
Na Mwandishi Wetu, Kigoma
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema mpango wa Serikali itakayoongozwa naye katika miaka mitano ijayo, ni kuufanya Mkoa wa Kigoma kuwa wa kimkakati.
Kutokana na mpango huo, amesema mkoa huo hautatambulika tena kwa sifa ya mwisho wa reli, badala yake, utakuwa kitovu cha biashara na maendeleo nchini.
Dkt. Samia ametoa kauli hiyo leo, Jumapili Septemba 14, 2025 alipozungumza na wananchi wa Kigoma Mjini, katika mkutano wa kuhitimisha kampeni zake za urais mkoani Kigoma, tayari kuanza safari ya kwenda visiwani Zanzibar.
Amesema ili kufikia lengo hilo, amejizatiti kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji inayounganisha mkoa huo na njia zote yaani barabara, reli, anga na majini.
Dkt Samia amesema Kigoma ni sehemu muhimu ya Reli ya Kisasa ya (SGR), kwa kuwa kipande cha sita Tabora-Kigoma na saba, Uvinza-Musongati vitajengwa mkoani humo.
“Tumekamilisha sehemu ya kwanza na pili ya Dar es Salaam hadi Dodoma na sehemu zote zilizobaki, ya tatu, nne na tano ambayo ni Mwanza-Isaka tutaikamilisha mwaka huu ya sita ambayo ni Tabora-Kigoma na mwisho Uvinja-Musongati kazi inaendelea,” amesema.



