
Aliyewahi kuwa mshindi katika mashindano ya wanasayansi chipukizi Ojung’u Laizer (aliyekaa katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu mashindano ya wanasayansi chipukizi yaliyoandaliwa na Shirikisho la Wanasayansi Chipukizi (YST) kwa lengo la kukuza na kuibua vipaji vya wanafunzi nchini.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SHIRIKISHO la Wanasayansi Chipukizi (YST) limesema kuwa kwa mwaka huu 2025 miradi 45 ya kisayansi imechaguliwa kuonyeshwa katika mashindano ya sayansi yanayotarajiwa kufanyika Septemba 18, mwaka huu.
YST imesema miradi hiyo ya wanafunzi wa Sayansi chipukizi itakayoonyeshwa inalenga kutoa suluhisho za vitendo katika maeneo ya usalama wa usafirishaji na mifumo ya kidijitali ya udhibiti wa foleni za Barabarani, usalama migodini na matumizi ya Akili Mnemba (AI) katika usalama na uhifadhi wa chakula.
Hayo yamebainishwa jana jijini Dar es Salaam na Mwanzilishi Mwenza wa YST Dk. Gozibert Kamugisha wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Kamugusha alisema miradi hiyo ya wanafunzi itakayoneshwa italenga pia kutoa suluhisho la matumizi ya Akili Mnemba (AI) katika uchunguzi wa kitabibu, upatikanaji na uboreshaji wa umeme, kuboresha mifumo ya mifereji ya maji kwa kutumia AI pamoja na uhifadhi wa mazingira.
“Miradi hii yote ikilenga kutoa suluhisho za maendeleo, itaoneshwa katima maonesho ya Kitaifa ya YST mwaka huu ambayo yatawakutanisha wanafunzi kutoka mikoa yote ya Tanzania, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Carolyne Nombo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi,” amesema
Kamugisha aliongeza kuwa dhumuni la kufanya maonesho hayo UDSM ni kutengeneza jukwaa la kuwaleta pamoja wanasayansi chipukizi kutoka shule za sekondari la kuwakutanisha na wanasayansi wabobevu kutoka chuo hicho kikuu na vingine ili kupata ushauri juu ya namna bora ya kuboresha gunduzi zao.
“Mpango huu wa kuibua na kulea vipaji vya kisayansi kwa vijana unadhaminiwa na Karimjee Foundation (KFI) / Toyota Tanzania. Tunaamini kupitia mpango wetu huu vijana ambao ni wanasayansi chipukizi wataendelea kuhamasika zaidi katika kufanya gunduzi mbalimbali za kisayansi.” amesema
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Karimjee Foundation, Caren Rowland, amesema tangu mwaka 2012 wamekuwa wadhamini Wakuu wa YST na kwamba kila mwaka wamekuwa wakitoa ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa wanafunzi ambao wameshinda katika kundi la washindi wa jumla na kundi maalumu la elimu katika mashindano hayo.
Amesema Karimjee Foundation imefadhili wanafunzi washindi 49 kwa ufadhili wa masomo ya elimu ya juu na mwaka huu wataongeza wengine wanne na kufikisha jumla ya wanafunzi 53 na kuongeza kuwa wengi wa wanafunzi hao kwa sasa wako vyuoni na baadhi yao wanaendelea kadi ngazi ya uzamili na hata uzamivu.
“Tunajivunia kuona vijana hawa wenye vipaji wakitumia Sayansi na ubunifu kutafuta suluhu za changamoto za jamii zero, ushirikiano wetu na YST sambamba na serikali kupitia Shule za serikali, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na COSTECH umeimarisha zaidi jitihada hizi,” Amesema Rowland.
Naye aliyewahi kuwa Mshindi wa Jumla wa mashindano hayo kutoka Shule Sekondari Lumumba iliyopo visiwani Zanzibar, Ramlat Hamad alisema anaishukuru YST na Karimjee Foundation kwani wamekuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi wengi wenye ndoto za kupata elimu ya juu.
Amesema kutokana na kushinda alifanikiwa kupata ufadhili kutoka Karimjee Foundation ambao umemsaidia kupata elimu ya juu na kwa sasa anaendelea kutimiza malengo yake aliyojiwekea.