Yanga yaanza ligi kwa kishindo

Na Mwandishi Wetu, Kagera

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, timu ya Yanga SC, imeanza kwa ushindi wa mabao 2-0 mbele ya Kagera Sugar, katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Kaitaba, mkoani hapa.

Hicho kinakuwa ni kipigo cha pili mfululizo kwa Kagera Sugar ambao katika mchezo wao wa kwanza walifungwa na Singida Black Stars.

Katika dakika 45 za kwanza, licha ya Yanga kutengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini kikwazo ilikuwa ni kuvusha mpira nyuma ya Kipa, Ramadhan Chalamanda ambaye kwa nyakati tofauti aliwakatalia Prince Dube, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz Ki nafasi za kufunga.

Hata hivyo kipindi hicho, Yanga SC ilifunga bao la kwanza kupitia kwa Max Nzengeli ambaye alipokea pasi kutoka kwa Zouzoua.

Kipindi cha pil, kilianza kwa wenyeji Kagera Sugar kufanya mabadiliko ambapo Kocha, Paul Nkata alimtoa Godfrey Manyasi na nafasi yake kuchukuliwa na mlinzi wa kati, Denis Bukenya.

Mabadiliko hayo yalionekana kuwanufaisha Kagera Sugar ambapo walianza kucheza kwa kujiamini huku wakifunga mianya ya Yanga kutengeneza nafasi zaidi za kufunga mabao.

Zikiwa zimesalia dakika mbili kabla ya kipyenga cha mwisho, Clement Mzize ambaye aliingia kipindi cha pili kuchukuwa nafasi ya Dube, alifunga bao la pili alipokea pasi safi kutoka kwa Aziz Ki na bao hilo liliwahakikishia Yanga SC alama tatu muhimu katika mchezo wao wa kwanza wa msimu.

Katika mchezo huo, kiungo wa Kagera Sugar, Nassor Kapama alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora baada ya kuonesha uwezo mkubwa licha ya timu yake kupokea kichapo.

Kikosi cha Yanga mara baada ya mchezo huo kitarejea tena uwanjani, Septemba 14 kuwaalika Mashujaa katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam katika muendelezo wa mechi za ligi hiyo.

Mchenzo mwingine;

KMC 1-1 Coastal

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *