Na Daniel Mbega,
Kisarawe
LEO Jumatano, Novemba Mosi, 2023, Rais wa Ujerumani Frenk-Walter Steinmeier atatembelea Makumbusho ya Vita vya Majimaji pamoja na Shule ya Msingi Majimaji mjini Songea.
Rais Steinmeier ambaye yuko nchini kwa ziara ya siku tatu, atakwenda kujionea makumbusho hayo ya kihistoria, ambapo watawala wa Kijerumani waliwanyonga machifu wa Wangoni waliokuwa wakipinga kutawaliwa enzi hizo, baada ya kuanzisha mapambano yaliyobatizwa jina la ‘Vita vya Majimaji’.
Hii ni siku ya mwisho ya ziara hiyo, ambayo kimsingi ina manufaa makubwa kwa nchi zote mbili kijamii, kisiasa, kidiplomasia na kiuchumi.
Kupitia ziara hii wafanyabiashara wa Ujerumani na Tanzania wamekutana jana katika kongamano maalumu kujadiliana kuhusu fursa za kibiashara zilizopo hapa nchini baina ya nchi hizo mbili.
Rais huyo wa Ujerumani, pamoja na mwenyeji wake Rais Samia Suluhu Hassan walishiriki Jukwaa la Biashara, lililohusisha wafanyabiashara na wawekezaji wa nchi hizo mbili, lililoandaliwa na Ubalozi wa Ujerumani kwa ushirikiano na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Rais huyo wa Ujerumani ameambatana na wafanyabiashara 12 waliojikita katika sekta mbalimbali ambazo mataifa hayo yanahusiana na kongamano hilo lililofanyika jana, limelenga kukuza na kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi baina ya Tanzania na Ujerumani huku likiibua fursa mbalimbali na maeneo mapya ya ushirikiano.
Ni ukweli ulio wazi kwamba, ziara hii ni ishara ya diplomasia ya uchumi kukua kwani huo ni muendelezo wa viongozi mbalimbali kuja hapa nchini kwa ajili ya kuimarisha uhusiano.
Taarifa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na TIC, zinaeleza kwamba, Tanzania imekuwa ikiiuzia Ujerumani bidhaa zenye thamani ya wastani wa Dola za Marekani milioni 42.04 kwa mwaka.
Bidhaa kuu ambazo Tanzania inaiuzia Ujerumani ni Kahawa, Tumbaku, Pamba, Asali, Samaki, Nta na vito vya thamani.
Kadhalika, Tanzania inaagiza bidhaa kutoka Ujerumani zenye wastani wa Dola za Kimarekani milioni 237.43 kwa mwaka na bidhaa kuu ni Dawa, Vifaa Tiba, Mafuta (manukato, vipodozi), Magari, Vifaa na Mashine za Umeme.
Kwa upande wa uwekezaji, Ujerumani ni miongoni mwa nchi 10 zinazoongoza kwa uwekezaji nchini.
Kwa mujibu wa TIC hadi Agosti 2023, miradi 178 ya Ujerumani yenye thamani ya Dola za Marekani 408.11 milioni ilisajiliwa na kutoa fursa za ajira 16,121.
Kwa upande wa Zanzibar, Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) imesajili miradi 15 yenye thamani ya Dola za Marekani 300 milioni iliyozalisha ajira 905.
Ujerumani na historia yetu
Achana na utani wa makabila kwa makabila, Wahehe ni watani wakubwa wa Wajerumani, na hili halina ubishi.
Utani huu ulianza tangu siku ya Jumatatu, Agosti 17, 1891, yaani miaka 132 iliyopita, wakati Wahehe walipofanikiwa kuvichakaza vikosi vya Wajerumani katika harakati zao za kutanua himaya yao Afrika katika eneo ambalo baadaye lilijulikana kama German East Africa likihusisha Tanganyika (Tanzania Bara), Rwanda na Burundi za sasa.
Hii ndiyo sababu nimesema kwamba, Rais Steinmeier wa Ujerumani kama angekuwa na nafasi, alipaswa kwenda kutembelea kaburi la Shujaa Chifu Mkwawa, ambaye aliwaongoza Wahehe, wakiwa na silaha za jadi, wakawadunda Wajerumani na kumuua kamanda wao Emil von Zelewiski.
