
Na Mwandishi Wetu
WAKATI Mgombea wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiweka msisitizo wa kudumisha amani katika msimu wa uchaguzi, wadau wa siasa wamesema ni muhimu kila Mtanzania atimize wajibu wake na kufuata matakwa ya sheria ili kuepuka vurugu.
Kwa mujibu wa wadau hao, mustakabali wa amani ya nchi, unajengwa na utii wa sheria za uchaguzi na kuepuka kufuata mkumbo wa wenye nia ovu, hivyo wananchi walizingatie hilo kwa ustawi wa utulivu wa Taifa.
Kauli za wadau hao wa siasa, zinakuja siku mbili baada ya Dkt. Samia kusisitiza kuwa, atailinda amani wakati wa uchaguzi, huku akiwasihi wananchi kufuata utaratibu utakaowekwa, kwa kuhakikisha wanapiga kura na kurudi nyumbani.
“Uchaguzi ni tendo la kidemokrasia, ni watu kwenda kwa utaratibu uliowekwa, kuweka kura zetu rudi nyumbani katulie ili nchi ibaki salama,” amesema Dkt. Samia akiwa Makunduchi visiwani Zanzibar.
Katika msisitizo wake kuhusu hilo, Dkt. Samia alisema matumizi ya silaha si wakati wote yataleta suluhu ya vurugu, ni muhimu amani izingatiwe.
“Si muda wote kushika silaha kunaleta suluhisho, muda wote kushika silaha yoyote, iwe ya moto au ya kimila hakuleti suluhisho la maana. Niwaombe sana wote wanaotusikiliza, amani na utulivu wa nchi yetu ni jambo la muhimu zaidi kuliko mengine yote hasa wakati huu wa uchaguzi,” anasema.
Kauli za wadau
Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Shirikisho la Vijana Tanzania (TYC), Lenin Kazoba alisema uzoefu unaonyesha matumizi ya silaha, mara nyingi yanachochea kuvunjika kwa amani, badala ya kuidumisha.
Kutokana na uhalisia huo, Kazoba alieleza kauli ya Dkt. Samia ni muhimu, inaakisi uhalisia na inapaswa kuzingatiwa na makundi yote wakiwemo vijana, ili kuhakikisha amani inadumishwa nchini.
Ili vyombo vya ulinzi na usalama visilazimike kutumia silaha, alisema wananchi wanapaswa kuzingatia matakwa ya kisheria katika mchakato wa uchaguzi na watu waepuke kufuata mkumbo wa matendo yanayohatarisha amani.
“Kushika silaha ni matokeo ya mambo fulani… fulani…, mara nyingi kama kuna watu wanataka kuleta tatizo, silaha zinashikwa ili kuwakabili. Kwa hiyo tujitahidi kufuata taratibu ili tusilazimishe vyombo vya dola vishike silaha,” amesema Kazoba.
Anasisitiza kila mtu anahitaji amani kuelekea uchaguzi na vijana wanapaswa kuelewa na kushiriki ipasavyo ili nchi ibaki salama, kwa maslahi ya kiuchumi na ustawi wa Taifa kwa ujumla.
“Kwa kuwa mimi ni kiongozi wa vijana, nitahakikisha nadumisha amani kwa kutoa elimu kwa vijana wenzangu kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii kuhakikisha vijana wanalinda amani ya nchi,” alisema.
Anasema kuna mambo mengi yanatokea, iwapo amani itavurugika, hivyo vijana wawe mstari wa mbele kumwelewa Dkt Samia kwa kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kudumisha amani iliyopo.
Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe, amesema kauli hiyo inatia moyo na muhimu zaidi isiishie mdomoni, badala yake iwe kwa vitendo.
“Ni kauli ya kutia moyo, lakini inahitaji vitendo zaidi na ianzie juu kwa kuheshimu zaidi majadiliano kuliko kutumia nguvu,” amesema.
Massawe alisisitiza watu wanapaswa kufahamu kuwa, kipindi cha uchaguzi sio kwamba sheria zinasimama, kila upande utimize haki na wajibu wake ili kuilinda amani.
Kipindi cha uchaguzi, anasema ndicho kipimo sahihi cha ukomavu wa demokrasia ya nchi, hivyo muhimu kila mmoja azingatie matakwa ya sheria ilia mani isiathirike.
Mchambuzi wa masuala ya sheria na siasa, Aloyce Komba anasema kauli hiyo inatoa funzo katika pande mbili, moja ni kwa wananchi kufuata matakwa ya sheria ili kuepuka kuvuruga amani.
Kwa upande mwingine, anasema inatoa funzo kwa vyombo vya dola kutambua ukweli kwamba, matumizi ya silaha hayasaidii kuleta amani, hivyo busara ni muhimu zaidi.
Kwa ujumla, anaeleza suala la kuhakikisha amani inakuwepo ni wajibu wa wananchi wenyewe kwa kuwa wao ndio waliopo katika nafasi ya kuamua nchi itulie au ivurugike kutokana na matendo yao.
Komba anagusia wagombea pia, kuhakikisha wanakubaliana na matokeo katika uchaguzi husika, ili kuepuka kujenga hamasa za chuki na vurugu zitakazochochea uharibifu wa amani nchini.
“Kila mtu awajibike kwa nafasi yake, kama yeye ni Mkuu wa Wilaya yeye ni Mweyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, bila upendeleo amani idumishwe na tutaendelea kuwa salama,” anasema.
Anasema Dkt. Samia anastahili kupongezwa kwa hatua yake ya kukumbushia umuhimu wa amani kwa kuwa anafahamu pasipo amani kuna matokeo hasi lukuki kwa Taifa.
“Mama yetu asingependa kutokee vurugu wakati yeye ni sehemu ya huu uchaguzi, angependa kama atashinda, aongoze vizuri Taifa likiwa shwari muda wote,” anasema.
Kwa upande wa Mchambuzi wa Masuala ya Siasa, Dkt. Hezrone Makundi alisema kwa Taifa la Tanzania, amani ni jambo linaloigusa asili ya nchi.
Kauli yake hiyo, inatokana na kile alichofafanua, waasisi wa Tanzania walijenga msingi wa amani na utulivu katika uasisi wao, hivyo nchi kuwa na amani ni utamaduni wake.
Kwa sababu ya uhalisia huo, anasema kauli ya Dkt Samia inarejea misingi iliyowekwa na waasisi wa Taifa, ili isitokee nchi imeharibika wakati wake.
Hata hivyo, alisema amani ina manufaa mengi na Tanzania imejifunza athari za machafuko kwa kuwa imezungukwa na nchi zilizokosa utulivu.
“Kwa hiyo Tanzania sio mgeni wa masuala ya migogoro kwa sababu imejifunza madhara yake kutoka kwa majirani. Ndiyo maana mkuu wa nchi anasisitiza amani kwa kuwa anajua umuhimu wake,” anasisitiza.


