Yanga sasa akili kufuzu robo fainali CAF

Na Zahoro Mlanzi

Klabu ya Yanga, imesema kwa sasa mipango yao ni kuhakikisha inajiandaa vizuri katika mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ili ifuzu kucheza robo fainali.

Yanga ilivunja mwiko uliodumu kwa miaka 25 na kutinga hatua hiyo baada ya kuiondosha Al-Merreikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 3-0.

Akizungumza na Tanzania Leo, Rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said, amesema baada ya kutinga hatua hiyo nguvu zao wataziweka katika kuhakikisha wanafika robo fainali.

“Malengo yetu ya awali ilikuwa ni kucheza hatua ya makundi, hilo tumefanikiwa na sasa tumejiwekea lengo lingine ni kuhakikisha tunapiga hatua zaidi kwa kucheza robo fainali,” amesema Said.

Amesema hakuna kinachoshindikana katika mpira wa miguu hususani kwa uwekezaji waliofanya ndani ya klabu hiyo ndio maana wanaona inawezekana.

Ametoa wito kwa wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kuendelea kuisapoti timu yao katika michezo mbalimbali.

Katika hatua nyingine, timu hiyo imefikia salama jijini Mbeya ambapo kesho itakuwa uwanjani kuumana na Ihefu FC katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Highland Estate jijini humo, Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ally Kamwe, amesema kikosi chao kipo imara na hawana majeruhi.

“Tunaomba mashabiki wetu wa Nyanda za Juu Kusini wajitokeze kwa wingi kwani kikombe tulichowapa Namungo, JKT Tanzania na KMC lazima na wao watakunywa tu, dozi itaendelea kama kawaida,” ametamba Kamwe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *