Na Salha Msangi, Dar es Salaam
BAADA ya kukamilika kwa zoezi la uandikishaji, orodha ya wapiga kura inabandikwa kuanzia leo katika sehemu za matangazo ya uchaguzi kwenye vijiji na mitaa.
Lengo ni waliojiorodhesha wakague orodha hiyo ili kuomba aidha kurekebisha majina, kubadilisha taarifa zilizoko katika orodha hiyo au kufuta jina lililoorodheshwa kwa vile aliyeorodheshwa amefariki.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, ameyasema hay oleo jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
“Ukaguzi huo utafanyika kwa muda wa siku 7 kuanzia Oktoba 21 -27, 2024. Hivyo, wananchi wote waliojiandikisha ni muhimu mkajitokeza kuhakiki orodha hiyo,”amesema.
Ametoa rai kwa wananchi wenye sifa za kuchaguliwa kuwa viongozi wajitokeze kuanzia Oktoba 26, hadi Novemba Mosi, 2024 ili waweze kutimiza haki yao ya kikatiba ya kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi huu.
Aliongeza kuwa, zoezi la kuchukua na kurudisha fomu litafanyika ndani ya siku saba kwa tarehe nilizozitaja.