Na Mwalimu Samson Sombi
MAPINDUZI makubwa katika nyanja ya uchumi yanatokana na mazingira bora ya biashara, uwekezaji na uhusiano mwema wa kidiplomasia kati ya nchi na mataifa mengine duniani hasa yale yaliyopiga hatua kubwa katika maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Ni ukweli usiopingika kwamba ukuaji wa sanyansi na teknolojia baina ya nchi na nchi na hata bara moja na bara lingine umetofautiana sana. Ukuaji huu umesababisha utofauti pia katika kasi ya maendeleo baina ya nchi za Afrika na mataifa yaliyoendelea.
Katika hatua nyingine, nchi nyingi za Afrika ikiwamo Tanzania, zimeendelea kupiga hatua kubwa sana katika maendeleo ya sayansi na teknolojia na kwamba uhusiano mwema na mataifa makubwa yaliyoendelea umekuwa na tija kubwa kwa maendeleo ya nchi ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa biashara na uwekezaji mkubwa huku sekta ya viwanda ikipewa kipaumbele.
Kwa kutambua umuhimu wa sekta ya uwekezaji, viwanda na biashara, serikali yetu imekuwa na Wizara ya viwanda na biashara, Wizara ya mipango na uwekezaji, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika kukuza diplomasia ya uchumi na mataifa mengine duniani.
Kasi ya ukuaji wa sayansi na teknolojia duniani inapanua wigo mkubwa wa biashara, uwekeaji na mahitaji makubwa ya viwanda kati ya mataifa yaliyoendelea nan chi za Afrika hali inayosababisha pande hizo mbili kukuza mahusiano ya kidiplomasia ya kiuchumi, pamoja na mambo mengine, nchi zilizoendelea duniani zimepiga hatua kubwa katika sanyansi na teknolojia vikiwamo pia viwanda huku nchi za Afrika zikiwa na utajiri mkubwa sana wa malighafi ambazo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi za Afrika na dunia kwa ujumla.
Mwishoni mwa mwezi Agosti 2018 nchi ya China iliitisha mkutano mkubwa uliofanyika katika jiji la Beijing kati ya nchi hiyo na mataifa ya Afrika. Katika mkutano huo Rais wa China Xi Jinping alisema nchi yake itaendelea kuwekeza katika miradi mikubwa yenye tija kwa China na Bara la Afrika na kwamba nchi hiyo imetenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya uwekezaji Afrika.
Akifungua mkutano huo wa siku mbili, Rais Jinping aliwaambia viongozi na wafanyabiashara wakubwa kutoka Afrika kuwa ushikiano wa China na bara hilo umelenga kuleta maendeleo makubwa Afrika na kusisitiza nchi za Afrika kuchangamkia fursa hiyo muhimu kwa ujenzi imara wa uchumi.
Kumekuwa na ushindani mkubwa sana baina ya China, Marekani na Uingereza katika kufanya biashara na uwekezaji Afrika na Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi wanufaika wa biashara na uwekezaji huo.
Baada ya kuingia madarakani Machi 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alieleza mikakati na dira ya serikali ya awamu ya sita katika eneo la biashara na uwekezaji kwamba ni kuboresha mazingira yake yanayotoa vivutio kwa wafanyabiashara na wawekezaji kuja kwa wingi hapa nchini.
“Nchi yetu imekuwa na changamoto ya kutokuwepo kwa mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji ikiwamo kutokuwa na sera zinazotabirika, urasimu unaokwamisha ustawi wa biashara na uwekezaji. Serikali ya awamu ya sita imekusudia kufanya marekebisho makubwa,” alieleza Rais Samia.
Rais Samia amekuwa akifanya ziara za nje ya nchi ambazo zinaendelea kuifungua nchi yetu, pia Rais amehudhuria mikutano mikubwa ya kimataifa hatua ambayo imeiweka nchi yetu katika ramani ya dunia kwa upande wa biashara na uwekezaji.
Kupitia ziara zake za nje, Rais Samia amekuwa akitafuta fursa za kiuchumi, kuimarisha uhusiano mwema wa kidiplomasia na kuingia mikataba yenye tija kwa nchi.
Fursa hizo za kiuchumi ni katika sekta za viwanda, afya, kilimo, elimu, maji, usafiri wa majini na anga, madini na nyinginezo.
Pia katika ziara hizo, Rais Samia hukutana na mamlaka na Jumuiya za Wawekezaji na Wafanyabiashara wakubwa wa nchi anakotembelea na kubadilishana uzoefu katika sekta hizo.
Mei 31, 2024 Rais Samia akiwa na ujumbe mzito alisafiri umbali wa kilometa 10,200 kutoka Jiji la Dar es Salaam hadi jiji la Seoul Korea Kusini katika juhudi mpya ya kuimarisha uhusino kati ya Tanzania na taifa hilo lililoendelea kiteknolojia la mashariki ya mbali.
Kwa mara ya kwanza katika ziara hiyo ya siku sita, Rais Samia aliambatana pia na baadhi ya wasanii wa filamu nchini ili kupata na kubadilishana uzoefu na kujifunza mambo yanayoweza kuboresha tasnia hiyo hasa ikizingatiwa Korea imepiga hatua kubwa katika sekta ya sanaa.
Tanzania na Korea zimekuwa na uhusiano mzuri kwa zaidi miaka 32 sasa huku Tanzania ikifaidika katika nyanja mbalimbali za maendeleo kutokana na uhusiano huo.