Kaburi la Chifu Mkwawa liko katika eneo la Mlambalasi, katika njia ielekeayo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, na ndiko mahali ambako alikuwa anajificha baada ya kubomolewa kwa Ngome ya Lipuli pale Kalenga na kuendesha mapambano ya msituni hadi alipolazimika kujiua Jumanne, Julai 19, 1898.
Pia ingekuwa vyema kama angetembelea Kaburi la Nyundo, ambalo lipo katika Kijiji cha Lugalo mkoani Iringa.
Kaburi hili linasemekana kuzikwa makamanda kadhaa wa Kijerumani, akiwemo Emil von Zelewiski maarufu kama ‘Nyundo’, waliouawa na Wahehe katika ‘Vita vya Lugalo’ siku hiyo ya Agosti 17, 1891.
Von Zelewiski alikuwa katili kweli kweli, kwani alikuwa akiwaua wapinzani wa utawala wa Ujerumani kwa kutumia nyundo, ndiyo maana akapewa jina la Nyundo.
Siku hiyo Wahehe, wakiongozwa na Chifu Mkwawa aliyekuwa na bunduki moja aliyopewa na Waarabu wakati ule wa Biashara ya Watumwa, huku wapiganaji wake wote walikuwa na silaha za jadi kama mikuki, kombeo, pinde na mishale na mapanga, waliwachakaza Wajerumani na kutwaa bunduki takriban 300.
Vita ya Lugalo ilifanyika takriban miezi nane tangu Wajerumani walipomnyonga Abushiri ibn Salim al-Harthi wa Pangani aliyeongoza upinzani katika ‘Vita vya Abushiri’ vya mwaka 1888 hadi 1889 akisaidiana na Bwana Heri wa Saadani. Abushiri alinyongwa Desemba 16, 1889 wakati Bwana Heri alipaswa kujisalimisha.
Ushindi alioupata Mkwawa dhidi ya Wajerumani ulikuwa mkubwa, na kama angeungwa mkono na machifu wa makabila mengine jirani, basi wangeweza kuzuia Wajerumani wasijitanue zaidi Bara, lakini mchifu wengi walimsaliti Mkwawa kwa vile tu alikuwa amewashinda katika vita baina yao.
Kwa hakika, kutembelea maeneo haya mawili kunaakisi mwangwi wa Filamu ya Royal Tour aliyoshiriki Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imeongeza idadi ya watalii kuzuru nchini Tanzania tangu ilipozinduliwa mwaka 2022.
Wengi wanaikumbuka Vita ya Maji Maji iliyodumu kwa miaka miwili baina ya Watanganyika na Wajerumani kati ya mwaka 1905 hadi 1907 (miaka tisa baada ya kifo cha Mkwawa) ambayo kwisha kwake ni baada ya Gavana Gustav Adolf von Götzen kuamua ‘kutengeneza’ njaa kwa kuzuia njia zote za upatikanaji wa chakula. Vita hivyo vilishuhudia takriban watu 300,000 wakipoteza maisha ama kwa kuuawa au kwa njaa na kusababisha kashfa kubwa ya tuhuma za rushwa na ukatili uliopindukia kwa kuwanyonga watu hadharani. Ndiyo maana mwaka 1907, Chancellor Bernhard von Bülow akaamua kumteua Bernhard Dernburg kuwa Gavana ili kuimarisha utawala wao kwenye koloni hilo.
Lakini kinachofanya wengi waendelee kuikumbuka ni mbinu zilizotumiwa na Mtawala wa Wangindo kule Kilwa, Kinjekitile Ngwale huko kwenye Bonde la Ngalambe alipowapaka na kuwanywesha dawa wapiganaji wake na kuwasadikisha kwamba risasi za Wajerumani zingegeuka kuwa maji.
Utaalamu huo ulisambaa karibu sehemu kubwa ya Kusini mwa Tanzania pamoja na Nyanda za Juu ambapo uliwaongezea ujasiri mkubwa wapiganaji hao waliokuwa wakiitetea ardhi yao isitawaliwe na Wazungu.
