Latra ilivyojizatiti kudhibiti usafiri vyombo vya ardhini

Na Frank Balile

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), imekuwa mhimili mkubwa kwa vyombo vya usafiri ardhini, huku ikifanikiwa kuongeza mapato kwa asilimia 32 katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mafanikio hayo ni ushirikiano uliopo kati ya wafanyakazi wa mamlaka hayo yanayoongozwa na MKurugenzi Mkuu, CPA Habibu Suluo.

Mkurugenzi Mkuu huyo anasema kuwa, mapato ya mamlaka yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka, ambapo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2021/22, yameongezeka kutoka Shilingi bilioni 25.945 hadi shilingi bilioni 28.53, ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 2.58 sawa na ongezeko la asilimia 10.

Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22 hadi 2022/23, mapato ya mamlaka yameongezeka kutoka shilingi bilioni 28.53 hadi shilingi bilioni 34.17 (kabla ya kukaguliwa na CAG), ikiwa ni ongezeko la shilingi bBilioni 5.64 sawa na ongezeko la asilimia 20.

Kwa jumla, katika kipindi cha miaka mitatu ya utekelezaji wa majukumu ya LATRA, mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2022/23, mapato ya mamlaka yameongezeka kutoka shilingi bilioni 25.95 hadi shilingi bilioni 34.17 (kabla ya kukaguliwa na CAG), ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 8.22 sawa na ongezeko la asilimia 32.

Mapato yatokanayo na adhabu yamepungua na mapato yatokanayo na leseni kujenga tabia ya utii wa sheria na kupunguza adhabu kwa watoa huduma za usafiri ardhini nchini,anasema.

CPA Habibu Suluo, anasema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeiwezesha LATRA kutekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi na hivyo, imeipa mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu yake.

Uongozi wa Rais katika Awamu hii, umetujengea mazingira mazuri na bora ya kusimamia sekta hii katika eneo letu la Udhibiti Usafiri Ardhini. Haya yamekuwa yakifanyika kwa ufanisi mkubwa kutokana na uongozi mahiri na madhubuti wa wasaidizi wake,” anasema.

Ameongeza kwamba, hivi karibuni Rais ameunda Wizara mpya ya Uchukuzi na kuwateua Prof. Makame Mbarawa, kuwa Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, kuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi na Dkt.Ally Posi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi.

Katika usafiri wa barabara, kwa kipindi cha mwaka 2020/21 hadi 2022/23, idadi ya leseni za usafirishaji iliongezeka kutoka leseni 230,253 hadi leseni 284,158 ikiwa ni sawa na ongezeko la leseni 44,205 ambayo ni ongezeko la asilimia 18.4.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 5(1) (b) cha Sheria ya LATRA, Mamlaka inao wajibu wa kutoa, kuhuisha, kusitisha na kufuta leseni za usafirishaji, hivyo mamlaka hutoa leseni kila mwaka kwa vyombo vya usafiri kibiashara.

CPA Suluo ameongeza kuwa, leseni hizo hutolewa baada ya mtoa huduma kukidhi masharti yanayotakiwa kwa aina ya huduma husika. leseni hizo hutumika kutambua idadi ya watoa huduma wanaodhibitiwa.

Anasema kuwa, mamlaka ina jukumu la kusajili wahudumu na kuthibitisha madereva wa vyombo vinavyodhibitiwa kwa lengo la kupata madereva wenye sifa na weledi kuendesha magari yanayotoa huduma kwa usafiri wa umma kwa kupima umahiri wao, hasa maarifa waliyopata ili kuimarisha usalama.

 Hadi, kufikia Septemba 30, 2023, madereva 17,990 wamesajiliwa na kuingiza taarifa zao kwenye kanzidata ya Mamlaka, ambapo madereva 1,617 wamethibitishwa baada ya kufaulu mtihani wa kuthibitishwa na LATRA.

Miongoni mwa madereva hao, wapo wa mabasi 645, wamesajiliwa kwenye mfumo wa kufuatilia mwenendo wa mabasi (VTS), na kupatiwa kitufe maalumu cha utambulisho (identification button, i-button). Matumizi ya kitufe hicho ni kurahisisha utambuzi wa dereva anayeendesha gari kwa wakati husika kupitia mfumo wa VTS.

Katika Usafiri wa Reli, CPA Suluo anasema kuwa Mamlaka, inaendelea kutoa mafunzo kazini kila mwaka kwa Wafanyakazi muhimu wa usalama katika uendeshaji wa reli (Safety Critical Workers), kwa Tazara na TRC ili kuwaongezea ujuzi wa kutimiza majukumu yao kwa weledi, kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Latra imepanga kuhakikisha usalama wa abiria na mizigo unazingatiwa katika usafiri wa reli.

