Na Mwandishi Wetu
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameizawadia timu ya Yanga SC shilingi milioni 20 ‘Goli la Mama’ ikiwa ni sehemu ya hamasa baada ya ushindi wao wa mabao 4-0 dhidi ya Vital’O kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akikabidhi fedha hizo kwa niaba ya Rais Samia, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, alisema lengo la kutoa fedha hizo ni kuzihamasisha zaidi timu kufanya vizuri tangu hatua za awali.
“Rais alikuwa anatoa fedha hizi kuanzia hatua ya makundi lakini msimu huu tumeona ni vyema kuanza mapema ili kuzipa morali timu kwa kupata matokeo ya ushindi,” alisema.
Rais Dkt. Samia ndio amekuwa mwanamichezo namba moja nchini ambaye amekuwa akizitakia kheri na mafanikio timu za michezo mbalimbali zinazopambania taifa.
Katika msimu wa 2022-23, Rais Samia alizindua rasmi ‘Goli la mama’ ambapo ni fedha taslimu zinazotolewa uwanjani kwa timu ya Tanzania inayowakilisha nchi iwe klabu au timu ya taifa.
Licha ya kuwa fedha hizo zimekuwa zikitumika kama posho na hongera kwa wachezaji lakini pia zimekuwa na mchango mkubwa katika kuinua morali ya wachezaji kwenye kupambana uwanjani.
Kwa upande wake, Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi licha ya kuibuka na ushindi huo lakini alionesha masikitiko yake kwa wachezaji wake kushindwa kutumia vyema nafasi nyingi za wazi za kufunga.
Alisema kwenye mchezo huo wangeweza kuibuka na ushindi mkubwa zaidi lakini alijivunia kwa matokeo hayo ya 4-0.
“Ndani ya kipindi cha kwanza tungeweza kufunga mabao zaidi ya matatu, tumepoteza nafasi nzuri ndio maana nimefurahi zaidi baada ya kufanya mabadiliko,” alisema.
Yanga inatarajia kurudiana na timu hiyo Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam ambapo mshindi wa jumla atasonga mbele hadi kwenye hatua ya mtoano.
Katika hatua ya mtoano, Yanga itacheza na aidha SC Villa ambao walifungwa nyumbani kwa mabao 2-1 dhidi ya Commercial Bank Of Ethiopia.