Kupigwa kwa Wajerumani na Mkwawa kulitokana na kosa alilolifanya Von Zelewiski, pamoja na uzoefu mkubwa wa vita aliokuwa nao, alijiamini kupita kiasi na kutotuma wapelelezi wakachunguze njia na uimara wa jeshi la Mkwawa. Aliamini kwamba, jeshi la Mkwawa lilikuwa kama yale mengine aliyoyapiga sehemu nyingine na kwamba huenda Chifu Mkwawa hakuwa na nguvu kama za Abushiri wa kule Pangani aliyepigwa mwaka mmoja nyuma.
Inasimuliwa kwamba, malengo ya Von Zelewiski yalikuwa kwenda kuivamia ngome ya Chifu Mkwawa kule Kalenga, lakini hakujua kama tayari Wahehe walikuwa wamejipanga njiani kukifanya kile ambacho hakuna aliyekitarajia.
Ili kuwazuia Wajerumani wasithubutu kufanya shambulio lolote, Wahehe ambao tayari walikuwa wanafahamu uwezo wa jeshi hilo la maadui pamoja na kulifahamu eneo lote na kupanga ni mahali gani waanze kushambulia, walipanga kuwazuia wasitumie mtindo wao wa nusu duara kushambulia. Kwa kuwa walikuwa wamepata taarifa za Wajerumani walivyopigana huko Pwani, Wahehe walikuwa wamejiandaa kuhakikisha wanakabiliana vilivyo na askari hao.
Awali Wahehe walitaka kufanya mashambulizi katika eneo la Ruaha Mbuyuni ambako Mto Ruaha unakatisha (kwa sasa ndipo ulipo mpaka wa Mkoa wa Morogoro na Iringa), lakini inaelezwa binamu wa Chifu Mkwawa aliyeitwa Kilonge ambaye alikuwa anashughulikia masuala ya habari na ujasusi, alikuwa ameota kwamba wangeweza kushindwa. Ni yeye ndiye aliyetoa ushauri mapambano hayo yakafanyike karibu na kilipo kijiji cha Lula-Lugalo, mbele ya Mto Mgella.
Mkwawa alikuwa na makamanda wenye nguvu kwenye jeshi lake kama Ngosi Ngosi Mwamgumba, Mtemimuma na kaka yake Mtwa Mpangile, ambaye baada ya kuanguka kwa Kalenga, Wajerumani walimtawaza kuwa ndiye Chifu wa Uhehe mnamo Desemba 24, 1896, lakini akanyongwa Februari 1897 kwa tuhuma kwamba alikuwa akivujisha siri na kumpa Mkwawa.
Mbali ya Wahehe, jeshi la Chifu Mkwawa lilikuwa na wapiganaji kutoka kabila la Wabena, ambao waliwekwa akiba na walikuwa wakilinda Kijiji cha Lula-Lugalo ili kama Von Zelewiski angefanikiwa kupenya kwenye mtego uliowekwa na Chifu Mkwawa, basi wao waweze kupambana na jeshi lake.
Wakati Von Zelwiski na vikosi vyake walianza safari ya kuelekea Kalenga saa 12:00 alfajiri, tayari Wahehe walikuwa wamekwishajipanga katika njia ambayo waliamini ndiyo wangepitia. Vikosi vya Wajerumani vilipita katika mstari mmoja kutokana na mazingira ya eneo lenyewe.
Wahehe walikuwa wakisubiri tu amri ya kamanda wao, Chifu Mkwawa, ili waanze kushambulia. Majira ya saa 1:00 asubuhi, wakati Wajerumani wakipita kwenye bonde hilo, ofisa mmoja Luteni Zitewitz akaliona kundi la ndege na kufyatua risasi kwa lengo la kupata kitoweo. Mlio huo wa risasi ukaonekana kama dalili za ishara ya kuanza mashambulizi.
Baadaye milio mitano au kumi ya bunduki aina ya Shenzi ikasikika. Wahehe nao wakadhani kwamba ndiyo ishara ya wao kuanza mashambulizi wakati vikosi vya Wajerumani havijafika kwenye eneo walilopanga kushambulia. Mamia ya askari wa Kihehe wakavamia kwenye kilima hicho na kuanza kuwashambulia Wajerumani waliokuwa wakipita bondeni, wakipiga kelele zao za vita “Hee hee Twahumite! Hee Heeee!” (yaani “Hee Heee Tumetoka! Hee Heeee!”).
Askari wengi wa Wajerumani walikuwa wanatembea bila kuzikoki bunduki zao na hawakuwa na muda wa kuzikoki, achilia mbali kutengeneza mfumo wa kujitetea kabla ya kushuhudia Wahehe wamewavamia. Muundo wa bunduki aina ya Mauser M71 iliyotengenezwa mwaka 1887 haukuwa unaeleweka vyema kwa askari wengi na walitumia dakika kadhaa kabla ya kuanza kufyatua risasi. Kelele ziliposikika wapagazi wote wakakimbia.
Punda waliokuwa wamebeba silaha wakaingia katika Kikosi Namba 5 ambapo askari wengi Wasudani wakaanza kukimbia kuokoa maisha yao.
Iliwachukua Wahehe dakika 15 tu (kuanzia saa 1:15 hadi 1:30 asubuhi) kuwafyeka Wajerumani na majeshi yao. Von Zelewiski aliuawa kwa kuchomwa mkuki ubavuni akiwa amepanda punda wake wakati akijiandaa kuwafyatulia risasi wapiganaji wa Mkwawa.
Kuhusiana na kifo cha Kamanda von Zelewiski, alijitetea mwenyewe kwa kutumia bastola yake kubwa na kuwapiga risasi watu watatu, wakati kijana mmoja wa Kihehe alipomchoma na mkuki ubavuni. Kijana huyo alikuwa na umri wa miaka 16 tu na alizawadiwa ng’ombe watatu na Mkwawa kwa kitendo hicho.
Luteni von Pirch na Dkt. Buschow pia waliuawa wakiwa juu ya punda wao ambapo majeraha yao yalikuwa makubwa mno. Karibu askari wote wa Kikosi cha 7, Kikosi cha Silaha, Kikosi cha 5 na baadhi ya askari wa Kikosi cha 6 waliuawa kabla hata hawajajua wafanye nini.
Luteni von Heydebreck, Luteni Usu Wutzer na Murgan Effendi pamoja na askari 20 hivi ndio waliofanikiwa kukimbia kutoka eneo hilo la mapigano na kukimbilia upande mwingine wa mlima na kuweka ngome wakijilinda dhidi ya mashambulizi ya Wahehe. Wapiganaji hao wa wajerumani walijificha kwenye pagala moja la tembe lililokuwa limetelekezwa mlimani. Askari mmoja Msudani ndiye aliyekiona kibanda hicho.
Lakini von Heydebreck aliishuhudia vita hiyo katika kipindi cha dakika mbili au tatu tu kabla ya kupoteza fahamu. Kulingana na ushuhuda wa Wahehe walioshiriki mapigano yale, vita hivyo havikumalizika mapema kama ambavyo Wazungu wa mstari wa nyuma walivyotegemea, badala yake askari walionusurika waliendelea kupambana hadi saa 4:30 asubuhi na kuwaua maadui wengi (Wahehe).
Askari wa mwisho wa kikosi cha Luteni von Tettenborn ndio hawakupata madhara makubwa ya mashambulizi ya Wahehe, washukuru kutokana na makosa ya ishara, vinginevyo wote wangeangamia katika kipindi hicho cha dakika 15 tu.
Von Tettenborn, Feldwebel Kay na askari kama 20 hivi Wasudani wakahamia upande wa kushoto wa eneo la mapigano na kutengeneza nusu duara kwa ajili ya mashambulizi huku wakiwa wameumia. Wakiwa hapo walipandisha bendera ya Ujerumani juu ya mti na kupiga mbinja ili kuwaita manusura wengine.
Wakati huo Wahehe waliendelea kuwakimbiza manusura na kushambulia kila waliyemuona mbele yao. Mkanganyiko ukaongezeka baada ya kuwasha nyasi.
Mnamo saa 2:30 asubuhi hiyo, Luteni von Heydebreck, Luteni Usu Wutzer na Murgan Effendi wakiwa na askari wao 12 walipenya na kuungana na kikosi cha von Tettenborn. Von Heydebreck alikuwa anavuja sana damu kutokana na majeraha mawili makubwa ya mikuki. Kwa kuwatazama tu watu hao, von Tettenborn akatambua kwamba vikosi vyao vyote vilikuwa vimesambaratishwa na kikosi cha silaha kutekwa, ambapo Mkwawa aliteka bunduki 300. Askari wa jeshi la Wajerumani waliouawa siku hiyo walikuwa zaidi ya 500.
