Na Mwandishi Wetu, Iringa
WAKIMBIAJI zaidi ya 350, wakiwemo kutoka Bara la Ulaya na Asia, wamejitokeza kukimbia mbio za Great Ruaha Marathon zilizokuwa na ujumbe wa kulinda vyanzo vya maji na kutangaza utalii wa ndani.
Mbio hizo zilifanyika mwishoni mwa wiki kwa mara ya kwanza ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Wakimbiaji kutoka Bara la Ulaya, waling’ara zaidi katika mbio za kilometa tano, 10 na 21 za wanawake na wanaume huku watanzania wakitanua bila upinzani katika mbio za kilometa 42.
Katika mbio za kilometa 5 wanawake, Mjerumani Regina Runmers, alitumia dakika 32 kushinda mbio hizo huku Nicola Schliter akitumia dakika 59 kushinda za kilometa 10 na Julia May akitumia saa 1:49 kuwa mshindi wa pili wa kilometa 21.
Wengine walioingia nafasi tano za juu na kuahidi kuanza mapema maandalizi ya kushiriki mbio zitakazofanyika tena mwakani ni pamoja na Yohannes Boneff, Warren Zambetakis, Emmanuel Manas, Faye Osborn, Emanuel Eser, Bruce Arndtt na Ucly Heichogan aliyekuwa mshindi wa tatu wa mbio za kilometa 10 wanawake.
Kwa upande wa mbio za kilometa 42, wanawake watanzania walioshinda walikuwa Mbisa Luhalwa aliyetumia saa 3:21 na Shamia John aliyetumia saa 3:50 huku nafasi ya kwanza kwa wanaume ikienda kwa Tumaini Habie aliyetumia saa 3:07, wa pili Leonard Ilapsha saa 3:42 na ya tatu ilienda kwa mzee wa zaidi ya miaka 60, Yona Mwalusamba aliyetumia saa 3:59 kuwagaragaza vijana.
Watazania wengine waliochomoza katika nafasi tatu za juu za mbio za kati ya kilometa tano na 21 ni pamoja na Greyson Mahimbi, Hoza Mbuya, Winnifrida Njilima, Magreth Daudi, Arifu Juma, Beni Kashiririka na Manfred Kimano, Atuganile Mfikwa, Catherine Simfukwe na Pascal Bilingi, Cresto Muhonja, Issack Kivamba na Samwel Nyangula.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mbio hizo, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi , Godwell Ole Meing’ataki, amesema Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) litatoa ofa kwa washindi wote wa kwanza wa mbio hizo kutalii kwa siku mbili katika hifadhi hiyo kwa gharama zao.