Na Zahoro Mlanzi, Pwani
KIWANDA cha Kibaiolojia cha Tanzania Biotech Product limited (TBPL) cha mkoani hapa, kimeingia mkataba wa miaka mitatu na Kampuni ya JJ Agricultural Ltd wa kusambaza dawa mpya za viuatilifu hai vitakavyotumika kupambana na wadudu dhurifu wa mazao mbalimbali ya kilimo.
Mazao hayo ni pamoja na pamba, mahindi, matunda pamoja na mbogamboga hali itakayosaidia kupatikana kwa dawa hizo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa zoezi la kutiliana saini mkataba huo jana, Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Rafael Rodriquez, alisema amefurahishwa na makubaliano waliyofikia ambapo hatua hiyo ni mafanikio makubwa katika kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kufikiwa na bidhaa hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.
“Tunatambua changamoto inayowakabili wakulima ya uwepo wa wadudu dhurifu katika mazao yao, makubaliano haya yanakwenda kuwasaidia wakulima katika kupatikana kwa dawa hii hali itakayowafanya wakulima kuongeza tija na uzalishaji katika mazao yao,” alisema Rodriquez.
Alitumia fursa hiyo kubainisha sifa za kipekee za dawa hizo za viuatilifu kuwa ni tofauti na dawa zingine zinazopatikana sokoni kwa kuwa zenyewe zimetengenezwa kwa namna ya viuatilifu hai ikilinganishwa na dawa zingine zisizo za kibaolojia kwa kuwa zinasababisha madhara kwa watumiaji kama vile magonjwa ya kansa pamoja na kuharibu mazingira huku akiwataka mawakala zaidi kuendelea kujitokeza kwa wingi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya JJ Agricultural Ltd, Mhandisi James Kilaba, aliishukuru TBPL kwa kufikia makubaliano hayo huku akiomba kupewa ushirikiano katika kipindi chote cha utekelezaji wake ambapo miongoni mwa kazi zitakazofanywa na kampuni hiyo ni pamoja na kuhakikisha wanaandaa mashamba darasa katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Alisema madarasa hayo yatatumika katika kutoa elimu kwa wakulima juu ya namna bora ya kutumia dawa hizo katika kupambana na wadudu dhurifu katika mazao yao.
Mkataba huo kwa kuanzia dawa hizo zinatarajiwa kupatikana katika Mikoa ya Dar es Salaam Pwani, Morogoro, Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga, Iringa, Dodoma, Singida, Katavi pamoja na Tanga na utahusisha pia utoaji wa mafunzo ya namna bora ya kutumia dawa hizo ambao utakuwa unafanywa na wataalam kutoka TBPL.