Yanga, Azam FC kukipiga Azam Complex J’mosi

Na Badrudin Yahaya

MTENDAJI Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Bara, Almasi Kasongo, amesema mchezo kati ya wenyeji Yanga dhidi ya Azam FC uliopangwa kufanyika, Novemba 2, utachezwa katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Kasongo amesema awali Yanga waliomba mchezo huo ufanyike katika Uwanja wa Benjamini Mkapa lakini wamiliki wamekataa ombi hilo kwasababu ya ukarabati unaoendelea.

Amesema kwasababu taarifa ya ombi kukataliwa imetolewa hivi karibuni na kwa mujibu wa kanuni Yanga hawana tena uwezo wa kuomba mchezo wao huo upelekwe sehemu nyingine ndio maana imeamuliwa kuwa mechi itachezwa katika uwanja wao wa nyumbani ambao wanautumia katika mechi nyingine.

“Kwasasa tunafanya majadiliano na wamiliki wa uwanja wa Azam Complex kuona ni utaratibu gani utatumika kuhusu mashabiki na hata viingilio na taarifa hiyo itatoka,” amesema.

Timu hizo zinatarajia kukutana katika mchezo wao wa kwanza msimu huu ambao unatarajia kuwa na mvutano wa aina yake.

Yanga mara ya mwisho wanakumbukumbu ya ushindi wa mabao 4-1 kwenye mchezo wa fainali ya Ngao ya Jamii lakini Azam wao wanajivunia ushindi wa 2-1 katika mechi ya ligi raundi ya pili msimu uliopita.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana katika dimba la Azam Complex, ilikuwa ni Aprili 6, 2022 ambapo Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 bao la ushindi likifungwa na Fiston Mayele.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *