Wasakeni watuhumiwa wa mimba za wanafunzi Songwe

Na Mwandishi Wetu, Songwe

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Francis Michael na Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa huo, wahakikishe wanawasaka watu wote wanaotuhumiwa kuwapa mimba watoto wa kike. 

Tangu Januari hadi sasa, Mkoa huo una kesi 59 za wasichana walioacha shule kwa sababu ya ujauzito lakini ni kesi mbili tu zimeeenda mahakamani.

Majaliwa alitoa agizo hilo jana akiwa katika ziara ya siku tatu mkoani humo na kuhoji kesi 57 kati ya 59 ziko wapi.

“Nani anazuia kesi hizi zisiende mahakamani? Jeshi la Polisi, kwanini hatuwafikishi watuhumiwa kwenye vyombo vya sheria?” alihoji na kueleza kuwa, kesi hizo 59 ni kwa shule za sekondari pekee.

“RC na Ma-DC wote kaeni na Kamati zenu za Ulinzi mbainishe wahusika, hakikishe hatua kali zinachukuliwa dhidi ya wote waliohusika,” alisema Majaliwa baada ya kukagua ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana Ileje.

Aliwakemea vijana wanaopenda kutembea na watoto wa shule akiwataka waache tabia hiyo mara moja kwani wanakatisha maisha ya baadaye ya watoto hao.

“Sheria iko wazi katika kosa hili, adhabu yake ni miaka 30, kijana kabla hujamfuata binti jiulize una miaka mingapi, tukikufunga utarudi ukiwa mzee,” aliongeza.

Akisisitiza haja ya kuwalinda mabinti, alisema hao ni watoto wetu, tunapaswa kuwalea ili wakue, kuja kushika majukumu ya nchi kwani Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewekeza kwao kwa kutoa elimu bila ada.

“Tunapaswa kuhakikishe wanatimiza ndoto zao kwa hiyo tuwalee ili waweze kuhitimu,” alisisitiza na kuwaomba Masheikh na wachungaji wakemee tabia hiyo kupitia mahubiri kwenye ibada.

Katika hatua nyingine, Majaliwa aliwapongeza wana-Ilejekwa kujenga maabara ya kompyuta kwenye shule hiyo yenye mikondo ya kidato cha kwanza hadi cha nne ili kuhimiza matumizi ya TEHAMA.

“Nimefurahi kuona mna jengo maalumu la TEHAMA, hii inaakisi malengo ya Rais Dkt. Samia kutaka TEHAMA, isambae nchi nzima,” alisema.

Alisema pia amefurahi kusikia halmashauri hiyo ina lengo la kuifanya shule hiyo iwe na kidato cha tano na sita.

“Mkurugenzi Mtendaji fanyeni maamuzi ili madarasa ya kidato cha tano na sita yajengwe, muweze kuwapa fursa watoto wa kike katika Wilayah ii.

“Pia mtatoa chachu kwa  hawa wa kidato cha kwanza hadi cha nne ili wasome kwa bidii,” alieleza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *