Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

TAASISI ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imesema kuongezeka kwa shughuli za utafiti wa madini nchini ni muhimu katika kugundua maeneo mapya yenye rasilimali hizo, kuongeza migodi na kuhakikisha upatikanaji wa malighafi za uhakika kwa ajili ya viwanda.

Akizungumza katika mdahalo wa kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya madini, Mtendaji Mkuu wa GST, Ali Samaje, amesema taasisi hiyo ina jukumu la kutoa taarifa za kisayansi zinazohusu jiolojia, jiokemia na jiofizikia ili kuwawezesha watafiti na wawekezaji kutambua maeneo yenye viashiria vya madini.

Amesema taarifa hizo zinasaidia kupunguza gharama na muda wa kufanya utafiti kwa kuwa wawekezaji wanaelekezwa katika maeneo yenye uwezekano mkubwa wa kuwa na madini.

Samaje amesema sekta ya madini ni miongoni mwa nguzo muhimu za uchumi wa taifa na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hivyo ni muhimu kuongeza uwekezaji katika utafiti ili kugundua mashapo mapya na kuanzisha migodi zaidi.

Ameongeza kuwa Tanzania inahitaji kwenda hatua nyingine ya kuongeza thamani ya madini kwa kuimarisha viwanda vya uchakataji, uyeyushaji na usafishaji, pamoja na kuanzisha viwanda vinavyotumia madini kama malighafi kuzalisha bidhaa za mwisho.

Amesisitiza kuwa GST itaendelea kutoa taarifa za jiosayansi zitakazosaidia kuongeza upatikanaji wa rasilimali za madini na kuhakikisha viwanda vinakuwa na uhakika wa malighafi kwa ajili ya uzalishaji endelevu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *