Washiriki 1500 kuadhimisha miaka 60 Chuo cha Tengeru

Na Sarah Moses, Dodoma

JUMLA ya washiriki 1500 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wanatarajia kuhudhuria maadhimisho ya miaka 60 ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD) ambayo yatafanyika Novemba 20 hadi 22, 2023.

Hayo aliyasema jana jijini Dodoma Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima ambapo alisema kuwa, pamoja na maadhimisho hayo kutakuwa na Kongamano la Wataalamu wa Kada ya Maendeleo ya Jamii Tanzania.

Alisema kuwa lengo kuu la kongamano ni kutoa fursa ya wataalamu kujadiliana juu ya mchango wa sekta ya maendeleo ya jamii na changamoto kwenye maendeleo ya taifa pamoja na kuendelea kubuni mbinu za kutekeleza mipango ya Serikali ya awamu ya sita katika kuwezesha wananchi kujiletea maendeleo endelevu kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka.

Kauli mbiu ya kongamano hilo ni “Sekta ya Maendeleo ya Jamii: Msingi Imara wa Uwezeshaji wa Wananchi.”

Alisema kuwa katika kuelekea maadhimisho hayo shughuli mbalimbali zinatarajiwa kufanyika kama vile, mutano mkuu wa Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka Sekretarieti na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mkutano wa Chama cha Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii, Maonesho ya shughuli za Maendeleo ya Jamii, Maonesho ya Taasisi na Vyuo vinavyotoa fani ya Maendeleo ya Jamii na Mijadala ya kitaaluma.

“Shughuli nyingine muhimu itakayofanyika katika kilele cha maadhiimisho ya miaka 60 ya Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru ni uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa bweni la wasichana lenye uwezo wa kulaza wanafunzi 568 na kumbi pacha za mihadhara yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1008 kwa pamoja.

“Mradi huu uliogharimu shilingi bilioni 4.8 zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan umekamilika na tayari umeanza kutumika,” alisema Dkt. Gwajima.

Alisema, jumla ya washiriki 1500 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar watashiriki kongamano wakiwemo kutoka, Sekretarieti na Mamlaka za Serikali za Mitaa,Serikali Kuu,Mamlaka mbalimbali za Serikali, Vyuo na Taasisi za elimu ya Juu, Mashirikia yasiyo ya Kiserikali, Mashirika ya kimataifa,Mashirika ya dini,Mabonde ya Maji,Majeshi, Taasisi za kifedha na Sekta binafsi,

Aidha, kwa wahitimu wa zamani wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru (Alumni), popote walipo watumie fursa ya maadhimisho ya miaka 60 kurudi nyumbani baada ya mafanikio waliyoyapata kupitia mafunzo mbalimbali kutoka Chuoni.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Cha Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD) Dkt. Bakari George alisema wamejianda vizuri na kongamano hilo nakusema kuwa mpaka sasa Maafisa Maendeleo 500 wameshajisajili kwaajili ya kushiriki kongamano  hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *