Yajue ‘mabifu’ ya makocha yaliyotikisa EPL 

LONDON, England

FUKUTO kubwa linaloendelea katika soka la Uingereza kwasasa ni bifu kati ya Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola dhidi ya Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta.

Wawili hao wakati fulani wamewahi kufanya kazi pamoja ambapo Arteta alikuwa msaidizi wa Guardiola ndani ya Etihad.

Hata hivyo zama zimebadilika ambapo kwasasa kila mmoja anafanya kazi katika timu mbili zenye upinzani wa kuwania taji kwa misimu miwili mfululizo.

Joto kubwa liliibuka wiki iliyopita ambapo miamba hiyo ilikutana katika mechi yao ya kwanza msimu huu na matokeo kuisha kwa sare ya mabao 2-2 ndani ya dimba la Etihad.

Kwenye mechi hiyo ambayo ilizua mikasa mingi ndani ya uwanja, imesababisha maneno kuendelea hadi baada ya mechi na sasa makocha wa timu mbili ambao waliwahi kuwa marafiki sasa wameingia katika vita kali ya kisiasa.

Hivi karibuni Guardiola alinukuliwa akidai kuwa upande wa Arsenal umekuwa ukiwadhihaki na hivyo alitangaza vita dhidi yao.

Pia Kocha wa Arsenal, Arteta baada ya kuiongoza timu yake kuifunga Leicester City, 4-2 alijibu kwa kusema kuwa ana muheshimu Guardiola lakini kama itatangazwa vita yeye hana uwezo wa kuzuia.

Hii sio mara ya kwanza kwa upinzani mkali wa makocha kuibuka kwa timu mbalimbali na kupitia makala haya, tutajikumbusha mabifu ambayo yaliwahi kutikisa.

Sir Alex Ferguson v Rafael Benitez

Msimu wa 2008-09 uliibuka upinzani mkali wa kuwania EPL kati ya Manchester United dhidi ya Liverpool. Hadi kufikia Januari, 2009, Liverpool walikuwa kileleni lakini nyuma yao walikuwa Man United ambao walikuwa hawapoi.

Hiyo ilimfanya Rafael Benitez kuibuka kwenye mkutano na waandishi wa habari na kuanza kueleza jinsi Sir Alex Ferguson alivyokuwa anafanya ushawishi kwa waamuizi ili timu yake ishinde.

Jambo hilo lilizua mgogoro mkubwa baina yao na mwisho wa msimu Man United walishinda taji kwa tofauti ya alama nne dhidi ya Liverpool.

Katika kitabu cha Ferguson alieleza alifanikiwa kushinda taji msimu huo kwasababu Benitez aliutoa ushindani wao ndani ya uwanja na kuupeleka kuwa binafsi.

Jose Mourinho v Arsene Wenger

Jose Mourinho alivyoingia kwa mara ya kwanza ndani ya Chelsea chini ya tajiri Roman Abramovich alionekana kufanikiwa zaidi kulingana na sera zao za usajili na ushindi wa mataji.

Hata hivyo haikuwa hivyo kwa Arsene Wenger ambaye mwaka 2005 alimkosoa wazi wazi kutokana na mbinu zake uwanjani akisema kuwa ni za kizamani.

Mourinho alipata nafasi yake ya kuja kurejesha mashambulizi mwaka 2013 alivyorudi Chelsea kwa mara ya pili ambapo alimuita Wenger ni bingwa wa kufeli “specialist in failure”.

Sir Alex Ferguson v Arsene Wenger

Kwenye miaka 1990 hadi miaka ya 2000 mwanzoni utawala ulikuwa ni kwa timu za Manchester United na Arsenal.

Timu hizo zilishinda takribani kila taji kati ya 1996-2004 huku makocha wakiwa ni Sir Alex na Arsene Wenger kweye mabenchi yao.

Wenger alikuwa ni mgeni katika soka la Uingereza akijiunga na Arsenal mwaka 1996 tofauti na Ferguson ambaye kipindi hicho alikuwa na miaka 10 tayari.

Wakati fulani Wenger alipendekeza kuwa ratiba ibadilishwe kwasababu ilikuwa inawabeba zaidi Man United.

Hali hiyo ilizua balaa na katika moja ya majibu yake Ferguson alisema kuwa “huyu jamaa ni mgeni amekuja zake kutoka Japan alafu anataka kutufundisha namna ya kusimamia ligi”.

Hiyo ilitafsiriwa kuwa kashfa na upinzani wao ulidumu kwa muda mrefu wakiwa na vita ya chini kwa chini.

Antonio Conte v Jose Mourinho

Jose Mourinho anaweza kuwa ni mmoja kati ya makocha ambao wameingia katika vita na mabifu mengi dhidi ya makocha wenzie wa upinzani.

Hii inatokana na kariba yake ya kupenda kuongea na hasa maneno ya shombo.

Mwaka 2016 wakati akiwa na kikosi cha Man United walialikwa ndani ya Stamford Brigde kucheza dhidi ya Chelsea ya Antonio Conte kwenye mechi ya ligi.

Matokeo ya mechi hiyo ilikuwa ni Man United kuambulia kichapo cha mabao 4-0 lakini kilichomkera Mourinho haikuwa matokeo bali ushangiliaji wa Antonio Conte.

Katika mahojiano yake baada ya mechi Mourinho alinukuliwa akisema kuwa “makocha wengine wamekuwa wakishangilia kama makatuni” hiyo ilikuwa ni meseji ya moja kwa moja kwa Conte ambaye naye alijibu kwa kusema “mtoto mdogo huyo”.

Kwa kukumbusha tu, Mourinho pia amewahi kuwa na bifu zito dhidi ya Pep Guardiola wakati wawili hao wakiwa katika timu za Barcelona na Real Madrid.

Mabifu mengine kwa ufupi ni Arsene Wenger v Sam Allardyce (Bolton miaka ya 2000) na Sir Alex Ferguson v Kevin Keegan (Newcastle United, 1996).

(Imeandaliwa na Badrudin Yahaya kwa msaada wa mashirika ya habari ya kimataifa)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *