Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MAKAMU wa Rais, Deogratius Ndejembi, amelitaka Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kusimamia kuunganishwa kwa mifuko na programu 75 za uwezeshaji wananchi kiuchumi kuwa mfuko mmoja ili kurahisisha upatikanaji wa mitaji na dhamana, hususan kwa vijana wasio na sifa za kukopa katika taasisi za fedha.
Ndejembi ametoa wito huo leo Novemba 23,2026 alipokagua maonesho ya vijana kabla ya kushiriki hafla ya kitaifa ya kuwasilisha mafanikio ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita, kipindi cha pili katika Sekta ya Maendeleo ya Vijana, iliyofanyika katika Ukumbi wa Super Dome, Masaki, jijini Dar es Salaam.

Akihutubia katika hafla hiyo, amesema Sh bilioni 200 zilizotengwa na Serikali kwa ajili ya uwezeshaji vijana zinapaswa kutolewa bila upendeleo na kuwafikia vijana wa mijini na vijijini, wakiwemo wenye ulemavu.
Ameonya dhidi ya matumizi ya fedha hizo kulipia posho za watumishi au kununua magari, akisisitiza mafanikio yapimwe kwa biashara zilizoanzishwa, zilizokua na ajira zilizozalishwa.

Aidha, amewataka Wizara, taasisi za umma na halmashauri kuhakikisha vijana wanaotekeleza zabuni wanalipwa kwa wakati ili kuzuia ucheleweshaji wa malipo unaoweza kukwamisha shughuli na ukuaji wa biashara zao.
Katika hatua nyingine, Ndejembi alisema taasisi za umma zimeahidi kutoa takribani nafasi 600 za mafunzo kwa vitendo, ambazo zitatangazwa hivi karibuni baada ya kukamilika kwa taratibu za uratibu.

Amesema nafasi hizo ni hatua ya awali kuelekea lengo la kupata angalau nafasi 10,000 katika mashirika ya umma na 20,000 katika sekta binafsi.Pia alitoa wito wa kutumia Mashindano ya Afcon 2027 kama fursa ya kiuchumi kwa vijana kwa kuwawezesha kupata mafunzo ya muda mfupi yatakayowajengea uwezo wa kuhudumia wageni na kufanya shughuli mbalimbali wakati wa mashindano hayo.

