Ziara ya Rais Samia India kukuza sekta ya afya, maji

Na Daniel Mbega,

Dar es Salaam

LEO Jumanne, Oktoba 10, 2023, Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru nchini India kinamtunukia Rais Samia Suluhu Hassan Tuzo ya Nehru kutokana na mchango wake katika masuala ya uongozi na kuziunganisha nchi za Tanzania na India.

Rais Samia anakuwa kiongozi wa pili wa Tanzania kupata Tuzo hiyo ya Nehru kwa Uelewa wa Kimataifa, baada ya Mwalimu Julius Nyerere kupatiwa Tuzo hiyo mwaka 1973.

Tuzo ya Jawaharlal Nehru ya Uelewa wa Kimataifa ni tuzo ya kimataifa inayotolewa na Serikali ya India kwa heshima ya Jawaharlal Nehru, waziri mkuu wa kwanza wa nchi hiyo.

Ilianzishwa mnamo mwaka 1965 na inasimamiwa na Baraza la India la Uhusiano wa Kitamaduni (ICCR) kwa watu “kwa mchango wao bora katika kukuza uelewa wa kimataifa, nia njema na urafiki kati ya watu wa ulimwengu”.

Taarifa zilizopo zinaeleza kwamba, mara nyingi Tuzo hiyo huambatana na fedha taslimu kwa anayepokea ambazo ni Rupia za India milioni 2.5 (sawa na TShs. 75,212,500).

Hii ni heshima kubwa kwa Rais Samia, ambaye amekuwa Mwafrika wa nne kupokea baada ya Dkt. Kenneth Kaunda wa Zambia (1970), Julius Nyerere wa Tanzania (1973), Nelson Mandela wa Afrika Kusini (1979), Léopold Sédar Senghor wa Senegal (1982), Robert Mugabe wa Zimbabwe (1989), Hosni Mubarak wa Misri (2002), na Mwanamazingira wa Kenya, Wangari Maathai (2005).

Watu maarufu wengine waliopata kutunukiwa tuzo hiyo ni Katibu Mkuu wa tatu wa Umoja wa Mataifa, U Thant kutoka Burma ay Mynmar ya sasa (1965), Martin Luther King Jr. wa Marekani (1966), Khan Abdul Ghaffar Khan wa Pakistan (1967), Yehudi Menuhin wa Marekani (1968), Mama Theresa wa India (1969), Rais wa zamani wa Yugoslavia ya zamani Josip Broz Tito (1971), André Malraux wa Ufaransa (1972), Raúl Prebisch wa Argentina (1974), Jonas Salk wa Marekani (1975), Giuseppe Tucci wa Italia (1976), Tulsi Mehar Shrestha wa Nepal (1977), Nichidatsu Fujii wa Japan (1978), Barbara Ward wa Uingereza (1980), Alva Myrdal Gunnar Myrdal wa Sweden (1981), Bruno Kreisky wa Austria (1983), Indira Gandhi (1984), Olof Palme wa Sweden (1985), Javier Pérez de Cuéllar wa Peru (1987), Yasser Arafat wa Palestina (1988), Helmut Kohl wa Ujerumani (1990), Aruna Asaf Ali wa India (1991), Maurice Strong wa Canada (1992), Aung San Suu Kyi wa Myanmar (1993), Mahathir Mohamad wa Malaysia (1994), Goh Chok Tong wa Singapore (1996), Sultan Qaboos wa Oman (2004), Luiz Inácio Lula da Silva wa Brazil (2006), Ólafur Ragnar Grímsson wa Iceland (2007), na Angela Merkel wa Ujerumani (2008).

Kwa ujumla, ziara ya Rais Samia nchini India imekuja wakati mwafaka katika kipindi hiki ambapo mataifa haya mawili yanahitajiana katika kiuchumi, kijamii na kiteknolojia.

Ingawa biashara baina ya Tanzania na wafanyabiashara kutoka bara Hindi ina historia ya karne nyingi zilizopita na uhusiano rasmi wa kiserikali ukiwa umedumu kwa zaidi ya miaka 50, ziara hii ni ina ladha tofauti.

Taifa la India liko njiani kuzipiku Japan na Ujerumani na kuwa taifa la tatu kwa uchumi duniani nyuma ya Marekani na China na linahitaji malighafi zaidi kukuza uchumi wake zaidi.

Tanzania ni miongoni mwa nchi za Kiafrika zenye uchumi unaokua lakini kutoka kuwa nchi masikini hadi ule wa kati na tajiri, inahitaji mitaji, uwekezaji mkubwa na soko la kuuzia malighafi zake duniani.

