
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) kimewataka wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbalu za uongozi.
Aidha, amewahimiza kuhakiki taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ili kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa TAWLA, Tike Mwambipile, ametoa rai hiyo wakati wa maadhimisho ya miaka 35 ya chama hicho, yaliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, yaliyokwenda sambamba na kongamano maalum la kutafakari mafanikio, changamoto na mwelekeo wa baadaye wa chama hicho wenye mchango mkubwa katika kulinda na kutetea haki za wanawake na watoto nchini.
Mwambipile amesema kwa sababu mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi wanatamani kuona wanawake wengi wanajitokeza kugombea ili kupata fursa ya kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi.
“Wanawake tujitokeze kugombea hizo nafasi tusiwaachie wakaka au wanaume, kwani na sisi tunaweza kuchukua hizo nafasi na tukazifanyia kazi vizuri, tunataka kuona bungeni pale asilimia imefika 50 kwa 50,” amesema Mwambipile.
Aidha, amesema pamoja na mafanikio waliyoyapata katika kipindi cha miaka 35 bado kuna kazi kubwa ya kufanya ikiwamo kuendelea kushinikiza mabadiliko ya sheria ya ndoa inayoruhusu mtoto mwenye miaka 14 hadi 15 kuolewa.
Amesema wanataka pia kuona sheria ya elimu inaingizwa kipengele cha kusema kwamba mtoto wa kike atakapopata ujauzito arudi shuleni kuendelea na masomo.
“Japo kuna jitihada za serikali katika jambo hilo ambazo zimechukuliwa sasa hivi watoto wakike waliopata ujauzito wanarudi shuleni lakini haipo kwenye sheria hivyo tunatamani iwepo kwenye sheria, pia tunatamani kuona tunakuwa na sheria moja ya ukatili wa kijinsia,” amesema.
Hata hivyo amesema lengo kuu la mkutano huo wa kuadhimisha miaka 35 tangu kuanzishwa kwa TAWLA ni kufanya tathmini ya safari ya chama hicho tangu kiliposajiliwa mwaka 1990 hadi sasa mwaka 2025, pamoja na kuweka mikakati ya mbele.
“Katika kujitafakari, tumeona ni muhimu kuchagua maeneo maalum ya haki ambayo kama chama tumeshayafanyia kazi au tunaweza kuyafanyia kazi kwa ufanisi zaidi. Maeneo hayo ni pamoja na haki za ardhi, magonjwa yasiyoambukiza, pamoja na haki za watoto hasa tukitazama suala la mimba za utotoni na ukatili wa kijinsia,” amesema
Alieleza kuwa licha ya changamoto zilizokuwepo miaka ya nyuma kama mfumo dume, ambapo wanawake walikosa fursa za umiliki wa ardhi au kushiriki uongozi, mafanikio makubwa yamepatikana. Leo hii, Tanzania ina viongozi wa juu wanawake akiwemo Rais na Spika wa Bunge, jambo ambalo linaakisi mabadiliko chanya katika jamii.
“Katika miaka hiyo ya mwanzo, tulikuwa na mawakili wanawake wasiozidi 10, leo hii ni zaidi ya 4,000. Tumeona pia wanawake wakipenya katika taaluma nyingine kama uhandisi na hata katika ngazi za Kata wanawake wengi sasa wanamiliki mali, wanafanya biashara na kushika nyadhifa za uongozi,” aliongeza.
Kwa upande wake, Wakili Scholastica Ndyanabo, amesema TAWLA inajivunia mafanikio yake ya miaka 35, hasa katika kuwasaidia wanawake na watoto kwenye masuala ya kisheria kama mirathi, migogoro ya ardhi na ndoa.
“Tumeweza kuwafikia watu zaidi ya milioni saba ndani na nje ya nchi. Wanawake na watoto ni makundi ambayo mara nyingi hayapewi kipaumbele cha huduma za kisheria, na sisi kama taasisi tumejikita kuwapa msaada huo muhimu,” amesema Ndyanabo.