“Mafunzo ya aina hii yanasaidia kuwajengea uwezo wafanyakazi hao muhimu kuzuia ajali zitokanazo na makosa ya kibinadamu (Human Errors), tathmini inaonesha kwamba, makosa ya kibinadamu katika uendeshaji wa shughuli za reli huchangia zaidi ya asilimia ya 85 ya ajali zote za treni kwa TRC na Tazara. Hivyo, mafunzo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali zinazosababishwa na makosa ya kibinadamu,” anafafanua CPA Suluo.

CPA Suluo ameeleza kuwa, Latra imepiga hatua kubwa katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), ambapo inatumia mifumo mbalimbali ikiwemo Mfumo wa Usimamizi wa Shughuli za Kiudhibiti (RRIMS), Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS), Mfumo wa Tiketi Mtandao, Mfumo Tumizi wa Latra (Latra App), Mfumo wa e-Mrejesho na Mfumo wa Taifa wa Ununuzi wa Umma wa Kieletroni (NeST).

RRIMS imeunganishwa na mifumo ya taasisi nyingine za Serikali kama vile TRA, Tira, Nida, GePG na Brela na pia imeunganishwa na mifumo ya wadau wengine wakiwemo watoa huduma wa tiketi mtandaoni ili kurahisisha utoaji huduma za mamlaka kwa wananchi.

Mkurugenzi Mkuu huyo anasema, Latra imeanza kutumia Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS), tangu mwaka 2017 na hadi sasa, zaidi ya magari 9,420 yameunganishwa na mfumo huo, ambapo magari 7,620 yapo hai na yanaendelea kutoa taarifa kupitia mfumo huu.

Mfumo umesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani zinazotokana na mwendokasi, umepunguza madhara ya ajali zinazotokana na mwendokasi na umerahisisha uchunguzi wa ajali pale zinapotokea.

Anaelezea mifumo mingine ni Mfumo wa Tiketi Mtandao ambao umesaidia kudhibiti upandishaji holela wa nauli. Mfumo Tumizi wa Latra (Latra App) unaopatikana Play Store kwenye simu zote za Android, unamwezesha mwananchi kupata taarifa za nauli za mabasi ya masafa marefu na mabasi ya mijini na mamlaka inaendelea kuboresha huduma za mfumo huo ili kuwezesha abiria kutambua mwendo kasi wa gari.

CPA Habibu Suluo, anasema mamlaka hayo yapo mbioni kutoa mwongozo kwa waendeshaji wa usafiri wa waya, ambapo wanatarajia uwekezaji huo utafanyika zaidi katika sekta ya utalii.

Usafiri wa waya wenzetu wanautumia kwa ajili ya utalii, starehe na kuwahi maeneo ambayo yanaonekana kuwa na foleni, sisi tunachotaka kufanya ni kuangalia ni namna gani ambavyo usafiri huu utakuwa na tija hapa nchini, hususan sekta ya utalii.”

Lengo letu ni kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuinua sekta ya utalii nchini, LATRA hatuwekezi huko bali, tunaweka miongozo na kanuni za udhibiti wa usafiri huo.

CPA Suluo katika kikao kazi kati ya Latra na wahariri wa vyombo vya habari nchini, chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, aliweka wazi shughuli za Latra.

Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, maono yake yamesaidia wahariri kupata darasa zuri na kufahamu kazi za taasisi zilizo chini msajili, amebuni utaratibu wa mashirika na taasisi za umma kukutana na wahariri na kueleza shughuli zao kwa watanzania ambao kimtazamo ndiyo wamiliki  wa hizo taasisi na mashiriki ili wajue changamoto na mafanikio ya mashairika yao.

Hatua hiyo inasaidai kuyaelewa mashiriki na taasisi za umma utendaji, faida na chamangoto zake, wakielewa jinsi yanavyosaidia kujenga uchumi wa nchi, badala ya kuyasikia.

Kutokana na utaratibu huo, kwasasa kumekuwa na matokeo mazuri kwa wananchi kuyafahamu kupitia taarifa zinazotolewa na vyombo vya habarki kuhusu shughuli za mashirika.

Pamoja na hayo, Mkurugenzi Mkuu anasema wadau wa Latra ni wasafirishaji wa mabasi ya njia ndefu na mabasi ya miji na majiji, magari ya mizigo, madereva wa mabasi na malori, wakiwemo watoa huduma wa magari maalum ya kukodi, teksi mtandao, abiria, taasisi za umma na wananchi.