Kwa taarifa zilizopo kwa mwaka 2022, Korea Kusini ambayo ni ya 12 kwa uchumi duniani iliuza kwa Tanzania bidhaa zenye thamani ya Dola 169 milioni huku biadhaa kuu ikiwa ni mafuta ikifuatiwa na mashine za X-Ray na Tanzania inauza Korea Kusini bidhaa zenye thamani ya Dola 37.3 na biadhaa inayoongoza ni tumbaku.
Katika ziara hiyo Tanzania na Korea Kusini Zimetiana Saini mikataba ya ushirikiano kwenye utafiti, uwekezaji na kujenga uwezo wa kuongeza thamani ya madini ya kimkakati yanayopatikana Tanzania kwa wingi hususani nikeli, lithium na kinywe.
Nchi hizo mbili zimetiana saini hati mbili za makubaliano pamoja na tamko la pamoja la kuanzisha mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi (EPA).
Ili kufungua milango zaidi ya ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi, Tanzania na Korea Kusini zimesaini mkataba wa EPA utakaowezesha ushirikiano huo kuwa wa kimkakati hususani katika nyanja za biashara, uwekezaji na viwanda.
Mkataba huo utaiwezesha Tanzania kupokea Mkopo kutoka Korea wa Dola za Marekeni 2.5 bilioni sawa na shilingi 6.5 trilioni kwa ajili ya miradi ya miundombinu kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2024 – 2028.
Mbali na mkataba huo Rais Samia alishuhudia itiaji saini Hati ya maelewano katika Sekta za Uchumi wa Buluu na madini ya kimkakati na pia alishuhudia kusainiwa kwa tamko la utayari wa kuanza majadiliano ya ushirikano wa kiuchumi.
Fedha hizo kwa ajili ya miundombinu za maendeleo zitatolewa chini ya Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kiuchumi wa serikali ya Korea (EDCF) kwa masharti nafuu.
Kwa mujibu wa Balozi wa Tanzania nchini Korea ya Kusini Togolani Mavura, nchi 59 zilizopo barani Afrika, Asia na Ulaya zinafaidika na mkopo wa aina hiyo kutoka EDCF.
Anasema mkopo huo wa Dola bilioni 2.5 ni wa masharti nafuu na una riba ya asilimia 0.01 na unalipwa kwa miaka 40 na una fungate ya miaka 25.
“Yaani unaanza kulipa baada ya mwaka wa 26. Hivyo si kweli kwamba mkopo huo utalipwa kwa miaka mitano,” anaeleza Mavura.
Katika hati za makubaliano zilizosainiwa ni pamoja na ushirikiano katika uchumi wa buluu ambapo Tanzania itashirikiana na Korea ya Kusini katika maeneo ya uvuvi, viwanda vya kuchakata mazao ya bahari, ujenzi wa bandari za uvuvi, teknolojia na tafiti za masuala ya bahari.
Katika hatua nyingine, Rais Samia alihudhuria mkutano wa viongozi wengine wa Afrika uliofanyika katika jiji la Seoul uliojadili kuhusu mustakabali wa ushirikiano wao na utakaochochea maendeleo ya nchi zao.
Katika mkutano huo, Rais Samia alisema ana imani mkutano wa Korea na Afrika utafungua milango ya ushirikiano wa uchumi na technolojia kwa faida ya maendeleo ya Afrika.
Alisema anatarajia nia thabiti ya Korea katika mafanikio ya pamoja na kuungwa mkono kuundwa mpango kazi wa kushirikiana kwenye biashara na uwekezaji bila kusahau sekta binafsi itazaa matunda.
Pamoja na kampuni moja ya Korea kushirikiana na Tanzania kwenye masuala ya madini, Rais Samia amewakaribisha wengine zaidi nchini kwa ajili ya ushirikiano kwenye uchimbaji na utafiti wa madini ya kimkakati.
Juni 6, 2024 baadhi ya mawaziri walioambatana na Rais katika ziara hiyo walieleza manufaa ya ziara hiyo January Makamba alisema “Manufaa yaliyopatikana Korea ni makubwa, ziara hii inafungua ukurasa kati ya Tanzania na Korea na Sifa za Taifa hilo zinajulikana hasa maendeleo ya kisayansi.
Kwa upande wake Waziri wa Mipango na uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo alisema ziara hiyo imeonesha mwanga na nia ya uwekezaji wa Korea Kusini kuwekeza kwenye sekta za madini, mifugo, na kilimo na kwamba itachangia ukuzaji wa biashara kati ya Korea na Tanzania.
“Korea ni Taifa ambalo kwa sasa kampuni zake zimetoka nje ya mipaka yake na kuwekeza hasa nchi za Asia hivyo inawezekana tukawavuta wawekezaji kutoka Korea kuja hapa Tanzania, wenzetu wamepiga hatua kubwa za maendeleo ya teknolojia,” alibainisha Profesa Mkumbo.
Waziri Nape Nnauye alisema wamejifunza namna Korea wanavyotumia technolojia ya habari kuboresha huduma kupitia Tehama na jinsi wanavyokusanya vijana na kuwasaidia kufikia ndoto zao katika ubunifu wa biashara zinazohusu teknolojia na kuwa na mkakati wa kujenga chuo maalum kuwasaidia vijana Wakitanzania.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji anasema “Moja ya mambo makubwa ni kujifunza kwa wenzetu kuwa wanafanyaje na walifikiaje kwenye viwango walivyonavyo leo hii ili tukizalisha bidhaa zetu ziende Korea, Marekani, na masoko yote ya mataifa yaliyoendelea.”