Ilipofika saa 3:00 Luteni Usu Thiedemann, akiwa na majeraha makubwa ya moto aliingizwa kwenye kikosi cha Luteni von Tettenborn akiwa amebebwa na askari waliokuwa wanafanya doria. Nyasi zilizokuwa zinaungua sasa zilimtisha von Tettenborn na manusura wengine.
Hadi kufikia saa 10:00 jioni Luteni von Tettenborn alikuwa amewakusanya majeruhi wengi na kuokota baadhi ya mizigo yao. Wahehe waliokuwa wamepagawa kwa hasira pamoja na moto mkubwa uliokuwa ukiendelea kuteketeza msitu viliifanya kazi ya kuwatafuta majeruhi wengine kuwa ngumu, hivyo wengi waliteketea kwa moto. Von Tettenborn akaamua kuanza kurudi nyuma kabla hajazuiwa na Wahehe.
Wakati wa usiku wa manane kikosi kilichokuwa na Luteni von Tettenborn kikapiga kambi ng’ambo ya pili ya mto tofauti na mahali walipolala kabla ya kuanza mapambano. Kikosi chake sasa kilikuwa na yeye mwenyewe na Luteni von Heydebreck, ma-NCO watatu wa Kijerumani (ingawa Luteni Usu Thiedemann alikufa baadaye njiani), maofisa wawili wa Kiafrika, ma-NCO 62 wa Kiafrika, wapagazi 74 na punda 7. Kutoka hapo wakaanza kutembea hasa nyakati za usiku kurudi nyuma ambapo walifika Myombo Agosti 29.
Hakuna takwimu halisi za idadi ya Wahehe waliokufa kwenye vita hiyo ingawa makadirio ni kati ya 260 hadi 700. Kwa ujumla, Wahehe walikuwa wameshinda vita dhidi ya wakoloni, ushindi ambao ni wa kihistoria kwa mtawala wa Kiafrika wakati huo dhidi ya Wazungu, ukiachilia mbali ushindi wa Ethiopia dhidi ya Waitaliano miaka mitano baadaye katika Vita ya Adwa iliyoongozwa na Mfalme Menelik wa Pili na Malkia Taytu Betul mnamo Machi 1896.
Mkwawa ni nani?
Alipozaliwa yapata mwaka 1855 katika eneo la Luhota, wazazi wake, baba Mtwa Munyigumba Kilonge Mwamuyinga na mama Sengimba, walimpa jina la Ndesalasi, likiwa na maana ‘Mtundu na Mdadisi’.
Lakini alipofikia ujana na kuanza kupigana vita akiwashinda maadui wengi, wakamwita Mkwavinyika, ikiwa na maana ‘Mshindi wan chi nyingi’. Jina hili baadaye likafupishwa na kuwa Mkwava au Mkwawa.
Mwaka 1887, ushujaa wake ukawafanya watu wamwite pia ‘Mtwa Mkwava Mkwavinyika, Mahinya Yilimwiganga Mkali Kuvago, Kuvadala Tage Matenengo, Manwiwage Seguniwagula Gumganga’.
Hili lilimaanisha: “Mtawala, mtekaji wa nyika, mkali kwa wanaume, mpole kwa wanawake asiyetabirika, aliyeshindikanika, mbabe mwenye nguvu, udongo pekee ndio utakaomuweza”.
Julai 16, 1898, baada ya kuna amezingirwa, Mkwawa akaamua kujiua kwa kujipiga risasi. Wajerumani wakakata kichwa chake na kukipeleka Ujerumani kwa kile kilichoelezwa kwenda kuangalia ubongo wake ulikuwaje hata akawa na mbinu za kuwashinda.
Fuvu lake lilirejeshwa nchini Tanzania mnamo Julai 9, 1954 (siku mbili baada ya kuzaliwa kwa Chama cha TANU) na kukabidhiwa na mjukuu wake Chifu Adam Sapi Mkwawa kabla ya kupelekwa Kalenga kwenye makumbusho.
Naam. Maeneo hayo tajwa ni sehemu ya Mali Kale, ambayo kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais Samia kwenye ukuzaji wa utalii, ni vyema yakanadiwa na watu wakaenda kujifunza historia hii muhimu.
Kijijini Msanga-Ngongele,
0629299688