ZAIDI ya wananchi 1,200 wamepata huduma za matibabu na kusikilizwa katika banda la Taasisi ya Tiba ya Mishipa na Ubongo Muhimbili (MOI) kwenye maonesho ya 48 ya kimataifa ya biashara sabasaba.
Hayo yamebainishwa jana na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Orest Mushi, wakati Menejimenti ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) ilipotembelea banda hilo, lengo likiwa kuona utoaji huduma za MOI kwa wananchi.
Menejimenti hiyo imeridhishwa na utoaji wa huduma ya ushauri na elimu ya matibabu ya mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu katika banda hilo.
“Leo tumekuja katika banda letu la MOI hapa Sabasaba kwaajili ya kujionea huduma zetu tunazotoa kwa wananchi wetu, banda letu linatoa huduma za kibingwa za mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu kwa wananchi ambapo mpaka sasa zaidi ya wagonjwa 1,200 wameshaonwa na kuchunguzwa pia zaidi ya wagonjwa 300 wamepewa rufaa ya kuja MOI ili wapate matibabu zaidi.” alisema Mushi.
Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kufika banda la MOI ili kupata ushauri bure juu ya lishe bora, vipimo mbalimbali vya magonjwa ya mifupa, ubongo na mgongo pamoja na viungo bandia.
Mkurugenzi wa huduma za uuguzi MOI, Fidelis Minja, amesema Taasisi ya MOI imejipanga vizuri kuwapokea wagonjwa wote waliopewa rufaa ya kwenda kupata matibabu katika taasisi hiyo.