikali imeendelea kuhimiza kufanya siasa za kistaarabu bila kumkera mtu mwingine, kama Sheria zinavyosema.

Mafanikio haya, kwa hakika, ndiyo yamemfanya Rais Samia kukubalika na mataifa mengi ulimwenguni kiasi cha kutunukiwa shahada mbalimbali za kimataifa.

Mnamo Juni 3, 2024, Rais Samia alitunukiwa Udaktari wa Falsafa wa Heshima (Honoris Causa) kwenye Sekta ya Anga na Rais wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga (Korean Aerospace University) Hee Young Hurr jijini Seoul, Jamhuri ya Korea.

Aprili 18, 2024, Rais Samia alitunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari (Honoris Causa) ya Uchumi na Chuo Kikuu cha Ankara nchini Uturuki kwenye hafla iliyofanyika chuoni hapo Ankara.

Desemba 28, 2023, Rais Samia alitunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Heshima ya Usimamizi wa Utalii na Masoko (Doctor of Philosophy in Tourism Management and Marketing (Honoris Causa) na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) visiwani Zanzibar.

Oktoba 10, 2023, alitunukiwa shahada ya heshima ya udaktari wa falsafa ya kielimu (Doctorate Honoris Causa) na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru nchini India, akiwa Mtanzania wa pili baada ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Novemba 30, 2022, wakati wa mahafali ya 52 duru ya 5 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Samia alitunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima na chou hicho kutokana na kuleta mageuzi ya kiuchumi na kuleta tumaini jipya.

Yapo mengi yanakuja kwa faida na maslahi mapana ya Tanzania, kwa sababu anachokifanya Rais Samia ni kwa ajili ya Watanzania wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *