Na Badrudin Yahaya
BAADA ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya pili mfululizo, Klabu ya Yanga imezidi kutanua mbawa kwenye viwango vya CAF ambapo sasa ni rasmi wamepanda kwa nafasi mbili.
Katika orodha mpya ambayo imezingatia viwango vya klabu katika misimu mitano iliyopita tangu 2020/21 hadi 2024-25, Yanga imepanda kutoka nafasi ya 13 hadi nafasi ya 11 baada ya kufikisha alama 29.
Yanga SC imeongeza alama 1 baada ya kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo na alama hizo zinaweza kuongezeka kwa alama tatu kama watatinga robo fainali, nne kama watafika nusu fainali, tano kama itakuwa washindi wa pili na sita kama watafanikiwa kunyakuwa taji.
Timu ambazo zimeporomoka kwenye nafasi za juu na kuipisha Yanga ni Petro Athletico de Luanda ya Angola ambayo imeshindwa kutinga makundi baada ya kuondoshwa na FC Maniema ya DR Congo na timu nyingine ni Raja Casablanca ambayo msimu uliopita haikushiriki kabisa.
Wakati mambo yakizidi kuwa mazuri kwa watani zao wa jadi, upande wa pili timu ya Simba SC, imeshuka kwa nafasi moja wakitoka nafasi ya saba hadi ya nane kwa kipindi hicho cha misimu mitano.
CR Belouizdad ambayo msimu uliopita ilicheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, imefanikiwa kutinga tena hatua hiyo kwa mara ya pili mfululizo na hivyo kufanya jumla wawe wamekusanya alama 31 wakiwashusha Simba.
Pia TP Mazembe ambayo msimu uliopita ilicheza nusu fainali msimu huu imetinga hatua ya makundi ambapo sasa wapo nafasi ya saba wakiwa na alama 30.5 sawa na Simba ambao kwasasa wameshuka hadi kwenye nafasi ya nane.
Kulingana na viwango hivyo vipya, kuelekea kwenye droo ya Oktoba 7 ya hatua ya makundi, Yanga ambao wapo Ligi ya Mabingwa Afrika wamesogea hadi katika Pot 2 ambayo pia inatimu za Pyramids, CR Belouizdad na Raja Casablanca tofauti na msimu uliopita ambapo walikuwa Pot 3.
Kwenye Pot 1 kuna Al Ahly, TP Mazembe, Esperience na Mamelod Sundowns ambazo kati ya hizo moja itapangwa kundi moja na Yanga kwenye kundi moja.
Kwa upande wa Simba, wao licha ya kushuka lakini kutokana na ushiriki wao katika michuano ya Shirikisho, watakuwa katika Pot 1 ambayo hii itakuwa ni rekodi mpya ndani ya soka la Tanzania.
Katika Pot 1, Simba atakuwa sambamba na timu za Zameleki, RS Berkane, USM Alger na hivyo hawatoweza kupangwa pamoja.