Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka viongozi wa Serikali za Mitaa na taasisi mbalimbali kuwa mstari wa mbele kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu usafi wa mazingira, akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuwa mfano kwa wananchi katika usafi na usimamizi wa sheria.
Aidha, amemtaka Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, kuchukua hatua kali dhidi ya viongozi na watendaji wazembe wanaoshindwa kusimamia sheria za usafi katika maeneo yao, akisisitiza kuwa usafi hauhitaji maneno bali uwajibikaji na vitendo.

“Lazima tukaishi kauli ya Rais kwa vitendo ili kumuonesha tunampenda Rais wetu na tunamuunga mkono. Kila kiongozi awe mfano wa kufanya usafi, si kusema tu, bali aoneshe kwa vitendo,” amesema Mpogolo, akiongeza kuwa Rais Samia amekuwa kinara wa utunzaji wa mazingira tangu alipokuwa Makamu wa Rais, hivyo maelekezo yake yanapaswa kutekelezwa kwa matokeo yanayoonekana.

Mpogolo pia amewapongeza wachezaji wa zamani, viongozi wa Chama cha Mabaunsa na wakandarasi wa usafi kwa kushiriki katika zoezi hilo na kuimarisha vifaa vya kazi.
Amesema wakandarasi wamepewa miezi mitatu kuboresha uwezo wao, huku magari mapya ya kisasa ya usafi yaliyoagizwa yakiwa njiani kuwasili nchini mwishoni mwa Novemba au mwanzoni mwa Desemba, na uzinduzi wake ukitarajiwa katikati ya Desemba.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, amesema usafi unaendelea kusimamiwa katika mitaa yote 159, ikiwa ni sehemu ya hatua ya pili ya kampeni ya kupendezesha Wilaya ya Ilala, huku elimu kwa wananchi ikiendelea kutolewa ili kuhakikisha usafi unakuwa utamaduni wa kila siku.
Mabelya amesisitiza kuwa kila mwananchi anapaswa kuwajibika kwa usafi wa eneo lake, akiwataka wenye maduka na kaya kuhakikisha wanakuwa sehemu ya kampeni hiyo kila siku.

Ameongeza kuwa wakandarasi wanaendelea kuboresha vifaa, ustawi wa watumishi na kuagiza teknolojia za kisasa ili kuongeza ufanisi wa huduma za usafi katika Jiji la Dar es Salaam.