India inahitaji malighafi na mazao ikiwemo dengu, mbaazi na korosho kutoka Tanzania ili kulisha watu wake wanaokisiwa kufikia bilioni 1.3.

Tanzania inahitaji kutumia mitaji kutoka kwa matajiri wa India na utaalamu wa teknolojia na biashara zaidi ili kukuza uchumi wake.

Vitu vichache katika ziara hii vinaonyesha namna ziara hii ya Rais Samia ya kwanza kufanywa na Rais wa Tanzania nchini India katika muda wa miaka minane, itakavyokuwa tofauti na za miaka iliyopita.

Kukuza sekta muhimu

Ushirikiano kati ya Tanzania na nchi nyingine ikiwemo India ni njia moja wapo ya kupata faida kiuchumi na kidiplomasia kwani tutapata mawazo mapya na ya muhimu kwa nchi yetu na pia tutaboresha yale ambayo yapo yanahitaji ufanisi zaidi.

Miongoni mwa mambo ambayo Rais Samia anayalenga kupitia ziara hii ni ujenzi wa Hospitali kubwa ya Figo nchini Tanzania pamoja na mwendelezo wa Kituo cha Ujenzi wa Chanjo ambazo Tanzania itazalisha na kuuza nje ya nchi.

Mbali ya kuboresha sekta hiyo ya afya, lakini ni wazi kwamba hata sekta ya maji itaendelea kuimarishwa hasa ikizingatiwa kwamba, India imefadhili mradi mkubwa wa maji nchini.

Itakumbukwa kwamba, Julai 7, 2023 wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya India, Dkt. Subrahmanyan Jaishankar, alipokuja nchini, aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa usimamizi mzuri wa fedha zinazotolewa na serikali hiyo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji nchini.

India inafadhili mradi wa upanuzi wa mtambo na mfumo wa maji wa Ruvu Juu na Dkt. Jaishankar alipotembelea mradi huo, alisema mafanikio ya usimamizi mzuri wa miradi ya maji nchini Tanzania yameipa imani kubwa Serikali ya India na hivyo itaendeleza ushirikiano katika kutekeleza miradi mbalimbali ukiwemo mradi wa miji 28 unaogharimu Dola za Marekani milioni 500 sawa na takriban shilingi trilioni 1.2 za Tanzania.

“Napenda uzifikishe salamu hizi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwamba Serikali ya India inaridhishwa na jitihada za Tanzania katika kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya maji unasimamiwa vizuri na thamani ya fedha inaonekana,” Dkt. Jaishankar alimweleza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.

Dkt. Jaishankar alisema, maji ni chakula, maji ni afya, maji ni uhai hivyo mafanikio ya Serikali ya Tanzania katika kuwafikishia wananchi huduma ya maji ni mafanikio ya serikali ya India kwa sababu uhusiano wa serikali ya India na Tanzania umekuwepo kwa muda mrefu na utaendelea kuwepo kwa ajili ya ustawi wa wananchi wa pande zote mbili.

Baadhi ya miradi ambayo imetekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya India ni pamoja na mradi wa kuboresha huduma ya maji kwa Jiji la Dar es Salaam na Chalinze ambao umetekelezwa kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 178.125.

Mradi mwingine ni wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika miji ya Tabora, Igunga, Nzega, Tinde, Uyui, Shinyanga, Shelui na vijiji 102 kwa kiasi cha Dola za Marekani milioni 268.35.

Wakati alipokuja nchini kwa ziara ya siku mbili Julai 9, 2016, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi aliahidi kwamba India itaipatia Tanzania msaada wa Dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kipaumbele.

India pia iliridhia kutoa kiasi kingine cha Dola za Marekani milioni 92 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji kisiwani Zanzibar.

Mara kadhaa Serikali imekuwa ikiwahimiza Watanzania kuongeza uzalishaji wa mazao ya jamii ya kunde hususan dengu kwa kuwa yana soko kubwa nchini India.

Kwa upande wa viwanda, mashirika ya viwanda vidogo ya India na Tanzania yaliwahi kuwekeana saini mkataba ambapo mashirika hayo yatafanya tathmini nchi nzima ya kubaini rasilimali zilizopo katika maeneo mbalimbali na aina ya viwanda vidogo vinavyoweza kuanzishwa kwenye maeneo hayo.

Serikali ya India iliahidi kutoa mkopo nafuu kwa ajili ya kujenga antamizi (incubators) za viwanda vidogo nchi nzima ambapo kupitia antamizi hizo, wananchi watapatiwa mafunzo maalum ya uzalishaji wa bidhaa, biashara na usimamizi wa fedha na baadaye kupewa mitaji kwa ajili ya kuanza shughuli za biashara.

