Watumishi wa umma zingatieni falsafa ya Samia katika uwajibikaji na uadilifu

Na Samson Sombi

FALSAFA ya uongozi inasema kiongozi anapaswa kuwa mfano wa kuigwa na wale anaowaongoza, anapaswa kuwapa matumaini makubwa na kuwa mstari wa mbele katika harakati za kutatua kero zao na kuwaletea maendeleo na kwamba uchapaji kazi wake hutoa kishawishi kikubwa kwa wananchi kuunga mkono juhudi zake.

Kiongozi anapaswa kuwa mzalendo wa kweli kwa nchi na watu wake, kuwatumikia wananchi bila ubaguzi wowote na kuwa kimbilio la wanyonge ambao utatuzi wa shida zao ndio kipimo cha ubora na umakini wake katika nafasi yake ya uongozi.

Mara nyingine kiongozi ni lazima awe mtu wa kwanza kugundua viashiria vya matatizo na changamoto zinazowakabili wananchi katika eneo lake kuwa mbunifu, kufanya kazi kwa weledi katika hatua mbalimbali za kutafuta ufumbuzi wa kero za wananchi na kuwajengea imani kubwa anaowaongoza kwamba anachapa kazi kwa maslahi ya wengi.

Kiongozi anaelezwa kuwa ni kielelezo cha msingi cha kazi, utumishi na uadilifu na anawajibu mkubwa wa kuongoza kwa kufuata na kuzingatia miiko ya uongozi huku akitanguliza mbele maslahi mapana ya umma katika kuwahudumia na kuepuka tamaa ya kujilimbikizia mali kwa jasho la wengine.

Ni wajibu wa kiongozi kuwasikiliza wananchi na kutafuta njia sahihi za kutatua kero zao, ikiwa ni pamoja na kutoa nafasi kubwa kwa wao kushiriki katika utatuzi wa kero hizo kwa sababu kuna baadhi ya kero ambazo husabishwa na wananchi wenyewe.

Kiongozi wa dini wa watibeti Dalai Lama aliwahi kusema “madhumuni ya msingi wa maisha yetu ni kusaidia wengine kama huwezi kuwasaidia basi angalau usiwaumize”

Baadhi ya watendaji na watumishi wa serikali katika ngazi mbalimbali wamekuwa ni chanzo cha mgogoro na kero kwa wananchi wa maeneo yanayoyaongoza kutokana na kutokuwajibika kwao kwa kuzingatia na kufuata sheria na kanuni za utumishi wa umma, badala yake wamekuwa mwiba kwa maendeleo na ustawi wa jamii. Vitendo hivi kusababisha wananchi kupeleka lawama kwa viongozi wakuu wa nchi.

Muundo wa serikali unaanzia chini kwenye serikali za mitaa kwa maana ya viongozi wa vijiji, vitongoji na mitaa kuna watendaji wa kata, kuna watendaji ngazi ya wilaya, ngazi ya mkoa, wakurugenzi wa halmashauri na majiji, mawaziri na makatibu wakuu katika wizara mbalimbali. Timu hii kubwa na wengine wanatosha kabisa kumsaidia Rais wan chi kupeleka huduma kwa wananchi kwa wakati.

Bila shaka kila kiongozi anafahamu majukumu yake na mipaka ya kazi yake katika eneo lake. Nchi haiwezi kuongozwa na mtu mmoja tu tukatarajia maendeleo makubwa, Urais ni taasisi kubwa yenye nguvu na uwezo mkubwa wa kutoa huduma kwa taifa na kuleta ustawi wa jamii.

Rais anapoteua watendaji ambao kimisingi ni wasaidizi wake anakuwa na mategemeo na matumaini makubwa na wateule hao katika nafasi zao za kuwatumikia wananchi na kwamba nchi hujengwa na wananchi wenyewe chini ya viongozi shupavu na wazalendo kwa taifa lao.

Kwa mara ya kwanza jumatano ya machi 31, 2021 Rais Samia Suluhu Hassan alifanya mabadiliko madogo katika baraza la mawaziri akiwabadilisha baadhi katika wizara kwa kile alichosema ilikuwa ni muda mfupi tangu walipoteuliwa kushika nafasi akaahidi kuendelea kufanya mabadiliko mbele ya safari na kuwataka kuchapa kazi kwa weledi kuwahudumia watanzania.

“Fanyeni kazi kwa lengo moja kwamba tunawatumikia watanzania sisi ni watumishi wa watanzania wote. Nitakuwa na kipimo cha mabega yenu nikiona mtu mabega yanazidi kupanda juu najua huyo siyo mtumishi bali anafurahia juu ya kiti chake, ni jambo ambalo si tarajii natarajia kusikia mko huko kwa wananchi kila mmoja kwa sekta yake anachapa kazi” alisisitiza Rais Samia.

Kwa nyakati tofauti viongozi wakuu wa serikali Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wamekuwa wakiwakemea watendaji na watumishi wa umma wanaofanya kazi kwa mazoea, wabadhirifu na wanaopenda kupokea rushwa kwamba vitendo hivyo huchonganisha serikali na wananchi wake.