Katika utaratibu huo, Latra ni taasisi ya 20 ambayo ipo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kukutana na wahariri wa vyombo vya habari.

Kupitia vikao kazi hivyo, wanapata nafasi ya kuelezea wanafanya mambo gani, wanaelekea wapi na yapi matarajio ya mashirika hayo na kwamba, mikutano hiyo ni muhimu kwa wahariri ambao kupitia vyombo vyao watafikisha taarifa sahihi kwa umma.

Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia mashirika ya umma, ndani ya hayo mashirika ya umma wana mashirika yenyewe, taasisi na kampuni ambapo zipo zaidi ya 298, miongoni mwa hizo kuna taasisi ambazo zinatoa huduma na zinafanya biashara huku nyingine zikijiendesha kibiashara, aidha kati ya hizo Serikali inamiliki hisa chache ambazo ni chini ya hisa asilimia 50.

Lengo la Serikali ni kuona mashirika hayo yanafikia lengo lake, ikizingatiwa kwamba yameanzishwa kwa mujibu wa sheria, mashirika haya kwa kiasi kikubwa yamefikia kiwango cha kuridhisha japo kuna machache ambayo hayajafikia malengo.

Mbali na hayo, CPA Suluo amesema, Latra ni mamlaka ya Serikali iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 3 ya mwaka 2019.

Sheria hii ilifuta Sheria ya iliyokuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra). Latra imepewa jukumu la kudhibiti sekta ya usafiri ardhini, hususani usafiri wa mizigo na abiria.

Usafiri ambao unajumuisha mabasi ya njia ndefu, mabasi ya mijini, magari ya mizigo, teksi, pikipiki za magurumu mawili na matatu, usafiri wa reli na usafiri wa waya.

Anasema malalamiko makubwa ambayo wanayapata mijini ni pamoja na daladala kukatisha ruti, lakini sasa wameweka namba maalumu ambazo abiria wakiona daladala inakatisha ruti au kufaulisha wawasiliane nao ili waweze kuchukua hatua za haraka.

Mkurugenzi Mkuu huyo anasema Latra inawezesha matumizi ya teknolojia kama suluhisho kwa changamoto katika sekta ya usafiri.

Anasema, hayo yanafanyika kwa ushirikishwaji wa wadau wa sekta ya umma na sekta binafsi, moja ya mafanikio yanayotambuliwa ni Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS).

Mfumo huu umekuwa ukifanya kazi tangu mwaka 2017 na umeonesha matokeo chanya katika kuokoa maisha na mali.

Latra inaaendelea kutumia teknolojia kutatua changamoto za usafiri nchini. Pia, amesema, kazi za mamlaka zimeainishwa katika kifungu cha tano cha Sheria Na.3 ya Latra ya mwaka 2019 ikiwemo kutekeleza majukumu ya Sheria za Kisekta.

Kwa namna ya kipekee tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuweka muundo mzuri wa uongozi ambao unatuwezesha kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi.

Anasema mchango wa sekta binafsi katika Sekta ya Usafirishaji nchini ni mkubwa, hivyo wataendelea kushirikiana nao bega kwa bega ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Majukumu mengine, CPA Habibu Suluo anasema ni kutoa, kuhuisha, au kufuta leseni za usafirishaji na kwamba, kwa kuzingatia matakwa ya sheria za kisekta, Latra inawajibika kusimamia viwango vya ubora wa huduma na usalama katika sekta zinazodhibitiwa.

Anasema wanaratibu shughuli za usalama wa usafiri ardhini, kusajili wahudumu na kuthibitisha madereva wa vyombo vya usafiri wa umma ardhini, huku wakihakikisha na kuthibitisha hali ya usalama wa vyombo vya usafiri wa umma ardhini kwa matumizi.

Kufuatilia mwenendo wa utendaji kazi wa sekta zinazodhibitiwa kwa kuangalia viwango vya uwekezaji, gharama, upatikanaji na ufanisi wa huduma.

CPA Habibu Suluo anasema wanashughulikia na kuwezesha utatuzi wa migogoro na malalamiko na kuelimisha umma kuhusu kazi na wajibu wa mamlaka.

“Latra tunahudumia na kuwajali wadau wetu wote wanaotumia usafiri wa barabara pamoja na usafiri wa reli.”

Katika kikao kazi hicho, wanahabari walihakikishiwa ushirikiano kutoka Latra.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *