Watu 400,000 wapo hatarini kuambukizwa TB kwa mwaka

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

KITENDO cha wagonjwa 27,033 wenye maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu (TB) kushindwa kuanza tiba ya ugonjwa huo mapema, kunawaweka watu 407,225 katika hatari ya kupata ugonjwa huo kwa mwaka mmoja.

Takwimu za Mpango wa Taifa wa Kutokomeza kifua Kikuu na Ukoma, mgonjwa wa TB ambaye hajapata matibabu anaweza kuambukiza watu 15-20 kwa mwaka.

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam katika mkutano mkuu wa mwaka wa wataalamu wa kifua kikuu na ukoma.

Alisema hadi sasa, watu 132,000 huambukizwa kifua kikuu nchini ambapo watu 25,800 hufariki dunia sawa na wastani wa watu 70 kila siku.

Aliwaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, kujumuisha magonjwa hayo kwenye shughuli zote za afya ambazo wanazitekeleza.

“Nikienda kila mkoa nitaangalia ni namna gani waratibu wa mikoa na Wilaya wanavyoshirikishwa katika shughuli zinazofanyika kwa rasilimali zilizopo,” alieleza.

Lengo la kujumuisha magonjwa ta TB na ukoma kwenye shughuli zinazofanywa na waganga hao ni kuendelea kuibua wagonjwa wapya ambao hawajaanza tiba.

Akizungumzia mikakati ya kutokomeza TB nchini, katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. John Jingu kupitia taarifa iliyosomwa na mwakilishi wake, Catherine Joachim, alisema Tanzania imewekewa lengo na umoja wa Mataifa kutokomeza maambukizi ya TB ifikapo 2030.

Mikakati iliyowekwa ili kufikia lengo hilo ni kuibua na kutibu wagonjwa wa TB kwa asilimia 90 ambapo hadi sasa wamefikia asilimia 78.

Lengo lingine ni asilimia 90 ya walioanzishiwa dawa wawe wamepona ambapo asilimia 95 ya walioanzishiwa dawa wamepona hivyo kupunguza vifo kwa asilimia 69 ya lengo la asilimia 90 walilojiwekea.

Dkt. Jingu alisema mkakati mwingine uliowekwa ni kupunguza maambukizi na vifo vitokaNavyo na TB, kuanzisha tiba kinga kwa makundi yaliyo katika hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa huo.

Makundi hayo ni watu wenye maambukizi ya UKIMWI, wachimbaji madini na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Mratribu wa Tiba Kinga na Kifua Kikuu na Ukoma kutoka Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Magonjwa hayo, Dkt. Allan Tarimo, alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 zinazotambulika na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa na watu wengi wenye kifua kikuu.

Kila mwaka, mwatu 100,000,195 wana kifua kikuu hivyo kupitia mkutano huo wataangalia namna ya kuboresha huduma ili kuibua wagonjwa wapya.

Ugonjwa huo husambaa kwa njia ya hewa wakati watu walioambukizwa wanapokohoa, kupiga chafya au kutema mate, ugonjwa huo huathiri mapafu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *