- Walitamani kifundishwe mpaka Cameroon kurahisisha utawala
Na Daniel Mbega
“NDUGU zangu ulimwenguni kote, kama shahidi katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki, nina uhakika Kiswahili ni lugha yenye uwezo wa kuvuka mipaka.”
Hivyo ndivyo Rais wa Burundi, Evariste Ndaishimiye, alivyoanza salamu zake kwa njia ya video za kuutakia ulimwengu maadhimisho mema ya kwanza ya Siku ya Kiswahili Duniani Julai 7, 2022 yaliyofanyika kwenye Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.
“Ni vizuri kuzungumza lugha moja kwa sababu tunaposhiriki mawazo tunakuwa kitu kimoja, tunakuwa na maono sawa, na kufanya kazi pamoja. Hii inatupa matumaini ya wakati bora ujao kwa watu wetu hivyo tuungane tufanye kazi kwa umoja na sauti moja. Shukrani kwa Waafrika wote wanaoendelea kudai kuwa Kiswahili kifanywe lugha rasmi ya Afrika.”
Tayari Kiswahili ni lugha rasmi inayotumiwa na jumuiya za kimataifa kuanzia Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN).
Rais Ndaishimiye akasema, “lugha hiyo imeonesha kwamba jumuiya ya kimataifa inaweza kuja pamoja na lengo moja. Kiswahili huzungumzwa nchini Burundi, huzungumzwa nchini Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC hata nchini Rwanda.”
Na katika kuonyesha namna jitihada za Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika kukipigania Kiswahili ulimwenguni, Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi, katika ujumbe wake wa siku hiyo alioutoa kwa Kiswahili alisema, Msumbiji inaamini kutambulika kwa lugha ya Kiswahili kimataifa ni tunu na heshima kubwa kwa wazungumzaji wote wa lugha hiyo duniani.
“Kiswahili ni lugha inayokua kwa kasi sana na yenye umuhimu mkubwa. Kuzungumza Kiswahil ni kurahisisha mawasiliano na kuunganisha watu mbalimbali. Kiswahili ni kielelezo cha kipekee cha desturi na utamaduni wetu, ustaarabu pamoja na fikra zetu. Kiswahili kinatuwezesha kupata habari, elimu, mawazo mapya pamoja na kumiliki sayansi na teknolojia.”
Akaongeza: “Kiswahili si lugha ya mitaani tu, bali kinatumika bungeni, kinafundishwa katika vyuo mbalimbali duniani, kinasikika kwenye radio, televisheni au runinga.”
Kinazungumzwa sana Burundi
Ukifika katika Jiji la Bujumbura, hasa katika Wialaya ya Buyenzi, upo mtaa maarufu wa Buyenzi ambao unafahamika zaidi kama ‘Uswahilini’. Ni eneo ambalo halina tofauti na maeneo ya Tandale au Manzese katika Jiji la Dar es Salaam.
Hapo utakutana na utamaduni kama ule wa Pwani ya Afrika Mashariki, watu wanazungumza Kiswahili na utakuta vijiwe vingi tu vya kahawa, huku baadhi ya wenyeji, hasa wanaume, wakiwa wametinga misuli na kanzu, kama watu wa Pwani. Hata chakula chao, Maisha na mitindo ya mavazi ni ya Kiswahili.
Ingawa lugha hiyo inazungumzwa sana katika maeneo mengine nchini Burundi, lakini Mtaa wa Buyenzi ndiyo kitovu chake. Yapo maeneo mengi nchini humo kama Kamenge, Bwiza, Buterere, Makamba, Rumonge, Cibitoke (Rugombo), Muyinga, Gitega, Nyanza-lac na kwingine ambako wanazungumza sana Kiswahili, licha ya kwamba lugha zao kuu ni Kirundi na Kifaransa, ingawa na Kiingereza nacho kinazungumzwa.
Kwa maana nyingine, anachokisema Rais Ndayishimiye wala siyo bahati mbaya, bali ni lugha ambayo inafundishwa hata shuleni kuanzia chekechea hadi katika vyuo, ingawa kuna changamoto kadhaa ambazo serikali inajitahidi kuzitatua.
Silaha ya Wajerumani
Mnamo mwaka 1885 Ujerumani ilianzisha koloni lake katika Afrika Mashariki likihusisha mataifa ambayo leo ni Tanzania Bara, Burundi na Rwanda. Hii ilikuwa ni baada ya kuanzisha makoloni yake katika Cameroon, Namibia na Togo katika mwaka 1884.
Koloni hili la Ujerumani katika Afrika Mashariki lilikuwa na ukubwa wa eneo la kilometa za mraba 994,996 likihusisha Burundi na Rwanda ya sasa, Tanzania Bara (Tanganyika) na eneo la Pembetatu la Kionga (Kionga Triangle) katika mdomo wa Mto Ruvuma, ambalo lilikuwa kama mpaka baina ya Koloni la Ujerumani na lile la Ureno la Msumbiji. Eneo hili lilirudi kwa Ureno mwaka 1916 baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.
Katika kuuangalia mzozo kwenye Koloni hili (Reichskolonialamt), inabainika kuwa Kiswahili kilitumika na kufundishwa sana katika koloni la Wajerumani (kama vile katika shule ya Wajerumani huko Gitega).
Mzozo huo ulihusu ufadhili wa Kamusi ya Kirundi, ambayo ilipendekezwa na mmisionari Mkatoliki van der Burg lakini ikakataliwa na Gavana wa Ujerumani wa wakati huo, Gustav Adolf Graf von Götzen, ambaye alipendekeza Kiswahili badala yake kwa sababu kilikuwa kinazungumzwa zaidi.
Kutokana na misafara ya biashara kutoka pwani ya Afrika Mashariki kuingia bara, lugha ya Kiswahili ilikuwa imezungumzwa kihistoria kuzunguka fukwe za Ziwa Tanganyika tangu nusu ya pili ya karne ya 19. Mamlaka za kikoloni za Kijerumani, ambazo zilihimiza kuenea kwa Kiswahili katika Tanganyika, kitovu cha Afrika Mashariki ya Kijerumani, hasa mwanzoni mwa karne ya 20, ziliisaidia lugha hiyo kama njia ya kukabiliana na uenezaji wa Kiingereza, hata hivyo, zilihusika na kuanzishwa kwa lugha hiyo hapo awali.
Wajerumani “walipendezwa sana na Kiswahili hivi kwamba walifikiria kukipandikiza hadi Cameroon” wakati wa ukoloni kwa sababu ilionekana kuwa silaha yao ambayo ingekifunika Kiingereza, lugha kuu ya wakoloni.
Kiswahili hakikuwahi kusambaa sana Burundi wakati huo kama ilivyokuwa chini ya uvamizi wa Wajerumani kule Tanganyika. Shule ya kwanza ya Usumbura (Bujumbura) ilianzishwa mwaka 1909 na Mkazi wa Kijerumani, ambaye alichagua Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia kwa sababu ndiyo iliyofanywa lugha pekee rasmi Ruanda-Urundi. Matokeo yake ni kwamba, “lugha ya Kiswahili, iliyoongezewa na sifa bainifu za utamaduni wa Waswahili, ilianzishwa mjini Bujumbura na wakazi wake wote walizungumza lugha hiyo kama lugha mama”.
Ikumbukwe tu kwamba, wakati huo wa utawala wa Wajerumani kulikuwa na lugha kama tisa ambazo wakoloni hao walizitambua, ya kwanza ikiwa Kijerumani ikifuatiwa na Kiswahili, Kiarabu (katika ukanda wa Pwani), Kirundi, Kinyarwanda, Maa (lugha za jamii za Kimasai), Kisukuma, Kiiraqw na lugha za jamii za Kichaga.
Lakini Kiswahili kimeendelea kutumika jijini Bujumbura tangu wakati huo, ingawa kimepitia changamoto kadhaa. Ni lugha iliyowaunganisha watu wa asili tofauti lakini baadaye ikabadilika na kuwa lugha ya wageni, Waislamu na watu “wasiostaarabika,” lugha hiyo haikuzungumzwa na makundi mbalimbali pekee bali pia ilihusishwa na itikadi mbalimbali za kiisimu na mitazamo asilia.
Ilivyokita mizizi Buyenzi
Wilaya ya Buyenzi ni jumuiya ya kihistoria (ya Mkoa wa Mairie wa Bujumbura magharibi mwa Burundi. Wilaya hii inajulikana kwa urithi wake wa Kiswahili na ushawishi sio tu katika Bujumbura lakini Burundi kwa ujumla. Kuna mitaa 25 ambayo ina namba na siyo majina, kama ilivyo katika Jiji la Tanga.
Historia inaonyesha kuwa, uhusiano wa kibiashara kati ya eneo la Ziwa Tanganyika na wafanyabiashara wa Waswahili wa Bahari ya Hindi katika miaka ya 1830 ulizidi kuwa mkubwa zaidi, na Ujiji, iliyokuwa mwisho wa mojawapo ya njia kuu za msafara wa nchi kavu, ilipata umaarufu haraka. Kupitia maingiliano ya kawaida ya kila siku kati ya wafanyabiashara na wakazi wa eneo hilo, Ziwa Tanganyika polepole likaendelea kuwa “Pwani ya pili ya Uswahilini,” ikichukua sifa nyingi bainifu za Kiswahili, kama vile lugha ya Kiswahili, usanifu na mavazi ya Kiislamu, na Uislamu wenyewe.
Kama makazi ya kwanza ya Waswahili kwa kitongoji hicho mahususi, Buyenzi ni makazi ya Waislamu wengi wa Burundi ambao wengi wao ni wazao wa wafanyabiashara Waswahili kutoka Pwani ya Uswahilini mwanzoni mwa Karne ya 19. Msikiti wa Al Jummaa wa Buyenzi, ulioko kati ya Barabara yaa 12 na 13 hapo Buyenzi, ni msikiti wa pili kwa ukubwa nchini Burundi na unaakisi turathi za Kiislamu za Kiswahili.
Kuzaliwa ‘Mtaa wa Uswahilini’
Ubelgiji ilikabidhiwa udhamini juu ya Ruanda-Urundi baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, wakati Ujerumani iliposhindwa. Sababu kuu iliyowafanya waimarishe sera ya lugha ya Kijerumani ni kwamba Kiswahili kilizungumzwa pia katika Kongo ya Ubelgiji kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika. Ilikuwa vigumu kueleweka kushindwa kuwasiliana kwa Kiswahili, lakini kwa muda, kanuni nyingi mpya zilianza kutumika, na kuathiri sana hali za kijamii, kiuchumi na lugha za wakazi wa Bujumbura. Bujumbura ilizidi kuwa na tabaka huku Wabelgiji wakijaribu kuunda sekta tofauti za kiuchumi na kimaumbile kwa ajili ya makundi mbalimbali ya rangi. Mipaka pia iliwekwa ndani ya mji, kama vile ilivyokuwa kati ya maeneo ya vijijini na mijini.
Kutokana na uhusiano wao na Uislamu, wazungumzaji wa Kiswahili hatimaye walitengwa na mamlaka za Ubelgiji kwa maelezo kwamba Kiswahili kilitumika kama nyenzo ya itikadi wakati wa utawala wa Wajerumani. Ili kutekeleza kwa uwazi mkakati yao, mipaka mipya iliwekwa kati ya makundi ya Kiislamu na yasiyo ya Kiislamu na vile vile kati ya mijini na vijijini. Wengi wanaozungumza Kirundi walipendelewa, wakati Waislamu na Waswahili walio wachache walikusudiwa kufukuzwa nje ya jiji.
Watu waliozungumza Kiswahili walilazimishwa na Wabelgiji kulipa kodi kubwa zaidi, na kuanzia mwaka 1927, Kirundi ndiyo lugha pekee iliyofundishwa shuleni.
Kundi la Waswahili liliathiriwa zaidi na mageuzi ya kielimu yaliyotekelezwa mwaka 1927, ambayo yalisababisha Kanisa Katoliki kuchukua takriban majukumu yote yanayohusiana na elimu na kubadilisha lugha ya kufundishia kutoka Kilatini hadi Kirundi katika shule za msingi na Kifaransa katika elimu ya juu.
Waislamu ambao walikataa kubadili dini na kuwa Wakristo walinyimwa fursa ya kupata elimu na ujuzi ambao serikali ya Ubelgiji na wafanyabiashara walihitaji. Hii pia ilitumika kwa ufundishaji wa ustadi wa ufundi. Kwa hiyo, fani ambazo zingeweza kujifunza bila mafundisho rasmi zilizidi kuwa za kawaida miongoni mwa jamii ya Kiislamu.
Maeneo tofauti ya makazi yaliundwa kando kwa Waafrika wasio Waislamu ambao walikuwa na kazi za kutwa, za mshahara ili “kudhibiti” idadi ya Waafrika. Waswahili wengi hawakuruhusiwa kuishi huko kwa sababu ya kazi zao mbalimbali.
Waasia [na Waarabu] kwa makusudi waliwafukuza Waswahili waliofika baadaye, wasio na uwezo mkubwa nje ya wilaya yenye Waasia wengi (Matongoni) na kuwapeleka katika kitongoji cha jirani kinachojulikana kama Kabondo, utabaka ukazidi kuwa mgumu zaidi.
Kufikia mwisho wa miaka ya 1920, migawanyiko ndani ya wakazi wa Bujumbura na jumuiya zilizogawiwa kwao ilizidi kutamalaki: Wazungu, Waasia, Waswahili, na Waafrika wengine, kila kundi likiwa na ujirani wake, kila moja likiwa na kazi zinazofaa.
Katikati ya miaka ya 1930, maeneo mawili ya ziada yalianzishwa. Moja ilikuwa Buyenzi, kijiji ambacho Waswahili walikianzisha kwa ajili ya Waswahili wenzao waliohamishwa kutoka Kabondo, Mbugani, au Matongoni. Huenda wakazi wengi walizaliwa, walioa, na kuaga dunia katika eneo hilo. Jumuiya nyingine, Belge, ilikuwa karibu na kituo cha mji na wakazi wake walikuwa Wakristo au wanamila. Mara nyingi walikuwa vijana ambao walikuwa wameenda Bujumbura kutafuta kazi, walioa, na kisha mara kwa mara hawakuwarudisha wake na watoto wao Bujumbura.
Kuanzia miaka ya 1950, ikawa kinyume cha sheria kuoa wake wengi katika eneo la Buyenzi, jambo ambalo limesababisha ongezeko la idadi ya wanawake wa Uswahilini ambao hawajaolewa. Serikali pia iliwachukulia kimakosa wanawake hao kwa kuwa bado walikuwa kwenye ndoa zao zisizo halali au makahaba na haikufikiri kuwa kweli hawajaolewa. Ushuru mkubwa unaotozwa kwa wanawake ambao hawajaolewa kwa sababu hiyo ulijulikana kama “kodi ya malaya” na makarani wa Kiswahili.
Prince Louis Rwagasore, kiongozi wa UPRONA na mtoto wa mwami (mfalme wa Urundi), Mwambutsa, alipendwa sana huko Buyenzi. Wakijua kwamba maofisa wa Ubelgiji hawakukubali shughuli zake, Waswahili walimtia moyo aendeleze na walikuwa na shauku ya kumfanyia kampeni. Waswahili walikuwa katikati kabisa ya chama cha Rwagasore. Walitaka uhuru, kupunguzwa kwa kodi kubwa, fursa katika jamii ya Warundi, uwezo wa kujihusisha na shughuli za kibiashara, na uhuru wa kusafiri mashambani kwa sababu walikuwa wamechanganyikiwa. UPRONA iliungwa mkono sana na Waswahili.
Jitihada za Waswahili katika kudai uhuru hatimaye zilipelekea lugha ya Kiswahili kurejeshwa redioni mwaka 1961, licha ya kwamba Kiswahili na wazungumzaji wake walikuwa bado wamekandamizwa. Waswahili walifurahi, lakini Warundi hawakushindwa na lugha hiyo. Hata hivyo, kwa muda, hali za Kiswahili na wazungumzaji wake ziliboreka taratibu. Karangwa alionyesha Burundi kama taifa linalozungumza lugha moja mwaka 1995, huku lugha mbili ikienea miongoni mwa wakazi wa Bujumbura na Kiswahili kikishika nafasi ya pili baada ya Kirundi, mbele ya Kifaransa na Kiingereza.
Matumizi na maarifa ya Kiswahili yamepanuka nchini Burundi kutokana na vita na misukosuko iliyofuata. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wakimbizi waliokimbilia mataifa jirani waling’ang’ana na lugha ya Kiswahili katika harakati hizo ambayo iliwaunganisha na wenzao ama wenyeji wao.
Katika kambi za wakimbizi, lugha hiyo inazungumzwa sana, hasa na vijana. Wakimbizi hawa sasa wanarudi na bado wanazungumza Kiswahili. Serikali ya Burundi pia inaundwa na wengi wao waliokuwa wakimbizi, wanachama waasi, wengi wao walitoka nje ya nchi, na watu wanaozungumza Kiswahili vizuri ambao waliishi katika mataifa yanayozungumza Kiswahili wakati wote wa vita. Wana upendeleo mkubwa zaidi wa kukuza Kiswahili nchini Burundi, na kwa sababu hiyo, wanasiasa wengi leo wanazungumza lugha hiyo.