Wadau kilimo wakuna vichwa uzalishaji ngano ya kutosha

Na Sarah Moses, Dodoma

WIZARA ya Kilimo imeshauriwa kukaa na kuweka mikakati bora na wakulima wa zao la ngano ili kuona namna ya kuzalisha kwa wingi nchini ili kuepuka kuagiza kutoka nje. 

Hayo ameyasema leo jijini Dodoma Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Daniel Mushi, wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Wadau wa Kilimo ulioandaliwa na Jukwaa Huru la Kilimo (ANSAF ).

Amesema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa kwa mwaka Bara la Afrika linatumia Dola za Marekani bilioni 55 kuagiza chakula nje ambapo kwa Tanzania kwa mwaka 2022/23 imetumia Dolla za Marekani  milioni 285 kwaajili ya kuagiza ngano nje ya nchi.

Pamoja na hayo aliwataka wakulima kuchukulia kama fursa kwao changamoto ya kupanda kwa bei za bidhaa za  chakula kwa kuzalisha chakula kwa wingi. 

Amesema kuwa sekta binafsi zinatakiwa kutumia fursa za mkutano wa AGRF ili kusonga mbele katika sekta ya kilimo na mifugo.

“Itakuwa ajabu sana kwa Watanzania kushindwa kutumia fursa hizo wakati mkutano huo ulifanyika nchini na nchi mbalimbali zilihudhuria ikiwamo kutangaza fursa. 

Pamoja na hayo amesema Tanzania inarasilimali kubwa, hivyo Taifa lina uwezo wa kulisha Tanzania na dunia kwa ujumla kutokana na ardhi iliyokuwapo.

Mbali na hilo amesisitiza uwepo wa ubora wa bidhaa ambazo zinazalishwa ili waweze kupata soko la kimataifa kwa urahisi zaidi na kuitangaza nchi.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao Wizara ya Kilimo, Nyasebwa Chimagu, amewataka wakulima kutumia ujuzi, maarifa na matumizi ya teknolojia kuongeza  ubora na tija  katika mazao wanayozalisha. 

“Serikali iko tayari kushirikiana na wadau wowote kwenye sekta ya kilimo ili kuleta mabadiliko kwenye sekta hiyo, hivyo katumieni fursa zilizopo kwenye mifumo ya chakula,” amesema na kuongeza kuwa, 

“Ni lazima tuongeze tija kwenye Kilimo, tunahitaji kupiga hatua mbele kama Rais Samia Suluhu Hassan, alivyoamua kuwekeza katika Kilimo.” 

Awali ameeleza lengo la mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi wa ANSAF, Honest Mseri alisema ni  kujadili fursa zilizopatikana baada ya jukwaa kuu la chakula lililofanyika Septemba 5-9  jijini Dare es Salaam pamoja na kuangalia namna gani vijana na wanawake wanaweza kushiriki kwenye mifumo ya chakula.

“Wakulima wanapaswa kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji yaliyopo kwenye sekta ya Kilimo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *