Taifa Stars yaitandika Mongolia 3-0 FIFA Series 2024

Na Badrudin Yahaya

TIMU ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, imeibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya timu ya Taifa ya Mongolia kwenye mechi maalumu ya kirafiki ya FIFA Series 2024 iliofanyika nchini Azerbaijan

Huo unakuwa ni ushindi wa kwanza kwa Stars tangu kuanza mwaka huu lakini pia ni ushindi wa kwanza kwa Kocha, Hemed Seleman ‘Morocco’ ambaye amekaimu nafasi ya Kocha, Adel Amrouche ambaye amefungiwa kwasasa.

Katika mchezo wa kwanza wa michuano hiyo ambao ulichezwa Ijumaa iliyopita, Stars ilikubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Bulgaria.

Katika mchezo huo wa jana, Stars ilionekana kuwatawala wapinzani wao tangu dakika ya kwanza ya mchezo lakini ukosefu wa umakini uliwafanya wachezaji kupoteza nafasi nyingi za wazi za kufunga mabao.

Wachezaji Feisal Salum, Novatus Dismass na Kelvin John ‘Mbappe’ walikuwa ni wahanga wa kukosa nafasi za kufunga kipindi cha kwanza na kusababisha mchezo kwenda mapumziko matokeo yakiwa ni suluhu.

Kipindi cha pili wachezaji wa Stars walirekebisha makosa yao na kuandika bao la mapema kupitia kwa John ambaye anasakata soka katika Klabu ya Genk nchini Ubelgiji.

Kuingia kwa bao hilo kulitoa nafasi kwa Stars kuendelea kusaka mabao ya ziada na walifunga bao la pili ambalo lilufungwa kiustadi na mshambuliaji wa Azam, Abdul Seleman ‘Sopu’.

Mchezaji huyo alipata nafasi nyingine nzuri ya kuongeza bao la tatu akipewa pasi safi na Ben Sterkie lakini alijikuta akipoteza nafasi hiyo kwa kupiga nje ya lango.

Bao la tatu lilifungwa na kiungo anayecheza soka la kulipwa katika Klabu ya Shakhtar Donetsk ya Ukraine lakini kabla ya kufunga bao hilo muda mchache uliopita alipoteza nafasi ya wazi zaidi katika mchezo huo.

Ushindi huo unakuwa ni mkubwa zaidi kupatikana kwa Stars baada ya kupita miaka miwili. Mara ya mwisho Stars kufunga mabao matatu ilikuwa ni kwenye mchezo mwingine wa kirafiki ambapo walishinda 3-1 dhidi ya timu ya Afrika ya Kati, mchezo uliopigwa Machi, 2022.

Katika mchezo huo Stars iliwakosa baadhi ya nyota ambao wanacheza Simba na Yanga kwakuwa walipewa ruhusa ya kurudi nchini ili kujiandaa na mechi zao za michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwishoni mwa wiki hii.

Hata hivyo wachezaji kama Bakari Mwamnyeto na Kennedy Juma walisalia na kikosi na walicheza kwa dakika zote 90.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *