Na Zahoro Mlanzi
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo, amesema ifikapo mwaka 2030, kila mkoa unatakiwa kuwa na viwanda vikubwa vitatu kwa lengo la kuleta mapinduzi ya sekta hiyo, kuongeza ajira na kuinua uchumi.
Jafo ameyasema hayo wakati wa kufunga Maonyesho ya pili ya Kimataifa ya Viwanda Tanzania (TIMEXPO 2024) yaliyoandaliwa na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) chini ya uratibu wa Kampuni ya Radian Limited.
Amesema mbali ya viwanda vitatu vikubwa, mikoa pia inatakuwa kuwa na viwanda vya kati vitano na vidogo visivyongua 30 kwa lengo la kuongeza soko la ajira si chini ya watu 185,000.
“Mpango huu wa kuleta maendeleo ya viwanda na biashara unatarajia kuanza mwakani ambapo kuanzia sasa, kila mkoa unatakiwa kutenga maeneo ya kujenga viwanda hivyo ili kuufanisha,” amesema Jafo.
Amefafanua Serikali ya chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuleta maendeleo makubwa katika sekta ya viwanda, biashara na nyinginezo.
Amesema serikali ina malengo ya kuendeleza nchi kwa kuwapatia Watanzania fursa nyingi huku akitoa wito kwa wamiliki wa viwanda kuzalisha bidhaa zenye ubora ili kupata wateja wengi na kuleta ushindani katika masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.
Kwa mujibu wa Jafo, serikali inaendelea kuimarisha Diplomasia ya Uchumi na kuwataka wenye viwanda na wafanyabiashara kuchangamkia fursa zinazopatikana bila kusahau kuwa biashara duniani ni huria na yenye ushindani.
“Hivyo naomba kusisitiza umuhimu wa wazalishaji wetu kuzalisha bidhaa zenye ubora na zinazoendana na matakwa ya soko, natoa wito kwa Taasisi zetu mbalimbali za serikali kuwa wasimamizi waelekezi na siyo wasimamizi wakwamishaji hususani kwa viwanda.
“Nawahakikishia wenye viwanda na wazalishaji wote kuwa wizara yangu itaendelea kusimamia sekta hii katika kuhakikisha kuwa azma ya serikali ya kukuza na kuendeleza sekta ya wiwanda nchini inafikiwa,” amesema.
Jafo pia ametoa wito kuendelea kujenga ushirikiano kwa serikali na taasisi zake mbalimbali katika kufanya majadiliano ili kuhakikisha kuwa changamoto mbalimbali zinazowakabili wawekezaji zinatatuliwa.
Katika hatua nyingine, Jafo amesema serikali inakuja na mpango mkubwa wa kufufua viwanda ambavyo havifanyi uzalishaji kwa sasa ukiwa kutoa fursa kwa wawezaji binafsi.
“Mfano kuna kiwanda kikubwa cha korosho Tunduru na kusababisha ajira zaidi ya 604 kupotea. Pia kuna viwanda zaidi ya 11 Nachingwea, Lindi na Mtwara ambavyo kwa sasa havifanyi uzalishaji. Nawaomba wawekezaji kuwa tayari kuwekeza katika viwanda ambavyo serikali itavitangaza kuhitaji wawekezaji wapya,” amesema.
Pia Jafo ameziomba taasisi za kibenki kupunguza riba ili kuwazesha wawekezaji wa ndani kupata mitaji.
Amesema wawekezaji wengi hawana mtaji wa kutosha na hivyo kutoa wito kwa taasisi za fedha kupunguza riba na kuwavutia wawekezaji wengi kupata mitaji na kuiwezesha nchi kuwa na viwanda vingi na kukuza biashara na uchumi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Latifa Khamis, amesema maonyesho hayo yamefanikiwa kutokana na washiriki kuongezeka kutoka 79 na kufikia washiriki 257.
“Nitoe wito kwa wenye viwanda kushiriki maonesho yanayokuja ambayo tunaamini yatakuwa na mafanikio zaidi,” amesema Latifa.
Wakati huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI), Leodgar Tenga, ametoa wito kwa wenye viwanda jijini Dar es Salaam na mikoa mingine kushiriki katika maonesho yajao ili kupanua wigo wa biashara na kupata washirika.