Wizara ya Katiba na Sheria yaibuka mshindi Maonesho ya Sabasaba

Na Salha Mohamed

WIZARA ya Katiba na Sheria, imeibuka mshindi wa kwanza kundi la wizara zote zilizoshiriki maonesho ya 49 ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) 2025.

Akizungumza Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini, amewataka wananchi kutembelea banda la Katiba na Sheria ili kupata elimu inayohusu masuala ya Sheria.

Sagini ametoa wito huo alipotembelea maonesho ya 49 ya kimataifa ya biashara Sabasaba yanaendelea katika viwanja vya Mwàlimu Nyerere vilivyopo Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Ameishukuru Serikali inayoingozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya maboresho yaliyofanywa katika viwanja hivyo.

Naibu Waziri Wizara ya Katiba na Sheria, Jumanne Sagini (katikati), akizungumza na mmoja wa wananchi waliofika kupewa huduma

Akiwa kwenye maonesho hayo, alitembelea Banda la Mahakama, Wakala wa Vizazi na Vifo(RITA) ambapo amebaini ushiriki wa watu wengi waliojitokeza kuomba vyeti vya kuzaliwa.

Amesema wananchi wanapaswa kufahamu kuwa huduma ya utoaji wa vyeti upo hadi ngazi za wilaya hivyo hakuna sababu ya kusubiri wakati wa maonesho ya Sabasaba ambapo wengine hukutwa vyeti vyao vimeshapelekwa kwenye wilaya wanapotoka.

Akizungumzia Banda la Katiba na Sheria, Sagini amesema wanastahiki kuwa washindi wa kwanza ambapo wananchi wameridhishwa na utolewaji wa huduma.

“Niwapongeze wataalamu wetu, mawakili wanaotoa huduma ya msaada wa kisheria niwapongeze Waziri na Katibu Mkuu kukubali kuleta idara zote za Katiba Sheria hapa ambao pia hutoa Elimu ya masuala mbalimbali yanayoratibiwa na hizo Idara,”amesema.

Akizungumzia kampeni ya Msaada wa Kisheria, Sagini amesema huduma hiyo imeleta matokeo chanya ambapo serikali imeridhishwa na utolewaji wa huduma hiyo.

“Wizara ya Katiba na Sheria inalifanya jambo hili kuwa endelevu kwa kupeleka maofisa ngazi ya Halmashauri ambapo wanawasaidia wananchi kwa kushirikiana na taasisi zingine za kisheria,”amesema.

Ameongeza wameweka kipaumbele kutoa elimu kwa wananchi kuhusu sekta kama ardhi.

Amefafanua licha ya migogoro ya ardhi, pia kuna migogoro ya ndoa ambapo elimu inatakiwa kutolewa kwa kushirikiana na maofisa waliopo kwenye mamlaka ngazi za Mitaa na wataalamu wa msaada wa kisheria waliopo ambao ni wadau wa huduma za msaada wa kisheria kwa kuelimisha wananchi kuhusu ndoa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *