Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SERIKALI kupitia Mjasili wa Vyama vya Siasa nchini, iko katika mkakati wa kutoa elimu kwa jamii kuhakikisha wanawake wanashiriki kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga (pichani), aliyasema hayo bungeni jijini Dodoma wakati wa Bunge la 12, Mkutano wa 13.
Nderiananga alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Anatropia Theonist kwa niaba ya Waziri Mkuu.
Katika swali lake, Theonest alitaka kufahamu wanawake wangapi wamekuwa wabunge wa majimbo na madiwani katika chaguzi tatu mfululizo zilizopita.
Akijibu swali hilo, Nderiananga alisema Serikali inatambua, kuthamini ushiriki wa wanawake katika siasa.
Kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama Siasa itaendelea kutoa elimu kwa wanawake na makundi mbalimbali kuwajengea uwezo wa kujiamini, kugombea nafasi hizo kwani kundi hilo lina mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.
“Niwatoe hofu wanawake wenzangu, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anawajali, kuwathamini wanawake na tutaendelea kufanya vizuri ili kuhakikisha tunawajumuisha wanawake katika ngazi zote za maamuzi.
“Serikali inatambua ushiriki wa wanawake katika shughuli za kisiasa na maeneo mengine, katika eneo hili mkakati uliopo ni kutoa elimu kwa wanawake kujiamini na kuthubutu,”alisema.
Aliongeza kuwa, Serikali inatarajia kupeleka mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa itakayovitaka vyama hivyo kuwa na sera itakayoweka muongozo mahususi wa kujumuisha wanawake kugombea nafasi za uongozi.
Alifafanua kuwa, kuanzia 2010 hadi 2020, zilifanyika chaguzi tatu katika ngazi ya Ubunge na Udiwani. Katika chaguzi hizo, wabunge wanawake 73 walishinda chaguzi hizo, kuchaguliwa kuwa Wabunge wa Majimbo, upande wa Madiwani, wanawake 654 waliichaguliwa kuwa Madiwani katika kata husika.