Kwa upande wa Sekta ya Afya, India imekuwa msaada mkubwa kwa Tanzania kwa miaka mingi, ambapo mbali ya kusaidia vifaatiba, lakini pia imekuwa ikisaidia wataalamu pamoja na kupokea wagonjwa wenye uhitaji wa kufanyiwa upasuaji wa kibingwa ambao wanashindwa kupata huduma hiyo hapa nchini.

India kwa sasa ni miongoni mwa mataifa yanayoongoza kwa uzalishaji wa dawa na matumizi ya teknolojia ya kisasa kwenye matibabu.

Rais Samia amewahi kuzungumza hadharani kwamba anaguswa sana na changamoto za kiafya zinazowakabili Watanzania na ziara hii inajibu mojawapo ya changamoto hizo.

Ujenzi wa hospitali ya kupandikiza figo nchini ni ukombozi mkubwa kwa sababu tatizo la figo ni miongoni mwa matatizo yanayoongezeka hapa nchini yakiathiri watu wengi. Matibabu yake ni gharama kubwa na wenye uhitaji wa huduma hiyo huonekana kama wana hukumu ya kifo.

Itakumbukwa kwamba, Machi mwaka 2022 aliyekuwa Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Alfelo Sichwale alisema Watanzania 5,800 walikuwa wanahitaji huduma ya kusafisha damu au kupandikizwa figo.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha kwa kila watu 10, mtu mmoja mfumo wa utendaji kazi wa figo zake hauko vizuri.

Hii ni sawa na makadirio ya asilimia 10 kwa wananchi wote kusumbuliwa na tatizo hilo, huku asilimia 2.4 wakipoteza maisha na asilimia 2.7 wakigundulika kwenye hatua ya mwisho.

Kwenye ziara hiyo ya kihistoria, Rais Samia amekutana na kufanya mazungumzo ya faragha na baadaye mkutano na waandishi wa habari na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi.

Oktoba 4, 2023, Serikali ya Tanzania ilipokea msaada wa magari 10 ya kubebea wagonjwa aina ya Ashok Leyland yenye thamani ya Sh bilioni 1.1 kutoka Serikali ya India.

Si hivyo tu, bali inaelezwa kwamba, hospitali za BLK-Max na MAX-Saket zitaendelea kushirikiana na Tanzania katika utoaji wa huduma za matibabu ya kibingwa bobezi nchini Tanzania.

Hospitali hizo zilizoko jijini New Delhi ndizo zilizoajengea uwezo wataalam kutoka Tanzania taaluma ya kuanzisha huduma za kupandikiza figo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili mwaka 2017, huduma za upasuaji mkubwa wa moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na pia kutoa mafunzo kazini kwa wataalam wa Mifupa na Mishipa ya Fahamu katika Taasisi ya Mifupa MOI.

Hospitali hizo kubwa za kisasa zinatoa huduma mbalimbali za kawaida na za ubingwa bobezi ambapo wana madaktari bingwa na bobezi zaidi ya 4,800 katika fani mbalimbali na zinauwezo wa kuhudumia wagonjwa zaidi ya milioni 3.5 kwa mwaka kutoka katika nchi zaidi ya 135.

India kimbilio la wagonjwa

Kwa miaka mingi sasa, wagonjwa wengi, hususan wa saratani, moyo na figo, kutoka Tanzania na nchi nyingine za Afrika maisha yao yamekuwa yakiokolewa katika Hospitali za Apollo nchini India.

Hata hivyo, Watanzania wanaotibiwa hospitalini huko hufarijika kwa kiwango fulani tofauti na wenzao kutoka nchi zingine ambao hujikuta wakiumia zaidi pale mjadala unapohusu gharama za matibabu.

Wakati wagonjwa kutoka nchi nyingine wakijitegemea katika kugharimia matibabu yao, kwa upande wa Tanzania ni tofauti kidogo, walio wengi wanagharimiwa na serikali pasipo kujali nafasi zao katika taifa wala itikadi zao, sifa yao kuu ni Utanzania wao.

Takwimu za mwaka 2014 kutoka Ofisi ya Mwambata wa Afya katika Ubalozi wa Tanzania nchini India zinaonyesha kuwa Watanzania takriban 25,000 waliomba vibali vya kuingia nchini India kwa ajili ya kupata matibabu.

Kwa mujibu wa taarifa za ofisi hiyo, visa hizo za matibabu ni zile zilizotolewa katika ofisi za Ubalozi wa India nchini Tanzania katika kipindi cha miaka mitatu nyuma.

Taarifa zaidi kutoka ndani ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zinaonyesha kuwa serikali, kupitia wizara hiyo katika kipindi cha Januari, mwaka 2011 na Desemba mwaka 2013 pekee, ilipeleka wagonjwa 2,252 katika hospitali mbalimbali nchini humo kwa matibabu.

Idadi kubwa ya wagonjwa waliopelekwa nchini humo kupitia utaratibu huo wa rufaa za serikali ni wananchi wa kawaida huku viongozi wakiwa asilimia tisa tu ya wagonjwa hao wote.

Magonjwa yenye rufaa zaidi kwenda katika hospitali za India ni pamoja na magonjwa ya moyo ambayo yanayoongoza kwa idadi ya asilimia 28.18 ya wagonjwa wote, yakifuatiwa na saratani yenye asilimia 27.59, figo asilimia 8.53 na magonjwa mengineyo yenye kuchukua asilimia 35.71.

Kwa mujibu wa taarifa za ofisi hiyo ya mwambata wa afya nchini humo, watoto wadogo wenye kusumbuliwa na magonjwa ya moyo, kitaalamu yakifahamika kama “congenital cardiac diseases,” ndio wenye kuongoza katika orodha ya wagonjwa wanaopelekwa nchini India kwa matibabu zaidi.

Uhusiano kati ya Serikali ya Tanzania na hospitali hizo za Apollo nchini India ulianza mwaka 2004 ambapo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iliingia makubaliano rasmi (Memorandum of Understanding), na katika makubaliano hayo wagonjwa kutoka nchini wanaogharimiwa na Serikali hupelekwa katika hospitali hizo kwa ajili ya matibabu ya rufaa.

Rufaa zinazopelekwa kwenye hospitali hizo ni zile ambazo matibabu yake hayapatikani nchini Tanzania kwa sababu ya ukosefu wa vifaa, tiba, wataalamu na baadhi ya dawa ambazo hata kama zingekuwepo nchini bado isingekuwa rahisi kutumika kwa kuwa hakuna huduma ya maabara kwa ajili ya kupima viwango vya dawa hizo mwilini na urekebishwaji wake.

Kabla ya utaratibu wa rufaa kupelekwa nchini India, serikali ilikuwa ikipeleka wagonjwa wake katika nchi za Uingereza, Afrika Kusini, Marekani na Kenya lakini ikabainika kuwa matibabu katika nchi hizo ni ghali ukilinganisha na gharama za matibabu nchini India, wakati ubora wa tiba kati ya nchi hizo na India unalingana.

Takribani asilimia 99 ya wagonjwa wote wanaopelekwa nje ya nchi na serikali hivi sasa, hupelekwa katika hospitali za mtandao wa Apollo nchini India.

Kutokana na kuwepo kwa gharama kubwa za kupeleka wagonjwa nje, Serikali sasa imeamua kuwapatia utalaamu wa kibingwa bobezi madaktari na wahudumu wa afya ili wagonjwa wawe wanapatiwa matibabu nchini, ambapo tayari jitihada za kufanya upasuaji kwa magonjwa mbalimbali zimeanza kufanyika.

Magonjwa ya moyo sasa yanatibiwa nchini Tanzania katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na upandikizaji wa figo nao umeanza.

Jitihada za sasa na Rais Samia za kutaka kujenga Hospitali Kubwa ya kupandikiza Figo siyo tu zitaleta unafuu wa gharama, lakini pia zitapunguza usumbufu hata kwa wagonjwa ambao walikuwa wanalazimika kusafiri nje ya nchi kusaka huduma.

Novemba 2017, Hospitali ya Taifa Muhimbili iliingia kwenye historia ya dunia, baada ya kuanza kutoa huduma ya upandikizaji figo nchini Tanzania kwa mara ya kwanza.

Gharama ya mgonjwa mmoja kupandikizwa figo nchini India ni kati ya Shis. milioni 80 hadi 100.

Mafanikio yaliyopo ni kwamba, baada ya huduma hiyo kuanza kupatikana nchini, mgonjwa mmoja sasa itamgharimu kati Shs. milioni 21 kwa ajili ya kupandikizwa figo.

Gharama hizo zina tofauti ya Shilingi milioni 60 ambazo serikali imeziokoa kutokana na kuanza kutoa huduma ya upandikizaji figo nchini, kwa kila mgonjwa, sawa na asilimia 75.

Tuna kila sababu ya kumpongeza Rais Samia kwa kufanya ziara hii muhimu ambayo italeta manufaa makubwa kwa Taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *