Na Mwandishi Wetu
MABINGWA wa Tanzania Bara, timu ya Yanga SC, imeendelea na upepo mzuri wa mavuno ya zawadi za ‘Goli la Mama’ linalotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, baada ya kuitandika Vital’O ya Burundi bao 6-0 na kuvuna sh. milioni 30 kutoka kwa rais huyo.
Mchezo huo wa marudiano hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika, ulichezwa juzi usiku katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi, jijini Dar es Salaam, ambapo uliiwezesha Yanga kutwaa fedha hizo kutoka kwa Rais Samia, kama zawadi kwa timu za Tanzania zinazopata mabao ya ushindi katika mechi za Kimataifa.
Akizungumza katika makabidhiano hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, alisema mama hana mbambamba katika kukamilisha ahadi yake kwa timu za Tanzania ambazo ni Yanga, Simba, Azam FC na Coastal Union ambazo zinawakilisha nchi katika michuano ya kimataifa.
“Mama hana mbambamba, ukifunga lazima upate zawadi yako, kama ilivyokuwa kwa Yanga ambao leo wamevuna sh. milioni 30 kutoka kwa Rais wetu wa nchi.
“Katika mechi ya kwanza Yanga walivuna sh. milioni 20 kwa mabao yao manne, hivyo ukichanganya na ushindi wao wa bao sita waliopata, timu hii itakuwa imevuna sh. milioni 50 kutoka kwa Rais Samia, kama zawadi yao nono ya Goli la Mama,” alisema Msigwa.
Kwa upande wa Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, aliwataka wachezaji wao wacheze kwa bidii ili wapate mabao mengi, wakiamini watatumia fedha hizo kama sehemu ya bonasi kwa vijana wao.
“Niliwaambia wachezaji wetu nyie chezeni kwa nguvu mpate mabao mengi kwa sababu bonasi anayo Rais Samia, ambapo amekuwa na utaratibu mzuri wa kutoa zawadi kwa timu za Tanzania zinazofanya vizuri, Alisema Said.
Rais huyo wa Yanga mwenye mafanikio makubwa tangu apate nafasi ya kuiongoza klabu hiyo, alisema kila tunda linalopatikana kwa timu za Tanzania, limesababishwa na moyo wa Rais Samia katika kuzitupia macho timu katika mashindano mbalimbali.
(Kwa taarifa zaidi usikose kusoma Gazeti lako la Tanzania Leo linalotoka kila Jumatatu hadi Ijumaa)