NDC, LABIOFAM zasaini mikataba ya mbolea hai, uhamishaji teknolojia

Na Zahoro Mlanzi

SHIRIKA la Taifa la Maendeleo (NDC), imetia saini mikataba miwili ya ushirikiano na Kampuni ya LABIOFAM kutoka Cuba, yenye lengo la kuimarisha uzalishaji wa mbolea hai na kuhamisha teknolojia ya kisasa kwa wataalamu wa Tanzania.

Mikataba hiyo inalenga kuongeza uzalishaji wa mbolea rafiki kwa mazingira inayotokana na teknolojia ya kibaolojia kutoka Cuba na kuiwezesha Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa bidhaa hiyo kwa matumizi ya ndani na soko la kikanda.

Aidha kupitia uhamishaji wa teknolojia, wataalamu wa Kitanzania watanufaika kwa mafunzo ya kitaalamu yatakayowezesha uendelevu wa mradi huo ndani ya nchi.

Akizungumza wakati wa tukio hilo Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Dkt. Nicolaus Shombe alisema ushirikiano huo ni hatua kubwa katika safari ya Tanzania kuelekea mapinduzi ya viwanda na kilimo hai.

Alisema kupitia mikataba hiyo, watahakikisha si tu wanazalisha bidhaa bora na salama kwa afya na mazingira, bali pia wanajenga uwezo wa ndani wa teknolojia, ajira na ujuzi kwa Watanzania.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole na Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Yordenis Despeigne Vera, ambaye alieleza kuridhishwa kwake na hatua hiyo muhimu katika kudumisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Dkt. Nicolaus Shombe (wa tatu kulia), akisaini mikataba miwili ya ushirikiano na Kampuni ya LABIOFAM kutoka Cuba akiwa na Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, Julio Gomes Gonzalez (wa pili kushoto). Wa kwanza kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole.

“Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Cuba umejengwa juu ya misingi ya mshikamano, maendeleo na ushirikiano wa kweli. Mikakati kama hii inaakisi dhamira ya mataifa yetu kuendeleza ustawi wa wananchi wake kupitia teknolojia na maarifa,” alisema Polepole.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa LABIOFAM, Julio Gomes Gonzalez, ambaye ndiye alisaini mkataba kwa niaba ya Serikali ya Cuba, aliwataka watanzania kutokuwa na shaka juu ya mkataba huo na kwamba utatekelezwa kama ambavyo wamekubaliana.

“Hakuna shaka huu uhusiano wa Cuba na Tanzania ulianza tangu zamani kupitia kwa waasisi wetu Fidel Castor na Mwalimu Julius Nyerere, hivyo tutautekeleza kama ambayo tumekubaliana na ndio maana tumekuwa na mikutano mingi iliyosaidia kuboresha zaidi uhusiano wetu,” alisema Gonzalez.

Alisema kampuni yao itahakikisha inasimamia utekelezaji wa makubalino hayo ili malengo waliyowekeana yafikiwe kwa asilimia 100.

LABIOFAM ni kampuni ya serikali ya Cuba inayojishughulisha na utafiti na uzalishaji wa bidhaa za kibaolojia, ikiwemo viuatilifu na mbolera hai.

Kampuni hiyo ni mshirika Mkuu wa TBPL, kiwanda cha kuzalisha viuatilifu vya kuua viluwiluwi wa mbu, chenye dhamira ya kusaidia juhudi za kitaifa za kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *