Na Badrudin Yahaya
TIMU ya Yanga SC, imehitimisha mechi zake za hatua ya makundi ya Kombe la Mapinduzi kwa kulazimishwa suluhu na timu ya KVZ.
Katika mchezo huo, Kocha wa Yanga, Miguel Gamond, aliwapa nafasi wachezaji wengi vijana akichanganya na baadhi ya wazoefu.
Hata hivyo licha ya timu zote kujaribu kutafuta bao la ushindi lakini milango iliendelea kuwa kimya hadi kipyenga cha mwisho.
Mchezaji mpya wa Yanga, Augustine Okrah, alipata nafasi ya kuingia kipindi cha pili lakini hakudumu uwanjani baada ya kupata jeraha la kichwani na kutolewa nje nafasi yake kuchukuliwa na Farid Mussa.
Pia kikosi cha Yanga kwa mara nyingine kilimkaribisha kikosini beki wao raia wa DRC, Joyce Lomalisa ambaye aliumia tangu mwanzo wa mwezi uliopita kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa matokeo hayo, msimamo wa Kundi C, timu ya Yanga, imejihakikishia kumaliza kileleni wakiwa na alama 7 na KVZ wamemaliza nafasi ya pili wakiwa na alama 5.
Michuano hiyo hatua ya makundi itamalizika kesho kwa Simba SC kuumana na APR ya Rwanda, mchezo ambao utapigwa saa 2:15 usiku huku Jamhuri FC na Jamusi ya Sudan Kusini zikitangulia kucheza saa 10 jioni.