Wingi wa watendaji na watumishi wa umma katika maeneo na ngazi mbalimbali nchini unapaswa kutoa matunda chanya na ufanisi mkubwa kwa wakati unaotarajiwa mgawanyo wa madaraka ambao uko kwa mujibu wa katiba ya nchi unapaswa kurahisisha shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo na sio kuchelewesha maendeleo kama ilivyo katika baadhi ya maeneo hapa nchini.

Viongozi wakuu kitaifa wanapofanya ziara za kikazi katika maeneo mbalimbali hapa nchini hupokelewa kwa mabango yenye jumbe za malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kwamba wanakero nyingi na za muda mrefu ambazo hazijapatiwa ufumbuzi ilhali viongozi na watendaji wapo katika maeneo hayo.

Aprili 2021 wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua Rais Samia aliwataka kwenda kutimiza majukumu yao ya msingi na wanapokwama waende wazungumze naye.

“Nendeni mkawe wabunifu sitegemei uzembe wa makusudi, nendeni mkafanye maamuzi mnachelewa sana kufanya maamuzi kama mlichelewa wakati ule sasa mko na mama nimeshawaambia ukifanya ovyo tutazinguana unataka kufanya umekwama njoo tuzungumze aliwaeleza wateule hao akitaka kazi yenye tija kwa taifa.

Katika msimamo wake wa kutaka uadilifu na weledi katika kazi Februari 27, 2023, Rais Samia alitoa onyo la mwisho kwa watendaji serikalini wanaogombana ofisini na kuacha kutimiza majukumu yao ya msingi.

“Jambo hili silipendi kwa sababu nitakuwa kama nawadekeza vile. Maana yake mnagombana huko ili nipangue nimweke huyu nimtoe hapa, nasema mara ya mwisho silipendi jambo hili nataka nikiwapanga mfanye kazi sio sababu ya kugombana na kuharibu kazi” anafafanua Rais Samia.

Mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe ulimfanya makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango kuweka rehani nafasi yake ya umakamu kama mradi huo ulioanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2014, hautatoa maji ifikapo Juni 2024.

Alhamisi ya Machi 21, 2024 Dkt. Mpango alitembelea mradi huo unaosimamiwa na wizara ya maji na kusema kwamba kama mradi hautakamika kufika mwezi Juni 2024 ataachia ngazi na kuacha kwake kazi hakutawaacha salama watendaji hao.

“Amri ya Rais Samia ni kwamba maji yatoke Mwanga na Same ifikapo Juni mwaka huu. Nataka nirudie tena mjipange vizuri wasimamizi, wakandarasi na wataalamu bahati nzuri wanauwezo, usiku na mchana maji yatoke. Mradi huu umekuwa kero kwa wananchi wa maeneo haya ni takribani miaka 19 imepita tangu umeanzishwa na kuanza kutekelezwa mwaka 2014” alisema Dkt. Mpango na kuongeza. 

“Kila mtu atimize wajibu wake kurudi kwa Rais kwamba maji hayatoki. Mimi nitaacha kazi kama maji hayatoki hapa mimi nikiacha kazi hao wengine sijui Katibu Mkuu na Waziri wake mimi sijui kwa hiyo tuelewane vizuri.” Dk Mpango alimtaka Waziri wa maji na wasaidizi wake kuweka kambi hapo kuhakikisha maji yanatoka ili kuwaondolea kero wananchi hao waliosubiri maji kwa miaka mingi.

Mbali na mradi huo Februari mwaka huu Waziri mkuu Kasim Majaliwa akiwa ziarani mkoani Mara alielezwa na kujionea mapungufu mengi katika utekelezaji wa miradi mingi ikiwamo ya maji na ujenzi wa shule za sekondari mkoani humo.

Majaliwa alitoa maagizo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi wa ubadhirifu wa fedha za umma zilizopotea katika miradi hiyo na wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

Kumekuwa na migogoro ya muda mrefu ya ardhi katika maeneo mbalimbali, vituo vya afya na huduma nyingine za kijamii kero na migogoro ni wajibu wa watendaji kutafuta ufumbuzi kwa wakati ili kuleta ustawi na maendeleo ya wananchi.

Jumatano ya Machi 13, 2024 Rais Samia aliwaapisha baadhi ya viogozi wa serikali wakiwamo wakuu wa mikoa na kuwataka kusimamia kwa uadilifu miradi ya maendeleo katika maeneo yao na ukusanyaji mapato kwa sababu kuna mitandao inayochepusha fedha za umma.

Rais Samia alisema kuna miradi mikubwa ya kitaifa kama vile mabwawa, reli, madaraja makubwa, barabara na miradi ya maji. Yote hii inahitaji fedha na usimamizi wenye uzalendo na uadilifu mkubwa ili kukamilika kwa wakati na kuleta matunda kwa wananchi wenye kiu ya maendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *