*Mfumo kuwaunganisha vijana na fursa za kiuchumi
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
JUMLA ya vijana 105,055 wamejisajili katika mfumo wa majaribio wa kidijitali wa uwezeshaji vijana (YES) unaotarajiwa kuzinduliwa rasmi na Serikali Novemba 23, mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya hatua za kurahisisha upatikanaji wa taarifa, huduma na fursa za kiuchumi kwa kundi hilo.
Mfumo huo ni miongoni mwa mifumo miwili itakayozinduliwa na Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, katika tukio la kitaifa la kuwasilisha mafanikio ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha pili kwenye sekta ya maendeleo ya vijana.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, aliyasema hayo leo Novemba 21, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia maandalizi ya mafanikio ya mwaka mmoja wa maendeleo ya vijana yatakayofanyika jijini humo Novemba 23, 2026.
Amesema vijana hao wamejisajili wakati mfumo huo ukiwa katika majaribio, kabla ya kuzinduliwa rasmi.
Amesema mfumo wa YES umelenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa za huduma na fursa zinazotolewa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali, huku ukiwaunganisha vijana na taasisi zinazotoa huduma hizo.
“Na hapa niwapongeze vijana ambao mpaka sasa katika majaribio ya mfumo huu wameshajisajili vijana 105,000 kabla haujazinduliwa ukiwa katika majaribio,” amesema Nanauka.
Amesema mfumo mwingine utakaokwenda sambamba na YES ni wa uratibu wa maendeleo ya vijana, ambao utaweka utaratibu wa pamoja kwa wizara, taasisi za umma, serikali za mitaa na wadau wengine katika kupanga, kutekeleza na kufuatilia programu za maendeleo ya vijana.
Ameeleza kuwa mifumo hiyo itasaidia kuimarisha uwajibikaji, ushirikiano na upatikanaji wa taarifa zinazohusu utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya vijana nchini.
Amesema tukio hilo limeandaliwa na Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa lengo la kuwasilisha kwa umma hatua zilizofikiwa, matokeo yaliyopatikana na mwelekeo wa Serikali katika kuendeleza vijana katika kipindi cha mwaka mmoja.
Pia litakuwa jukwaa la kukutanisha taasisi za Serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia, wadau wa maendeleo na vijana ili kujadili programu zinazotekelezwa, changamoto zilizopo na fursa zinazoweza kutumika katika kuimarisha maendeleo ya vijana.
Sambamba na uzinduzi wa mifumo hiyo, kutakuwa na maonesho ya bidhaa, huduma na ubunifu unaofanywa na vijana, ambapo wizara za kisekta, taasisi za umma, taasisi za fedha na sekta binafsi zitashiriki kueleza huduma na fursa zinazopatikana kwa vijana.
Amesema maonesho hayo yatatoa nafasi kwa vijana kupata ufafanuzi kuhusu mitaji na mikopo, ujasiriamali, urasimishaji wa biashara, masuala ya kodi, ununuzi wa umma, masoko na teknolojia, mambo yatakayowasaidia kuanzisha, kuendesha na kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Aidha, amesema vijana walionufaika na uwezeshaji katika kipindi cha mwaka mmoja watatoa shuhuda za mafanikio yao, wakiwemo walioanzisha viwanda, mashamba makubwa ya umwagiliaji, wanaojihusisha na ufugaji wa samaki kwenye vizimba pamoja na wale walionufaika na fursa za kushughulikia tenda za Serikali.
Nanauka alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwa maendeleo ya vijana, akisema uamuzi wa kuanzisha Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana umeimarisha usimamizi mahususi wa masuala ya kundi hilo na kuweka mfumo wa kuratibu huduma na fursa zinazotolewa na Serikali pamoja na wadau.
Waziri huyo aliviomba vyombo vya habari kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhabarisha, kuelimisha na kuhamasisha vijana kuhusu fursa zinazopatikana kupitia programu mbalimbali za Serikali na wadau wa maendeleo.
Aidha tukio hilo litafanyika chini ya kaulimbiu isemayo ‘Mwaka Mmoja, Vijana Pamoja’, ikiwa ni fursa ya kutathmini hatua zilizofikiwa, kujifunza kutokana na matokeo yaliyopatikana na kuimarisha ushirikiano katika kutekeleza vipaumbele vya maendeleo ya vijana nchini.